Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mahakama yafuta hati ya kumkamata Chenge

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter


Andrew Chenge


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wa Kinondoni imefuta hati yake ya kuruhusu kukamatwa kwa mwanasheria mkuu wa zamani, Andrew Chenge iliyotolewa juzi kutokana na mshtakiwa huyo kushindwa kutokea mahakamani.

Hakimu Sundi Fimbo alitoa hati hiyo juzi wakati Chenge, ambaye anatetea kiti chake cha ubunge wa Jimbo la Bariadi Mashariki akiwa kwenye mkutano wa kampeni ambako alipigiwa debe na mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete ambaye kwa sasa yuko mikoa ya Kanda ya Ziwa.
   Lakini mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, David Mwafwimbo aliiambia Mwananchi jana kuwa mdhamini wa Chenge aliibuka juzi akiwa amechelewa na akamuomba hakimu afute hati hiyo na ombi lake likakubaliwa.

"Mdhamini wake anayeitwa Masanja alimrudisha Hakimu Fimbo mahakamani ili kuomba kufutwa kwa kibali cha kumkamata mshtakiwa... ingawa mdhamini huyo alifika mahakamani hapo akiwa amechelewa, alienda kumuomba hakimu afute  hati hiyo na akakubaliwa" alisema Mwafwimbo.

Mwafwimbo alisema baada ya mdhamini huyo kufika, hakimu aliitisha tena jalada hilo na kuifuta amri hiyo ya kukamatwa kwa mshtakiwa huyo.

Chenge alitakiwa kuanza kujitetea jana katika kesi inayomkabili ya kuendesha gari kizembe na kufanya makosa mawili ya kusababisha vifo vya watu wawili na jingine la kuendesha gari bila bima halali.

 Chenge anadaiwa kugonga pikipiki ya maguruduma matatu, maarufu kama Bajaj iliyowabeba wasichana wawili na kusababisha vifo vyao ambavyo kisheria huchukuliwa kama makosa mawili tofauti.

Kutokuwepo kwake kulimfanya Hakimu Fimbo kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 5.
Lakini Zulfa Mfinanga na Herman Meza wanaripoti kutoka Shinyanga kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo lilikuwa halijapokea hati ya kumkamata.

Afisa upelelezi mkoani humo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi((SSP),  Adam Nyakipande alikiri kusikia habari hiyo, lakini akasema walishindwa kuitekeleza kwa kuwa hawakupata kibali cha mahakama hiyo.

"Ninachoweza kusema ni kwamba sisi tunasubiri hati ya kumtia nguvuni... kwa ufupi bado hatujapewa kibali cha kumkamata lakini tukipata tutalifanyia kazi," alisema.

Tags:

0 comments

Post a Comment