**Ni mwenyekiti na naibu katibu wake JOTO la kisiasa ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM sasa limefikia nyuzi 100, baada ya Mwenyekiti wake Hamad Yusuf Masauni na Naibu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo visiwani Zanzibar, Nassoro Moyo, kuamua kujiuzulu. Ramadhan Semtawa, Dar na Leon Bahati, Iringa Tangu juzi, vijana hao wa CCM wamejichimbia mjini Iringa kwa ajili ya mkutano huo muhimu wa baraza kuu, ambao ulitanguliwa na semina na kamati ya utekelezaji lakini ukiwa umegubikwa na msuguano ambao unakiweka chama katika wakati mgumu katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba. Kabla ya kwenda Iringa, tayari wajumbe walishaingia kwenye vita baada ya kusambazwa waraka uliokuwa ukimtaka Masauni ajiuzulu huku wajumbe wengine kutoka kambi ya mwenyekiti huyo nao wakimtaka Moyo aachie ngazi. Hadi jana jioni, hali ilikuwa ni ya wasiwasi baada ya kufanyika kikao cha kamati ya utekelezaji ambacho inaelezwa Moyo aliandika mwenyewe barua ya kujiuzulu kwa maslahi ya umoja huo. Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, Moyo aliandika barua hiyo ikiwa ni sehemu ya kunusuru jumuiya katika kipindi hiki ambacho imekumbwa na mparaganyiko mkubwa. Wakati wote jioni, ukumbi wa Siasa ni Kilimo ulikuwa umedhibitiwa vema na polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakishirikaina na wana usalama wengine. Habari zinasema Masauni alijiuzulu saa mbili usiku baada ya kubanwa na katibu wa CCM, Yusuf Makamba ajiuzulu kwa hiari yake dhidi ya kashfa inayomkabili ya kughushi umri wakati anagombea nafasi hiyo mwaka 2008. Hali tete ilianza kwenye kikao cha sekretarieti ya umoja huo ambayo iliwajadili viongozi hao wawili kwa muda mrefu, kuliko hata ilivyokuwa imekadiriwa kwa mkutano huo kufanyika. Habari tulizozipata wakati tukienda mitamboni saa 3.00 usiku jana zilisema mara baada ya kumalizika kwa Kamati ya Utekelezaji, Makamba alimwita kwa mara nyingine Masauni na kumshinikiza kujiuzulu. Hata hivyo, vyanzo vya habari vilisema kuwa hata Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa CCM alikuwa amebariki viongozi hao kujiuzulu. Kutokana kujiuzulu kwa Masauni sasa nafasi itakaimiwa na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa. Taarifa zaidi zilidai kuwa baada ya wajumbe wa Baraza Kuu kupata habari kuwa Masauni aliamua kujiuzulu wengi wao walionekana wakiwa kimya huku wakitafakari mustakabali wa jumuiya hiyo.Mkutano huo ulianza saa 2:30 asubuhi na ulipaswa uwe umekamilika kabla ya saa 3:30 asubuhi ili kupeleka ajenda zinazotakiwa kujadiliwa na kikao cha baraza kuu, kwenye kikao kingine cha kamati ya utekelezaji ili zipitishwe. Awali vyanzo vyetu vya habari, vilieleza kuwa kuchelewa kukamilishwa kwa kikao hicho kulitokana na mvutano mkubwa ulioibuka kutokana na pande mbili kupingana, kila moja ikotoa sababu za kutaka mmoja kati ya viongozi hao wawili ajiuzulu. Baraza kuu lilikuwa lianze saa 4:00, lakini kutokana na kikao cha sekretarieti kumalizika saa 6:20, iliamuliwa kuwa kikao cha baraza kianze saa 8:00 na kuwataka wajumbe wajiandae, wakati huo ndipo wajumbe wa kamati ya utekelezaji wakakutana. Mkutano wa kamati hiyo ulipokea taarifa za sekretarieti juu ya mada za kujadiliwa kwenye baraza kuu na kabla ya kuanza kwa kikao, Moyo aliwasilisha barua ya kukubali kujiuzulu kupisha uchunguzi wa kile kinachoitwa ni kuvuruga chama. Katika tuhuma hizo, Moyo anatajwa kuzusha vurugu ndani ya umoja huo, akidaiwa kushiriki kusambaza nyaraka za kumpinga Masauni. Mvutano mkali pia ulielezwa kuzuka ndani ya kamati ya utekelezaji na hadi saa 12:00 jioni kikao hicho kilikuwa hakijamalizika na taarifa zikawepo kwamba baraza hilo lianze kwa semina ndogo kuhusu mada ya ugonjwa wa Ukimwi ili kuweka sawa mambo. Taarifa nyingine zinadai kwamba, kundi linalopinga Masauni kulazimishwa kujiuzulu liliibuka na hoja kwamba kuna kundi la mafisadi ambao wanataka aondolewe kwenye madaraka yao ili wamuweke mtu wao ambaye atajenga mazingira mazuri ya ushindi wa rais kwa mwaka 2015. Hadi jana mchana ajenda za kikao cha baraza kuu zilikuwa bado hazijajulikana huku baadhi ya wajumbe, akiwemo Makamba akiachia jukumu hilo viongozi wa jumuiya hiyo. Makamba alipoulizwa alichukuaje kitendo cha kutojulikana kwa ajenda za mkutano saa chache kabla ya baraza kuanza kikao, alijibu: "Mimi ni mjumbe tu, ajenda wanapanga wenyewe watendaji, muulize katibu mkuu wa UVCCM." Lakini, vyanzo vingine vilidokeza kwamba juzi usiku Makamba alimtaka Masauni ajiuzulu, hatua ambayo mwenyekiti huyo aliipinga na kutaka kwanza arudi kwa wapiga kura wake akawaeleze. Kuhusu madai kuwa wanachama wanaomuunga mkono Masauni walipanga kuandamana, Makamba alisema:" Kwanza waandamane kwenda wapi? Mimi nasisitiza siwezi kumwambia mtu ajiuzulu kwa tuhuma... halafu wanamtaja na Ridhiwani Kikwete, (mtoto wa rais)... yeye ana mamlaka gani kumshinikiza Masauni ajiuzulu? "Huku ni kumwonea tu kijana huyu na kutaka kumhusisha katika mambo ambayo hahusiki wala hajatenda. Waache kumchafua kijana wa watu, sijakuwa naye popote kushinikiza mtu ajiuzulu. Ni uongo mtupu. "Ridhiwan ni mjumbe kama nilivyo mimi; sisi sote ni wajumbe tu ndugu yangu; tuna mamlaka gani ya kumshinikiza mtu ajiuzulu. Waache fitna; waache kumchafua; kijana wa watu hajatenda chochote." Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, jana jioni wajumbe 38 wa Baraza Kuu kutoka Zanzibar walitanda eneo la ukumbi wa mikutano wakitaka kumuona kwanza mwenyekiti wao Masauni akiwa amekalia kiti, ndipo waingie ukumbini. |
You Are Here: Home - - Vigogo UVCCM wajiuzulu
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments