Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - CCJ mambo magumu

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter SIKU moja baada ya kuambulia wanachama 13 Dar es Salaam, Chama cha Jamii (CCJ) kimeshindwa kuwasilisha wanachama wake wa mkoa wa Pwani kwa ajili ya uhakiki.

Hali hiyo ilitokea jana katika vijii vya Picha ya Ndege na Kwa Mathias, Kibaha, ambako ndiko uhakiki ulikopangwa kufanyika kwa ajili ya kutambua wanachama wa mkoa huo.

Hatua hiyo pengine inatokana na kauli ya Mwenyekiti wa CCJ, Richard Kiyabo aliyoitoa juzi katika uhakiki wa wanachama wake wa mkoa wa Dar es Salaam uliofanyika katika viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, Dar es Salaam.

Katika kauli hiyo, Kiyabo alisema chama chake hakina imani na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, na hivyo kuhitaji vyama vya hiyari na waangalizi wa kimataifa kushuhudia uhakiki ili kujenga heshima kwa nchi na chama hicho.

Wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema hatua ya CCJ kumkataa Tendwa, inaweza ikawa inaipotezea muda, kwani haitakuwa rahisi kwa ofisi nyingine kuendesha uhakiki huo kwa kuwa kisheria ofisi ya Tendwa ndiyo inahusika.

Kwa hali ya kawaida isingekuwa rahisi pia kwa chama kama hiki kilichoibuka kwa kishindo kukosa mwanachama hata mmoja mkoani Pwani, wakati kikijua kwamba uhakiki utafanyika katika mkoa huo ambao ni jirani na Dar es Salaam, yaliko makao makuu yake.

Hiyo inathibitisha kauli ya Kiyabo ya kususia uhakiki na hivyo inawezekana wanachama wakawa wamekatazwa kujitokeza kuhakikiwa, hali ambayo hata hivyo inakiweka katika hali mbaya ya kukosa usajili wa kudumu.

Timu ya uhakiki huo ikiongozwa na Tendwa, ilipowasili jana katika vijiji hivyo, haikukuta mwanachama, kiongozi wala kuona ofisi ya CCJ, mazingira yanayohatarisha usajili wa kudumu wa cghama hicho kilichopania kushiriki uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

"CCJ wamekuwa wakipiga kelele kwamba ofisi yangu inawahujumu, haitaki kuwahakiki, wanataka kuwahi uchaguzi, sisi tumejitolea kuwahakiki ili wafanye uchaguzi, lakini ninyi ni mashahidi hali halisi ya uhakiki ndiyo hii," alisema Tendwa.

Alisema pamoja na nia njema ya ofisi yake kufanya uhakiki wa wanachama wa CCJ ili kama hesabu yao itatosha waweze kukipa usajili wa kudumu, chama hicho kimerudi nyuma na kushindwa kutoa ushirikiano kwa ofisi yake na kukosa wanachama katika mikoa kama yalivyokuwa makusudio yao.

"Sisi tumejitolea tuwahakiki wafanye uchaguzi, kama wao wanarudi nyuma tena, hiyo ni bahati mbaya kwao, nia yetu ni nzuri, tungekuwa na ushirikiano mzuri na wao tungemaliza hii vizuri, kama kungekuwa na mkwamo wowote tungeshirikiana kutatua matatizo hayo," alisema Tendwa.

Msajili alisema CCJ katika uhakiki wa Dar es Salaam juzi hawakufanikiwa, Pwani kwa Mathias na Picha ya Ndege hawapo kabisa, hakuna mtu yeyote anayewajua, hawana viongozi wala ofisi.

Alipoulizwa kuna haja gani kuendelea na uhakiki katika mikoa mingine wakati hali imeonesha kuwa mbaya, Tendwa alisema tayari walishapanga, baada ya CCJ kuleta barua iliyopanga maeneo ya kufanyiwa uhakiki waliyodai wanayamudu na kusisitiza kuwa lazima yote yahakikiwe.

Alisema leo watakuwa Ifakara mkoani Morogoro kuendelea na uhakiki na baada ya hapo, watakwenda Unguja na hatimaye watatoa taarifa ya uhakiki wao.

"Nimechukua jukumu hili mimi mwenyewe, nitatenda haki na kutimiza wajibu wangu, kama watashindwa kujitokeza na mikoa mingine, CCJ watakuwa wameshindwa kutekeleza wajibu wao kama chama cha siasa," alisema Tendwa.

Juhudi za kumpata Kiyabo azungumzie mazingira ya wanachama wake kutojitokeza Kibaha jana kuhakikiwa, hazikuzaa matunda kutokana na simu yake kuita bila kupokewa.
Tags:

0 comments

Post a Comment