Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kada maarufu billionaire wa CCM aichangia CHADEMA sh mil. 100 Makamba: Si dhambi kuchangia Chadema

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MFANYABIASHARA maarufu nchini, Mustapha Jaffar Sabodo, amekuwa mwanachma wa kwanza wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kujitokeza hadharani kukichangia chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kiasi cha sh milioni 100.
Hatua ya kada huyo wa CCM, imekuja wakati Watanzania wakijiandaa na uchaguzi mkuu na kwamba amefungua ukurasa mpya wa kambi ya upinzani nchini kujizatiti na kukabiliana na mikikimikiki ya kampeni za uchaguzi huo zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Sabodo alikabidhi hundi ya kiasi hicho jana nyumbani kwake Upanga jijini Dar es Salaam, kwa Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliyeambatana na viongozi wa kitaifa akiwemo Katibu Mkuu, Dk. Wilibrod Slaa na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Antony Komu.

KATIBU mkuu wa CCM, Yusuph Makamba amesema kitendo cha kada wake maarufu na bilionea Mustafa Sabodo kuichangia Chadema, si dhambi kwa kuwa hata "Waislamu huchangia Wakristo" katika shughuli mbalimbali.

Akikabidhi hundi hiyo, Sabodo alisema licha ya kuwa mwanachama halisi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka mingi, angependa kuona upinzani na demokrasia ya kweli inaimarika nchini huku akisisitiza kuwa CHADEMA ni chama makini.

Sabodo mmoja wa wazee wanaoheshimika katika jamii kutokana na msimamo wake hata kufikia hatua ya kuikosoa serikali pindi anapoona mambo yanakwenda kinyume hasa kukiuka misingi ya utawala bora, iliyojengwa na mwasisi wa taifa hili, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Mimi ni mwanachama wa CCM, lakini napenda kuona demokrasia inakua, huku kambi ya upinzani ikiimarika na kuwa na wabunge wengi bungeni ili kushamirisha maendeleo nchini… leo (jana) nawachangia CHADEMA kwa kuwa natambua umakini wenu katika siasa za hapa nchini na hasa bungeni,” alisema Sabodo.

“Nitaendelea kuwa mwanachma halisi wa CCM na nitaendelea kukiunga mkono, lakini bila upinzani kama CHADEMA ilivyo, CCM italala na hakiwezi kuwa makini,” aliongeza mfanyabiashara huyo ambaye alikuwa kipenzi cha hayati Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake.

Katika kuonyesha kuwa CCM kinahitaji kuwa na chama mbadala, mfanyabishara huyo alisisitiza kuwa kuongezeka kwa wabunge wa upinzani bungeni ni jambo muhimu ili kutoa upinzani kwa CCM na kusukuma maendeleo ya wananchi.

Alisema mbali ya kutoa kiasi hicho, bado ana mpango wa kukichangia fedha zaidi chama hicho, ili kiweze kuimarisha harakati zake za kisiasa na kuahidi kufanya hivyo atakaporejea nchini akitokea India kwenye matibabu.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alishukuru na kutaja msaada huo kuwa ni wa kihistoria katika siasa za vyama vingi nchini.

Mbowe aliainisha kuwa imekuwa ni vigumu kwa wafanyabiashara wakubwa wa kada ya Sabodo, kuchangia kwa uwazi tena kiasi kikubwa cha fedha na kutaka hatua hiyo kuigwa na wafanyabiashara wengine nchini.

“Kwa kweli tunashukuru sana hii ni historia mpya katika siasa za vyama vingi nchini, ni wajibu wa wafanyabiashara wakubwa kuona umuhimu wa kusaidia vyama vyote makini nchini bila ubaguzi wala woga, mzee umeonyesha njia naamini itakuwa ni mfano kwa wengine wenye uwezo,” alisema Mbowe.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Dk. Slaa, alishukuru kwa mchango huo na kusema utatumika kwa kadiri ya vipaumbele vitakavyopangwa kwenye Kamati Kuu ya chama inayotarajiwa kufanyika Julai 20.

Alisema pia fedha hizo zitalenga zaidi kutekeleza mipango endelevu ya kuimarisha chama, kama vile Operesheni Sangara na utekelezaji wa mikakati ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

“Nawaomba Watanzania wengine wa kada na uwezo mbalimbali kuichangia CHADEMA ili kuondokana na ukiritimba wa chama kimoja kwani ni hatari kwa maendeleo na usalama wa nchi kama michango yote ikielekezwa kwa chama tawala pekee.

Natoa mwito kwa vyombo vya dola, kuacha kuwatisha Watanzania wenye mapenzi mema wanaochangia vyama mbadala kama CHADEMA kwani kufanya hivyo ni kuhujumu taifa na kukwamisha maendeleo ya nchi,” alisema Dk. Slaa.
Tags:

0 comments

Post a Comment