Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kilango amvaa Pinda • AONYA IKO SIKU DAMU ITAMWAGIKA

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MBUNGE wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela, amesema iko siku damu itamwagika katika ardhi ya Same kama Waziri Mkuu Mizengo Pinda ataendelea kukaa kimya kwa gazeti moja (jina tunalo), kuendelea kutoa taarifa za uongo za jimbo hilo.
Kilango alisema kuwa gazeti hilo ambalo amelituhumu kwa kutumiwa na mpinzani wake, (Vuvuzela), aliyetangaza nia ya kuwania ubunge wa jimbo hilo, limekuwa likiandika habari za kumchafua pamoja na kukejeli juhudi za wananchi za kujikomboa kiuchumi.
Akizungumza bungeni jana huku akiwa amelishikilia gazeti hilo, Kilango alisema wiki iliyopita aliwasilisha malalamiko yake kwa Waziri Mkuu Pinda ili ayatolee tamko lakini kiongozi huyo mkuu wa shughuli za serikali bungeni, alishindwa kutoa tamko.
“Waziri Mkuu unayapuuzia mambo haya, lakini napenda kukuambia kuwa huku mbele yatakuwa na madhara zaidi na tunaweza kushuhudia umwagaji wa damu,” alisema mbunge huyo.
Kilango kama ilivyo kawaida yake ya kuongea kwa sauti kali na ya juu, alisema gazeti hilo wiki hii limekejeli juhudi zake na za wananchi wa Same ambao wameamua kujenga kiwanda kidogo cha kusindika tangawizi.
Alisema gazeti hilo limeandika kuwa kiwanda hicho ni kibanda cha kuku kisicho na kuku ndani yake.
Alisema anasikitishwa na waandishi wa gazeti hilo ambao hawajafanya utafiti wa kile wanachokiandika kwa sababu mkataba wa uwekaji wa mitambo ya kiwanda hicho, ulisainiwa Mei mwaka huu kati ya Halmashauri ya Same na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).
Huku akionyesha mkataba huo, Kilango alisema ujenzi wa kiwanda hicho utagharimu zaidi ya sh milioni 88 na kinatarajia kukabidhiwa mikononi mwao, Oktoba 4.
Aliongeza kuwa fedha za mitambo na ujenzi wa kiwanda hicho, zilipatikana katika harambee iliyohudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete ambapo kiasi cha sh milioni 300, zilipatikana.
Alibainisha kuwa ameshafanya utafiti wa mtu anayemchafua katika gazeti hilo na anamuomba apambane naye kwa kutumia hoja badala ya kuchafuana kwenye magazeti.
Alisema ana ushahidi wa CD unaoonyesha kuwa mgombea huyo anazungumza na waandishi wa habari ambao mara nyingi wamekuwa wakiandika habari za kumchafua.
“Ukitaka kumtongoza mwanamke, usianze kumtoa kasoro kuwa ana makengeza, nawaomba wale wanotangaza nia tupambane kwa hoja si kuchafuana kupitia magazetini,” alisema.
Alisema yeyote mwenye kutangaza nia ya kuwania jimbo ni vema akaacha kuziponda kazi zilizofanywa na mbunge aliye madarakani kama wanavyofanya baadhi ya watu.
Aliongeza kuwa fedha na fitna zisizokuwa na mipaka zinaweza zikasababisha vurugu miongoni mwa jamii.
Kilango alibainisha kuwa yeye si mwanasiasa legelege kama anavyodhani mpinzani wake, ndiyo maana amejikuta akifanya mbinu chafu za kutaka kumng’oa madarakani.
Wiki iliyopita alipokuwa akichangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kilango alitoa malalamiko kama hayo ya kuchafuliwa na gazeti hilo na kumwomba Waziri Mkuu Pinda atolee kauli, lakini hakupata majibu.
Tags:

0 comments

Post a Comment