Wanaharakati wawasili Uturuki
Wanaharakati hao walilakiwa katika uwanja wa ndege wa Istanbul na wanasiasa kadhaa wa Uturuki wakiongozwa na Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki Bulent Arinc, pamoja na mamia ya wafuasi wao huku baadhi yao wakiimba nyimbo za kuipinga Israel.Ndugu na marafiki wa wanaharakati wa Kituruki wakiwasubiri, jamaa zao hao katika uwanja wa ndege wa Ataturk, Istanbul, mapema leo. Akizungumza na Waandishi wa habari uwanjani hapo, Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki alisema kwa sasa diplomasia imefanikiwa, hata hivyo Israel kwa kufuata sheria itapaswa igharamie mauaji iliyoyafanya. Amesema wote wamelaani shambulio hilo la Israel kwamba halikuwa la haki, na lilikuwa la kikatili na kwamba ni kitendo cha kiharamia. Aidha amefahamisha kuwa ndege hizo pia zilibeba miili ya wanaharakati tisa waliouawa wakati makomando wa Israel walipochukua udhibiti wa meli hiyo ya mizigo katika shambulio la Jumatatu. Israel imewatambua watu wanne kati ya hao waliouawa kuwa ni raia wa Uturuki, lakini haijasema chochote kuhusu kuwatambua na utaifa wao. Kwa upande wa Israel, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu alitetea kitendo cha kuzuiwa kwa meli hiyo.Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Amesema kulikuwa na wanachama wa makundi ya watu wenye msimamo mkali, ambayo yanaunga mkono jumuia za kigaidi za kimataifa na wanaunga mkono kundi la kigaidi linaloitwa Hamas. Ameongeza kuwa Israel inajutia watu kupoteza maisha. lakini kamwe haitaomba msamaha kwa kujilinda wenyewe. Katika hatua nyingine, kiongozi wa shirika la hisani la kiislamu, ambalo liliratibu msafara huo wa baharini wa misaada kuelekea Gaza Bulent Yildirim amesema kupigwa kwa baadhi ya wanajeshi wa Israel kunakoelezwa wakati wa shambulio hilo ilikuwa ni jitihada za kujihami. Mwanaharakati huyo ambaye pia amerudishwa kutoka Israel na wanaharakati wengine, alisema wanaharakati waliwashambulia makomando wa Israel kwa kutumia viti, fimbo ili kujilinda. Wakati huo huo, Israel leo imeupuua uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kutaka kufanyika kwa uchunguzi wa shambulio hilo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Israel Ygal Palmor amesema baadhi ya waliosaini azimio hilo la umoja wa mataifa, kama vile Djibouti, Pakistan, Cuba na Saiud Arabia hazistahili kujiita kwamba ni watetezi wa haki za binadamu. Katika hatua nyingine Mataifa ya kiarabu yatalitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitaka Israel iondoe vizuizi ilivyoweka dhidi ya Gaza. Katibu mkuu wa Umoja wa nchi za Kiarabu Amri Moussa ameyasema hayo leo baada ya mawaziri wa jumuia hiyo kukutana kwa ajili ya kutoa tamko juu ya shambulio hilo lililofanywa na Israel. Amesema kwamba watayataka mataifa yote kudharau vizuizi hivyo vilivyowekwa dhidi ya Gaza na kupeleka misaada katika eneo hilo.
0 comments