IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
ZAIDI ya watanzania 100 wamefungwa nchini Iran kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki na Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mohammed Mzale, alisema hayo jana wakati akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu madai ya kuwapo watanzania nchini Iran wanaotamani kurudi nyumbani lakini hawana nauli.
Inadaiwa kuwa watanzania hao wamekuwa wakiteseka baada ya kutoka jela kwa kukosa nauli ya kurejea nchini.
Alisema, baada ya kupata malalamiko hayo, waliyafanyia kazi na kugundua kuwa takwimu za watanzania waliotoka jela Iran ni kati ya 10 na 12 na si wengi kama ilivyodaiwa.
“Si kweli kuwa wamekosa nauli bali wanaendelea na shughuli zao na kama hawana nauli kuna utaratibu wa kuwasiliana na balozi zetu na kwa kushirikiana na ndugu zao nchini tunaangalia jinsi ya kuwarejesha na hii si kwa Iran tu bali nchi zote,” alisema Balozi Mzale.
Naye Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi anaripoti kutoka Tabora, kwamba Polisi mkoani humo inashikilia watu wawili akiwamo raia wa Oman kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya Heroin.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Liberatus Barlow, aliwataja waliokamatwa kuwa ni Mbaraka Hemed (34) wa Oman na Mohammed Sharifu (41) Mtanzania mwenye asili ya kiarabu.
Walikamatwa Igunga baada ya raia wema kuwaeleza Polisi kuhusu kuwapo kwa watuhumiwa hao kwenye gari aina ya Toyota Chaser namba T 676 ANM huku wakijidunga sindano zenye dawa hizo.
Kutoka Morogoro, Agnes Haule, anaripoti kwamba wanawake wawili wa Kenya, wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuwanywesha dawa zinazodhaniwa kuwa za kulevya, wanaume wawili na kuwasababishia kupoteza fahamu na kulazwa hospitalini.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye, alisema watu hao walifanya kitendo hicho Juni 19 mwaka huu saa 12.15 asubuhi katika nyumba ya kulala wageni ya Baraka, Kichangani.
Alitaja wanawake hao kuwa ni Rose Muthoni (32) na Marysia Njeka (30) wote wakazi wa Nairobi. Andengenye alisema wanawake hao waliwanywesha dawa zinazodhaniwa ni za kulevya wanaume wawili Inspekta Victor Mchauru (48) ambaye ni askari Magereza na aliyejulikana kwa jina moja la Julius.
Kamanda Andengenye alisema baada ya unyama huo, wanawake hao waliwaibia vitu mbalimbali zikiwamo nguo, pete za ndoa na simu za mkononi ambavyo vyote kwa pamoja thamani yake bado haijajulikana.
Wanawake hao wanashikiliwa Polisi na upelelezi unaendelea na watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
You Are Here: Home - - Watanzania 100 wafungwa Iran
0 comments