Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mpendazoe aonywa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemuonya aliyekuwa Mbunge wa Kishapu, Fred Mpendazoe, ambaye siku za hivi karibuni alijiunga na Chama Cha Jamii (CCJ), kuacha kutoa kauli za kejeli dhidi ya chama hicho.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Mpendazoe kukabidhiwa rasmi kadi ya uanachama ya CCJ katika viwanja vya Mwembeyanga juzi mjini Dar es Salaam na kuhutubia mkutano wa hadhara.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, alisema:
“Siwezi kubishana na Mpendazoe; alikuwa mwenzetu, aliondoka… sasa mimi nibishane naye nini? Sina muda huo kwani kazi iliyo mbele yangu ni utekelezaji wa ilani ya chama tu.”

Alisema kauli zinazotolewa na Mpendazoe kuwa CCM imekuwa kinara wa rushwa na kushindwa kuwapatia Watanzania maisha bora, hazina ushahidi wowote kwani chama chake kinakubalika kwa wananchi.

“Huyu anasema CCM inakula rushwa… alete ushahidi wake, chama hiki kinakubalika kwa wananchi, utakumbuka mwaka jana katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa tuliibuka na ushindi wa asilimia 91… jamani hapa hatukubaliki kweli?!” alihoji Makamba.

Alisema tafiti za kitaalam zilizofanywa na Taasisi za Utafiti ya Synovet na RIDET zinaonyesha CCM inakubalika kwa wananchi huku Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, bado anakubalika zaidi kwa Watanzania.

“Nawaomba wana CCM mpuuzeni huyu, madai haya si ya msingi… sisi tunazungumza kwa tafiti zinazofanywa na wataalam wetu jamani,” alisema Makamba.

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi, Kapteni John Chiligati, alimtaka Mpendazoe aendelee kuzungumza tu kwa vile hana jambo jipya huko aliko.

“Yeye aendelee tu kuzungumza hana jambo jipya… hatuwezi kubishana naye tuna kazi moja tu ya kutekeleza-ilani,” alisema Kapteni Chiligati.

Alisema CCM ilishamtakia kila heri baada ya kujivua uanachama wa chama hicho na kwenda CCJ mwezi uliopita.

“Hatutaki kuingia kwenye malumbano na mtu, tunakabiliwa na majukumu mengi…aendelee tu hatuna muda wa kumfuatilia mtu muda huu,” alisema Kapteni Chiligati.

Juzi akihutubia mkutano wa hadhara, Mpendazoe alisema tatizo la matumizi makubwa ya rushwa na kutumia fedha nyingi katika uchaguzi limo ndani ya CCM, hivyo kuweka sheria kwa ajili ya kupunguza gharama hizo ni jambo ambalo haliwezekani.

Alisema Rais Jakaya Kikwete, siku za nyuma aliwahi kukiri kuwa matumizi ya fedha katika uchaguzi ni makubwa na kwamba ataweka mkakati wa kutafuta mbinu ya kumaliza tatizo hilo, lakini badala yake CCM wanatafuta sh bilioni 40!

Mpendazoe ambaye alipewa kadi namba 004408, alidai CCM ni chama kinachoongozwa kisanii na kudanganya watu, lakini umefika wakati wa Watanzania kubadilika na kutafuta chama mbadala.

Alisema kitendo cha kuendelea kutumia fedha nyingi kwa ajili ya uchaguzi ndiyo sababu serikali imekuwa ikishindwa kusaidia kutatua kero muhimu za wananchi na kutumia muda mwingi kuweka mikakati ya kununua uongozi.
Tags:

0 comments

Post a Comment