IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MGOMBEA wa ubunge Jimbo la Musoma Mjini, kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Vicent Nyerere, amesema, akichaguliwa atahamisha duka la kuuzia majeneza lililopo nje ya Hospitali ya Mkoa wa Mara na kujenga duka kubwa la kuuzia dawa ambazo zitauzwa kwa bei nafuu.
“Kwa sababu wameona watu wetu hawaponi wanapoenda hospitali, wameamua kujenga duka la kuuzia majeneza, sasa mkinichagua tu lile duka tutalihamisha na kuweka duka kubwa la dawa ambazo zitauzwa kwa bei nafuu na kutafuta wataalamu ili wagonjwa wanaokwenda kutibiwa wapone na sio wafe,” alisema.
Mgombea huyo aliyekuwa katika Kata ya Kagera pia ameahidi kuongeza magari ya wagonjwa na kuhakikisha yanagawiwa katika kila kata ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
“Ndugu zangu tunayo magari ya wagonjwa ndani ya manispaa yetu lakini hayawanufaishi wagonjwa badala yake yanatumika kwa shughuli za watu binafsi kwa manufaa yao.
“Mkinichagua tu nitajitahidi tuyaongeze kisha kila kata ipate gari moja moja na yatakaa huko huko ili kurahisisha huduma kwa wagonjwa waliozidiwa wanaotakiwa kupelekwa hospitali kuu,” alisema.
Aliwaahidi wakazi wa kata hiyo kuwa atahakikisha anawaunganisha na mjini kwa kutengenezewa barabara ya lami ili kuwarahisishia usafiri ambao utawafanya wagojwa wanaougua na kuwa na hali mbaya wanawahishwa hospitali bila kikwazo chochote.
Aliwataka wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini, kumpigia kura ili aboreshe miundombinu ya maji na kuyauza magari yote ya mradi wa maji.
Alisema , baada ya kuyauza, fedha zitakazopatikana zitatumika kununua mabomba pamoja na pampu za kusukumia maji.
“Endapo mtanipatia ridhaa yenu kwa kunichagua kuwa Mbunge wenu, nitashughulikia matatizo ya maji ambayo yamekuwa tatizo sugu wakati mji wetu umezungukwa na Ziwa Victoria.
Akiwa katika kata hiyo, alimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo kupitia CUF, Gabriel Ocharo kwa kuwa Chadema haikumsimamisha mgombea wake kwa nafasi hiyo ambapo aliwataka wananchi kuunganisha nguvu na kumchagua ili awahudumie.
“Chadema haina ubaguzi baada ya kuona ninyi wananchi mnamkubali sana Ocharo tuliamua kumuachia yeye awe diwani wenu kwa mara nyingine kwa hivyo namuombea kura za ndiyo siku ya tarehe 31 Oktoba mwaka huu mchagueni tena,” alisema.
You Are Here: Home - - 'Nitabadili duka la majeneza liwe la dawa'
0 comments