Ahmadinejad akosoa vikwazo dhidi ya Iran
Rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad ameionya Jumuiya ya Kimataifa kuwa, nchi yake itafutilia mbali mazungumzo yote kuhusiana na mradi wake wa nyuklia- iwapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaiwekea Iran vikwazo vipya.
Kitisho hiki cha vikwazo vipya dhidi ya Iran kinakuja wakati baraza hilo la usalama lenye wanachama 15 linajitayarisha kukaa katika kikao kingine cha faragha, kuzungumzia azimio la nne la vikwazo dhidi ya Iran. Kikao hiki kinafanyika baada ya wanachama 15 wa Baraza hilo kutofautiana jana iwapo Jamhuri hiyo ya Kiislamu inafaa kuwekewa vikwazo vipya.
Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad.Wanachama wa kudumu wa baraza hilo- Uingereza, Ufaransa, China, Urusi na Marekani ndio waasisi wa azimio hilo- ambalo linatarajiwa kupigiwa kura kabla ya kumalizika wiki hii.
Akiwa ziarani nchini Uturuki, katika mkutano wa kiusalama unaoyaleta pamoja mataifa ya bara Asia- Rais Mahmoud Ahmedinejad alikuwa na onyo kwa Marekani na washirika wake.
'' Utawala wa Marekani na washirika wake watakuwa wanakosea sana iwapo, wanadhani, pande moja watashika fimbo ya vikwazo, na pande nyingine watakaa katika meza ya mazungumzo kuzungumza nasi- hilo halitowezekana. Alisema Rais Ahmedinejad.
Ahmedinejad aliongeza kusema, Iran haitosita kuzungumza na mtu yeyote ule- alimuradi kuna usawa na kuheshimiana- ila yule ambaye anataka mazungumzo na utawala huo wa Jamhuri ya Kiislamu lakini akitumia mbinu za kiburi basi anaelewa vyema matokeo yake.
Waziri Mkuu wa Urusi Vladmir Puttin ambaye pia anahudhuria mkutano huo wa kikanda mjini Istanbul- amesema atakutana kwa mazungumzo na Rais Ahmedineajd leo, kabla ya kikao hicho cha faragha.
Waziri Mkuu wa Urusi, Vladimir Putin.Putin pia alikuwa mwepesi wa kuwaambia waandishi wa habari kwamba- vikwazo hivyo visiwe vikali mno. Kwa upande wake Ahmedinajad ameyaambia mataifa ya Magharibi yasipuuzilie mbali ule mkataba wa kusafirisha madini yake ya Uranium nje ya nchi ulioafikiwa kwa juhudi za Uturuki na Brazil.
'' Maafikiano hayo yalikuwa fursa nzuri kwa Marekani na washirika wake, matumaini yangu ni kwamba watatumia vizuri fursa hiyo, kwani nafasi kama hizo hazipatikani mara kwa mara, asliema Ahmedinejad.
Marekani na mataifa ya Magharibi yametoa majibu baridi kuhusiana na mkataba huo- ambao Iran ilikubali itayatupa madini yake ya Uranium kilogramu 1,200 nchini Uturuki yarutubishwe na kisha yarejeshwe nchini Iran wayatumie kama nishati katika vinu vyake.
Iwapo Iran itawekewa vikwazo vipya, hili litakuwa kosa kubwa- Alisema Ahmedinejad. Marekani imekuwa mstari wa mbele kupigia debe Iran iwekewe vikwazo vipya, kutokana na shaka shaka zake kuhusu madhumuni ya mradi wa Nyuklia wa Iran.
0 comments