IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Salma Said, Zanzibar na Boniface Meena
MAKAMU wa Rais, Dk Ali Mohammed Shein ametajwa kuwa ni mmoja wa wanachama wa CCM wanaotarajiwa kuchukua fomu za kuwania urais Zanzibar Juni 21 mwaka huu.Kwa muda mrefu, Dk Shein amekuwa akiombwa na rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume achukue fomu ya kuwania nafasi hiyo kubwa ya kisiasa visiwani humo. Rais Karume anamaliza vipindi vyake viwili vya urais mwaka huu baada ya kuingia Ikulu mwaka 1995.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini Dar es salaam na Zanzibar, Dk Shein alikuwepo visiwani humo na kufanya mazungumzo maalumu na Rais Karume na habari zinasema kuwa kiongozi huyo wa Zanzibar alimuomba Dk Shein kukubali kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo moto.
Hamu ya Rais Karume kumtaka Dk Shein kuwa mrithi wake inatokana na makamu huyo wa rais kuonekana ana msimamo wa wastani katika siasa za Zanzibar zisizo na chuki za Upemba na Unguja, huku akionekana kuwa hana makundi kulinganisha na wagombea wengine.
Sababu nyingine ni Dk Shein kuonyesha dhamira ya kutaka kuendeleza maridhiano yaliyofikiwa Novemba 5 mwaka jana kati ya Rais Karume na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Hata hivyo, msemaji wa makamu wa rais, Said Ameir alisema hajui lolote kuhusu taarifa hizo kwa kuwa yuko likizo.
"Hakuna taarifa kama hizo. Mimi niko likizo na sijui lolote kuhusu hilo... kama mmepata taarifa na mnataka kushirikisha watu sawa, lakini sijui lolote," alisema Ameir.
Mwandishi wa habari wa makamu wa rais, Penzi Nyamungumi alisema hajawahi kusikia hilo kwa kuwa hata Dk Shein mwenyewe hajawahi kutamka lolote kuhusu hilo.
"Sijui lolote ndio nasikia kutoka kwako; sina uhakika na hilo kwa kuwa makamu wa rais hajawahi kutamka kuhusu urais wa Zanzibar," alisema Nyamungumi.
Lakini chanzo chetu kimesema awali, Dk Shein alikuwa mgumu kukubali ombi la Rais Karume kutokana na wana CCM wahafidhina wanaotoa salamu za chuki dhidi ya wana CCM wenye asili ya Pemba wanaowatishia kwamba kamwe wasijaribu kugusa fomu za kuwania urais.
“Kwanza Dk Shein alisita kwa sababu anawajua vizuri wana-CCM wenzake hasa hawa wa Zanzibar ambao wanajifanya wao ndio wana mapinduzi na wao ndio wenye haki ya kuchukua fomu. Wanataka watu kutoka Pemba wasijaribu kuchukua fomu na wameanza kutoa vitisho kwa hiyo kama mnavyomjua dokta huwa hapendi mazonge.
Amekuwa na hofu kwa sababu anataka heshima yake ibaki, lakini baada ya kuelezwa mengi amekubali na inshaallah tutamshindikiza akachukue fomu,” kilisema chanzo chatu.
Kujitokeza kwa Dk Shein kunaelezwa kupata baraka zote za Rais Karume na baadhi ya viongozi wengine wa serikali ya Zanzibar na ile Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Mtu ambaye hana upande hadi sasa kati ya wanaotaka kuwania urais wa Zanzibar ni Dk Shein; kwanza anaweza kufanya kazi na mtu yeyote, hana chuki na watu na tabia yake ya upole inachangia kuonyesha uadilifu wake.
''Katika suala la maridhiano anaonyesha kuliunga mkono tofauti na wenzake ambao wanasema wazi wazi kupitia wapambe wao kwamba wakiingia watalitupilia mbali,” kilieleza chanzo hicho.
Kabla ya kuwa makamu wa rais, Dk Shein aliwahi kuwania uwakilishi wa jimbo la Mkanyageni mwaka 2000 kisiwani Pemba Kijiji ambacho amezaliwa. Kiti hicho kinashikiliwa na mwakilishi wa CUF Haji Faki Shaali.
Kuingia kwa Dk Shein katika kinyanganyiro cha urais wa Zanzibar kutasababisha mfadhaiko kwa baadhi ya watu wanaotaka kuwania nafasi hiyo kuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na rekodi zake za uadilifu na nidhamu ndani ya chama kikongwe cha CCM.
Pia kutaibua changamnoto mpya kwenye siasa za Zanzibar ambako tayari wanachama wa CCM wameshaanza kupigana vijembe kuhusu nia ya baadhi yao kuwania urais. Katika siasa za Zanzibar, watu kutoka Pemba wamekuwa wakilaumu ndani ya CCM kuwa wanabaguliwa.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wanaotaka kuwania kinyanyanyiro cha urais wa Zanzibar wameelezwa kutaka kumuunga mkono Dk Shein iwapo atatangaza nia yake ya kutaka kuchukua fomu ya kuwania urais wa Zanzibar.
Viongozi hao wameelezwa kuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia mambo ya Muungano, Mohammed Seif Khatib anayetokea Bambi Unguja na Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud Mohamamed ambaye anatokea Wawi Kisiwani Pemba.
Wengine wanaotajwa kutaka kuwania urais wa Zanzibar ni Dk Mohamed Gharib Bilal ambaye aliwahi kuwa waziri kiongozi wa SMZ kipindi cha utawala wa Dk Salmin Amour Juma.
Wengine wanaoelezwa kuwa wanataka nafasi hiyo ni Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Ali Karume, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman na Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna.
Takriban wajumbe wote wanaotajwa kutaka kuingia katika kinyang'anyiro hicho hawajaeleza waziwazi nia zao, lakini kila mmoja alisema ikifika wakati atatangaza na baadhi yao wamesema wiki ijayo watatangaza nia zao za kutaka kuchukua fomu muda utakapofika.
Wakati hayo yakitarajiwa kufanyika wiki ijayo, tayari CCM imewataka watendaji wake, wakiwemo makatibu wa itikadi na uenezi kutenda haki kwa wagombea wote watakaojitokeza katika zoezi hilo pamoja na ubunge na uwakilishi katika kura ya maoni na kuacha tabia ya kuwabeba wagombea.
Akizungumza katika mafunzo ya siku mbili ya watendaji wa chama, katibu wa idara ya itikadi na uenezi ya kamati maalumu ya halmashauri kuu ya CCM upande wa Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema sio busara kwa sasa watendaji hao kuwabeba wagombea kabla ya kutangaza nia zao na kuwataka kujiepushe na vitendo vya kupokea au kutoa rushwa.
You Are Here: Home - - Dk Shein atajwa kujitosa kinyang'anyiro cha urais Zanzibar
0 comments