IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah, amesema kifungo cha miaka miwili alichohukumiwa wiki hii aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba, ni matunda ya kazi iliyofanywa na taasisi yake.
Hoseah alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa wakaguzi na wadhibiti wa fedha za serikali uliokuwa katika siku yake ya pili, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo aliitaja kesi ya Liyumba aliyepatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka, kuwa ni kielelezo cha kazi njema inayofanywa na TAKUKURU ambayo imekuwa ikikabiliwa na lawama nyingi.
Mbali ya hilo, Hoseah alisema tayari taasisi yake imeshakamilisha uchunguzi wa kesi kubwa mbili za rushwa za vigogo ambazo ameziwakilisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kwa ajili ya kuzitolea uamuzi.
Alisema licha ya kesi hizo, ofisi yake iko hatua za mwisho kukamilisha uchunguzi wa kesi nyingine moja kubwa ya rushwa kabla ya kuikabidhi kwa DPP ili aandae utaratibu wa kuwafungulia mashtaka wahusika.
Alisema uchunguzi wa kesi hizo umetokana na ripoti ya ubadhirifu wa fedha za umma iliyowasilishwa kwake na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Alisema muda wowote, kuanzia sasa, DPP anatarajiwa kutoa uamuzi juu ya kesi hizo ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
“Tunatarajia kumkabidhi DPP kesi hii kwa ajili ya uamuzi wa mwisho… katika hili kumbukeni kwamba ofisi yangu imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na ofisi ya CAG ili kuhakikisha tunadhibiti vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma,” alisema Hoseah.
Akitoa ufafanuzi kuhusu madai ya kuwa TAKUKURU imeshindwa kuchunguza kesi za vigogo wa ufisadi na badala yake kuwashughulikia wala rushwa wadogo, Dk. Hoseah alisema ofisi yake haimuogopi mtu yeyote katika kutimiza wajibu wake kwa vile taasisi hiyo ni huru.
Alisema uchunguzi wa kesi za vigogo wala rushwa sio kazi rahisi kama jamii inavyodhani, kwa kuwa wanakutana na vikwazo vikubwa.
Alisema inapotokea kukawa na madai ya kuwapo kwa fedha zilizosafirishwa nje ya nchi, TAKUKURU hulazimika kuwasiliana na nchi husika ili kupata ushahidi uliokamilika.
“Ni kazi ngumu sana kuwachunguza vigogo, kuna wakati unakuta fedha ambazo unazitafutia ushahidi zimesafirishwa zaidi ya nchi moja na unalazimika kuwasiliana na nchi hizo ili zikupe ushirikiano na wakati mwingine unawaandikia barua kwa Kingereza wao wanakutaka uandike kwa lugha yao, jambo linalochangia ucheleweshaji wa kesi hizo,” alisema Hoseah.
“Baada ya kupata mawasiliano nao tunalazimika kutoa taarifa kwa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria kwa ajili ya kupata msaada wa kisheria na ndipo tunapoweza kutuma wapelelezi wetu kwa ajili ya kupata vielelezo kwa kesi husika. Kwa hiyo sio kazi rahisi na ya muda mfupi kama jamii inavyodhani,” aliongeza.
Hossea alisema mchakato huo unasababisha kesi nyingi za vigogo kuchelewa upelelezi, kulinganisha na zile za watu wadogo ambao ushahidi wake upo ndani, na hivyo kuzua maneno kwa jamii kuwa TAKUKURU inawalinda baadhi ya vigogo jambo ambalo alisema halina ukweli ndani yake.
Akijibu madai kuwa taasisi hiyo, haiko huru katika kutekeleza majukumu yake kutokana na kuwa chini ya ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Hoseah alisema tatizo sio kuwa chini ya mtu au taasisi, kinachotakiwa ni kuwa na uwezo kuchunguza kesi yoyote.
Aidha, alisifu mafanikio yaliyoanza kupatikana katika kesi ambazo taasisi hiyo, imechunguza kwa wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria, akitolea mfano kesi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, aliyefungwa miaka miwili Jumatatu wiki hii na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka.
You Are Here: Home - - Hoseah ashangilia Liyumba kufungwa
0 comments