IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
• AFICHUA ALIVYOMBWAGA YUSUF MANJI KORTINI
na Martin Malera, Dodoma
MBUNGE Karatu, Dk. Wilbrod Slaa (CHADEMA), kwa mara nyingi tena ameibua hoja za mashambulizi dhidi ya watuhumiwa wakubwa wa ufisadi na akawataka watu aliowataja kuwamo katika 'Orodha ya Aibu' mwaka 2007 kumbuluza mahakamani.
Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CHADEMA, jana alilieleza Bunge namna Mahakama ya Rufani ilivyompa ushindi katika kesi aliyofunguliwa na mfanyabiashara, Yusuf Manji.
Mbunge huyo machachari na muasisi wa msamiati wa ufisadi katika siasa za hapa nchini, alitoa kauli hiyo wakati akichangia mjadala wa Hotuba ya Makadirio na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, iliyowasilishwa bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Akisimulia, Slaa alisema Manji alimshtaki Mahakama Kuu kutokana na kauli aliyoitoa kwenye gazeti la The Economist” akipinga dhana kwamba mfanyabiashara huyo kuwa nguzo ya uchumi wa taifa.
Dk. Slaa alisema chanzo cha kesi hiyo kilitokana na shirika moja la nchini Uingereza kupanga kufanya mkutano wa uchumi ambao ungefanyika katika Hoteli ya Kempinski mwaka 2007 na kumtangaza Manji kama mmoja wa waandaji wa mkutano huo na alipangwa kuwasilisha mada mojawapo kuhusu hali ya uchumi nchini.
“Mheshimiwa Spika, mwaka 2007 shirika mmoja la Uingereza lilitangaza kufanya mkutano wa uchumi ambao ungefanyika hoteli ya Kempinski na kutangazwa katika gazeti la The Economist.
Waandalizi wa mkutano huo walitangazwa kuwa ni pamoja na Yusuf Manji, ambaye walimtaja kama ni mmoja wa nguzo kubwa za uchumi wa Tanzania, na pia angelikuwa mtoa mada mmojawapo.
“Nilipotakiwa maoni yangu na waandishi wa habari wa gazeti hilo nikapinga sana kuwa Manji hawezi kuwa nguzo ya uchumi wa Tanzania kwa vile anahusishwa na kutuhumiwa mambo mbalimbali katika uchumi wa Tanzania,” alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema kutokana na kauli hiyo, aliyoitoa kwenye gazeti hilo, Yusuf Manji alimfungulia kesi ya madai katika Mahakama Kuu ya Tanzania Civil Case, namba 140 ya mwaka 2008, kwa kosa la kumchafulia jina.
“Mheshimiwa Spika, Nafurahi kuliarifu Bunge lako tukufu, kuwa nimeshinda kesi hiyo. Nashukuru kuwa haki ya Watanzania inalindwa. Katika uamuzi wake, Jaji G.P. Shaidi, aliyotoa Januari 14 mwaka huu, amekataa kesi hiyo katika hatua ya PO.
Kwa maneno yake mwenyewe, Jaji anatamka “ Under the circumastances, of this Case, I hold the view that the plaint as drafted does not fully disclose cause of action against the defendant, I therefore reject it under Order V11 Rule 1 of the Civil Procedure Code,” alisema Dk. Slaa.
“Kwa ushindi huo, ninapenda kuwasisitiza Watanzania wawe majasiri kulinda heshima ya nchi yetu, kulinda rasilimali za taifa hili kwa gharama yoyote, na nina hakika tukisimamia ukweli, Mungu atalinda taifa lake kwa njia ya majasiri wachache. Ninaipongeza pia mahakama kwa kusimamia ukweli na haki,” alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa alikuwa akisikilizwa kwa utulivu mkubwa na wabunge, huku wale wa kambi ya upinzani wakipiga makofi kumshangilia, ambapo aliwataka wote aliowataja kwenye orodha ya mafisadi katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye Viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke jijini Dar es Salaam, wamfungulie kesi haraka kama walivyoahidi.
“Mheshimiwa Spika, mwaka wa 2007 mimi pamoja na wenzangu na kwa kushirikiana na wabunge wa Kambi ya Upinzani pale Mwembe Yanga, tulitoa ’List of Shame’ iliyokuwa yenye majina ya watu tuliowatuhumu kuhusika na ufisadi mkubwa katika nchi yetu.
Miongoni mwa ufisadi ule ni uliofanyika ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT). Kwa kuwa baadhi ya kesi ziko mahakamani sitaki kuzungumzia zilizoko huko.
Kuhusu rushwa na ubadhirifu nchini, Dk. Slaa alisema mambo hayo yamelisumbua taifa hadi sasa, lakini wapo watu wachache wanaotaka mjadala dhidi ya ufisadi ukome na badala yake tuzungumzie maendeleo.
“Ukweli ni kwamba huwezi kuwa na maendeleo kama rushwa na ufisadi havitapigwa vita kwa hali na mali. Iwapo fedha za wananchi walipa kodi watu wachache wakazitumia kwa njia ya kifisadi, shule haziwezi kujengwa, zahanati hazitajengwa wala hazitapata dawa, barabara nazo hazitajengwa.
“Ni kwa msingi huo, tunaoamini kuwa ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma tunashikia bango kuwa suala la ufisadi ni lazima serikali ichukue hatua madhubuti,” alisisitiza.
Mbunge huyo aliibua hoja aliyoiasisi ya ufisadi uliofanyika kupitia Kampuni ya Deep Green Finance Company Ltd, ambayo ilisajiliwa Machi, 18 2004.
“Mheshimiwa Spika, ndani ya Bunge hili tukufu kambi ya upinzani imeendelea mwaka hadi mwaka kuuliza maswali ambayo hayajapata majibu. Mwaka huu ninarudia tena, kuuliza na kutaka maelezo ya kina kuhusu ufisadi uliofanyika kupitia Kampuni ya Deep Green Finance Company Ltd, ambayo ilisajiliwa Machi 18, 2004 kwa taarifa za Brela wanahisa waanzilishi wakiwa ni Mawakili Protase R.G. Ishengoma na Stella Ndikimi wa Kampuni ya IMMA Advocates,
“…Mheshimiwa Spika, mawakili hao walihamisha hisa zao kwa kampuni ya Needbank Ltd na Nedbank Africa Investment Ltd Aprili 15, 2005. Mei 1, 2004 siku ya Sikukuu (ya wafanyakazi), Kampuni hiyo ilifungua Akaunti benki ya NBC, Corporate Branch, Akaunti na 011103025840 na haikuingiza hata senti moja katika akaunti hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
“Serikali imekataa kujibu hoja hizi, na Bunge hili na Watanzania tunahitaji kujua kampuni hii ni ya nani, kwa dhahiri siyo ya kijeshi, na hivyo hakuna usiri wowote,” alisisitiza mbunge huyo.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kampuni ya pili ambayo kambi ya upinzani inataka kujua ukweli ni kampuni ya Tangold ambayo ilisajiliwa katika kisiwa cha Mauritius Aprili 5, 2005 ikiwa na hati ya usajili na 553334 na kupata Global Business Licence (C2/ GBL), Aprili 08 mwaka huo huo.
Kampuni hiyo pia ilipata hati ya kutimiza masharti hapa nchini Februari 20, 2006. Hata hivyo Mhe. Spika, taarifa zilizoko ni kuwa Tangold imekuwa na akaunti NBC Corporate Branch, no. 0lll03024840 iliyofunguliwa Januari mosi, 2003, yaani miaka miwili kabla ya kampuni hiyo haijasajiliwa Mauritius na takriban miaka minne tangu imepata hati ya ‘Kutimiza Masharti’ Tanzania.
“Mheshimiwa Spika, serikali inaweza kukataa kujibu maswali haya, inaweza kutumia ubabe, lakini kuna siku itafika taifa haliwezi kukaa kimya, majibu lazima yatapatikana tu!” alisisitiza.
Mbunge huyo alimbana Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa safari hii lazima atoe majibu ya maswali hayo, kwani ndani ya Bunge hilo, aliwahi kukataa kutoa majibu yanayohusu Meremeta, lakini kambi ya upinzani haitachoka kuingiza ndani ya Bunge.
“Mheshimiwa Spika, narudia tena, ni lazima serikali ilieleze Bunge kwa niaba ya Watanzania wote undani wote kuhusu kampuni ya Kagoda na hatua zipi imechukua au inafikiria kuchukua dhidi ya kampuni na watendaji wake na au watendaji na viongozi wa serikali waliohusika angalau hatua za kiutawala na au kinidhamu.
Hiyo pia ni kwa watendaji wake ambao labda hawakuwa makini wakati kampuni ya Kagoda iliposajiliwa, jambo linaloleteleza kuwa vigumu kwa kampuni hii kujulikana hasa ni mali ya nani, iwapo hivyo ndivyo ilivyo,” alisema.
Kuhusu ufisadi kupitia kashfa ya rada, mbunge huyo alisema kambi ya upinzani inaona fahari kuwa baada ya miaka tisa tangu walipoiibua bungeni na kuamua kutoka nje, serikali imekiri na sasa imetuma maafisa wake kwenda kudai chenji.
“Miaka tisa baadaye, kambi ya upinzani inaona fahari kubwa, tulichokisimamia siyo tu kimeelekea kuthibitika lakini imekuwa ni hadithi dunia nzima na imehusishwa na kitendo kikubwa cha ufisadi au rushwa au wizi wa mali ya umma.
“Ufisadi huo umejadiliwa ndani ya Bunge la Uingereza (House Commons) mara kadhaa na uchunguzi kuanzishwa na Shirika la Upelelezi la Uingereza la Serious Fraud Office (SFO).
“Kambi ya Upinzani inayo furaha ya pekee kusikia kuwa serikali iliyokuwa imekanusha katakata kuwa hakuna ufisadi wa aina hiyo, ndio inayotuma wataalam wake kwenda kudai mgawo wa serikali ya Tanzania baada ya serikali ya Uingereza kutamka kuwa itatoa mgawo huo kwa NGOs.”
Dk. Slaa alimtaka Waziri Pinda wakati wa kuhitimisha mjadala wa hotuba yake, kutoa majibu kwa nini serikali haijachukua hatua yoyote dhidi ya wahusika ambao wanajulikana.
You Are Here: Home - - Slaa atikisa Bunge
0 comments