Friday, 28 May 2010 09:09 |
MKURUGENZI wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah jana amesema kesi za ufisadi zitakazofikishwa mahakamani hivi karibuni ni nzito na zitastua wengi. Dk Hoseah pia alisema uchunguzi wa kesi mbili kati ya hizo umeshakamilika na zitaanza kunguruma mahakamani mwezi ujao na kwamba kesi hizo tatu zimeibuliwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Kigogo huyo wa Takukuru, ambaye alikuwa akizungumzia uhusiano wa ofisi yake na CAG kwenye mkutano uliohusisha wakaguzi wa mahesabu na wanasiasa kutoka nchi mbalimbali, alisema tayari majalada ya mashauri hayo matatu yameshawasilishwa ofisi ya mwendesha mashtaka huyo kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria. “Tumemaliza kuyafanyia uchunguzi mashauri matatu mazito ya ubadhilifu na matumizi mabaya ya fedha uliofanywa serikalini ambayo yaliibuliwa na CAG,” alisema Dk Hoseah. “Kesi hizo ni nzito na zitastua," alisema Dk Hoseah akionekana kujiamini. Awali Dk Hoseah hakutaka kufafanua juu ya kesi hizo, lakini alipopigiwa simu baadaye alisema uchunguzi uliokamilika ni wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo na ile ya sakata la mbolea ya Kigoma. Katika sakata hilo la Bagamoyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitimua watumishi wanne vigogo baada ya CAG kubaini ubadhirifu wa zaidi ya Sh900 milioni za miradi, lakini kauli ya Dk Hoseah inamaanisha kuwa kuna mengi makubwa yataibuliwa kwenye kashfa hiyo, ambayo mmoja wa mawaziri wa serikali ya awamu ya nne anatajwa kuhusika. Akizungumza katika mkutano huo uliowakutanisha wakaguzi wa mahesabu pamoja na wanasiasa kutoka ndani na nje ya nchi, Dk Hoseah alisema rushwa katika manunuzi ya umma inasababishwa na serikali kutokana na kutokuwa makini katika kufuatilia manunuzi hayo. “Mfano ni gari aina ya shangingi; Tanzania italinunua kwa Sh100 milioni, lakini Uganda na hata Zambia wao watanunua chini ya hapo au hata kwa asilimia 50 ya bei hiyo," alisema. “Hapa unaona jinsi serikali isivyokuwa makini katika kusimamia manunuzi ya vitu vya umma.” Akizungumzia kuhusu rushwa kubwa, Dk Hoseah alisema taasisi yake imekumbana na changamoto kubwa ya kuwafungulia kesi watu wanaojihusisha na vitendo hivyo. Alifafanua wengi wa wanaojihusisha na rushwa kubwa, wana mbinu nyingi ikiwemo ya kuhifadhi fedha nje ya nchini na mara nyingi huzihamisha kwenda nchi nyingine. “Mfano baada ya mtu kula rushwa, fedha ataweka katika benki ya Barclays nchini kisha atazihamishia Barclays ya Uingereza kisha ataziamishia katika Barclays iliyopo nchini Shelisheli au Italia," alifafanua. “Ili ufanikishe kumtia nguvuni ni lazima ushirikiane na Wizara ya Mambo ya Nje na pia upate ushirikiano wa karibu na nchi husika na mara nyingi majibu kutoka katika nchi hizo unaweza kuyapata baada ya miezi sita.” Alisema kutokana na hali hiyo, Takukuru hulazimika kuchukua muda mrefu kukamilisha uchunguzi dhidi ya rushwa kubwa, tofauti na ilivyo kwa rushwa ndogo na za kawaida. Akizungumzia mfumo ambao unaiweka Takukuru chini ofisi ya rais na hivyo kuifanya isiwe na uhuru katika uwajibikaji, Dk Hoseah alisema hiyo si hoja ya msingi na kuwa taasisi hiyo inafanya kazi katika mazingira huru na yanayofuata sheria, kanuni na utaratibu uliopo. “Kwangu mimi kuwa huru ni kufanya kazi katika mazingira huru na kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo pasipo kuingiliwa. Hali hiyo ndiyo iliyopo Takukuru,” alisema. |
You Are Here: Home - - Dk Hoseah: Kesi tatu zitakazotikisa zinakuja
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments