IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAKATI harakati za kuwania urais Serikali ya Muungano na Zanzibar zikipamba moto, mgombea Dk. Mohamed Gharib Billal anayewania kumrithi Rais Abeid Aman Karume, amekuwa hashikiki kutokana na kuungwa mkono na wananchi wengi wa Zanzibar, wakiwemo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Tanzania Daima Jumatano, limebaini.
Duru za kisiasa kutoka Zanzibar zinasema licha ya Dk. Billal kuwa na umri mkubwa kuliko wagombea wote waliokwishajitokeza hadi sasa, Waziri Kiongozi huyo mstaafu, anaonekana kuungwa mkono zaidi kutokana na kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Zanzibar.
Mbali ya Dk. Bilal, wengine waliochukua fomu juzi ni Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzinar, Shamsi Vuai Nahodha, Balozi Ali Karume na Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna.
Katika kinyanganyiro hicho, yumo pia Makamu wa Rais wa Serikali ya Muungano, Dk. Ali Mohammed Shein, Hamad Bakari Mshindo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohamed Aboud.
Wengine wanaotarajia kuchukua fomu leo ni pamoja na aliyekuwa mshauri wa Rais, Dk. Salmin Amour, upande wa uchumi na michezo, Mohamed Raza, Haruna Ali Suleiman na Mohamed Yusuf.
Sababu zinazotajwa na wachambuzi wa mambo ya siasa waliozungumza na Tanzania Daima Jumatano ni kwamba Dk. Bilal anaungwa mkono na wengi kwani anaonekana kama majeruhi wa kisiasa hasa baada ya kuenguliwa kuwania nafasi hiyo mwaka 2000, licha ya kumshinda Rais Karume kwenye kura za maoni Zanzibar.
Dk. Bilal aliwania nafasi hiyo mwaka 2000, lakini NEC ya CCM ilimpitisha Rais Amani Abeid Karume, licha ya Dk. Bilal kumshinda kwenye uteuzi wa kikao cha Kamati Maalum ya NEC Zanzibar.
Mwaka 2005, Dk. Bilal aliwania tena kiti hicho na kugoma kuondoa jina lake kwenye kikao cha Kamati Maalum ya ZEC, Zanzibar, ili kumpisha Rais Karume amalize muda wake, lakini aliamua kuliondoa mjini Dodoma baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kitendo cha Rais Karume kumwacha Dk. Bilal nje ya serikali yake kwa miaka kumi, kinaelezwa na wachambuzi wa mambo ya siasa kwamba safari hii kimeongeza kura za huruma kwa kundi la kada huyo.
Nguvu za kundi la Dk. Bilal zinatokana na kuungwa mkono na kundi la Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma, mwenye maskani yake eneo la Migombani, mjini Zanzibar.
Vyanzo vyetu vya habari vinasema Dk. Bilal anadaiwa kuwa na idadi kubwa ya kura za wajumbe wa NEC, hali inayomweka kwenye nafasi nzuri ya kupitishwa kuwa mgombea wa nafasi hiyo mwaka huu.
Habari zinasema kuwa ili kujihakikishia ushindi, kundi la Dk. Bilal limepanga kuibua kashfa dhidi ya Dk. Shein ambalo nalo linapewa nafasi kubwa kutokana na kuungwa mkono na Rais Aman Karume pamoja na vyombo vya dola.
Moja ya mbinu chafu inayotumika na mahasimu wa kisiasa wa Dk. Shein ni pamoja na kuzungumzia hoja ya matabaka na asili za watu watokao Pemba, Ngazija, Tumbatu, Makunduchi na kwingineko.
Hoja hiyo imepangwa kutumika kama silaha ya kisiasa katika harakati za kutafuta kuwa wagombea wa chama hicho mwaka 2010.
“Ukiangalia hali ilivyo Zanzibar, Dk. Bilali ana zaidi ya nusu ya kura za wajumbe wa NEC watakaopitisha jina la mgombea urais Zanzibar. Na kama Rais Kikwete asipofanya kazi ya ziada kumsaidia Shein, Dk. Bilali anaweza akashinda kutokana na ushawishi alionao kisiasa visiwani Zanzibar,” alisema mmoja wa wajumbe NEC.
Habari zaidi ambazo gazeti hili imezipata, zinasema kuwa kutokana na nguvu alizonazo Dk. Bilal, kuna mkakati wa kumpoza kwa kumpa nafasi ya Makamu wa Rais wa Muungano ili nafasi ya urais Zanzibar, iende kwa Dk. Shein anayeungwa mkono hata na Chama cha Wananchi (CUF), kutokana na msimamo wake wa kuzibeba hoja za Serikali ya Maridhiano.
Kundi lingine linaloonekana kuwa na nguvu ni la mwanasiasa machachari wa visiwani humo, Ali Juma Shamuhuna, ambaye ni Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar.
Shamuhuna anaokena kuwa na nguvu zaidi kwa sasa baada ya kuonyesha msimamo wake ambao umekuwa ukitofautiana na viongozi wenzake wengi ndani ya chama chake, kuhusu masuala yanayoihusu Zanzibar.
Hatma ya wagombea wa urais Zanzibar, itajulikana Julai 11 wakati wa mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC), unaotarajiwa kufanyika mjini Dodoma na kufuatiwa na mkutano mkuu wa taifa, unaotarajiwa kufanyika Julai 12 kwa ajili ya kupitisha jina la Rais Jakaya Kikwete, anayetarajiwa kuwa mgombea pekee wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano.
You Are Here: Home - - Dk. Bilal hashikiki Zanzibar • MKAKATI WA KUMPOZA WAANDALIWA TANZANIA BARA
0 comments