UDASA YAANDAA TAMKO
Na Boniface Meena
WAKATI wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), wakajiandaa kutoa tamko lao kuhusu ajira ya Profesa Mwesiga Baregu, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine (SAUT), kipo tayari kumwajiri mwanazuoni huyo.
Makamu mkuu wa chuo hicho, Dk Charles Kitima aliliambia gazeti hili jana kuwa Profesa Baregu, ambaye amejikita kwenye sayansi ya jamii na uhusiano wa kimataifa, ni msomi anayekubalika na kwamba chuo chake kinamhitaji hata leo kama atakuwa tayari kuajiriwa.
"Aje hata kesho (leo) kwa kuwa tunamhitaji na taaluma yake tunaihitaji. Kujiunga na chama cha siasa si uasi kwa kuwa kila mtu ni mwanachama wa chama cha siasa lakini, kinachotakiwa ni kutoingiza siasa kwenye kazi," alisema Dk Kitima.
Alisema SAUT ingependa kuwa na mwanazuoni huyo kwa kuwa inaamini kuwa hawezi kuingiza siasa darasani.
Alisema kutokana na suala la Baregu kuisumbua serikali ni muhimu sasa ikaamua kujiondoa katika ajira za waalimu wa vyuo vikuu kwa kuwa vyuo hivyo ni mali ya wananchi.
Alisema kuwa hilo ni muhimu kwa kuwa wanasiasa wanapenda wawe wanasikilizwa zaidi kuliko watu wengine na kuacha wenye taaluma wakififia na taaluma ambazo zinahitajika.
Serikali ilitangaza kuwa imeamua kutomuongezea mkataba Prof Baregu kwa mara ya nne kwa sababu hahitajiki tena baada ya kustaafu na kupewa mikataba ya ziada mitatu na pia kwa sababu sasa anashikilia wadhifa wa juu kwenye chama cha siasa, kitu ambacho ni kinyume na sheria za ajira za utumishi wa umma.
Katika hatua nyingine Chama cha Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udassa) wamesema kitendo cha serikali kutoa tamko linalohusu ajira ya Profesa Mwesiga Baregu tu ni kumtisha, hivyo watatoa tamko lao Januari 22 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Udassa, Dk Dalmas Nyaoro alisema kuwa inashangaza kuona jinsi serikali ilivyomkamia Prof Baregu hadi kuamua kutoa tamko hadharani.
"Tamko la serikali linamtaja Baregu tu, huko ni kumtisha tunataka serikali itueleze inataka aende wapi wakati kuna upungufu wa wanataaluma hapa," alisema Dk Nyaoro.
Dk Nyaoro alisema idara ina upungufu na ndiyo maana Baregu anahitajika na upungufu huo usipofanyiwa kazi, wanafunzi wanapata wakati mgumu.
Katika tamko la serikali lililosomwa na Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia ajira ya mwanazuoni huyo maarufu nchini ilikoma alipostaafu kwa mujibu wa sheria mwaka 1999.
Waziri Ghasia alisema ameamua kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, kutokana na taarifa nyingi kuhoji kwa nini Baregu hakupewa mkataba mpya wa ajira kama ilivyokuwa kwa wahadhiri wengine waliostaafu kama yeye.
Alisema kuwa pamoja kuwa si sera ya serikali kuajiri wastaafu katika utumishi wa umma, serikali imekuwa ikitoa ajira kwa mikataba ili wasaidie kutoa huduma wakati serikali ikifanya jitihada za kujaza nafasi zilizoachwa wazi.
Ghasia alisema uamuzi wa serikali kuajiri wastaafu si endelevu, kwa kuwa nafasi wanazotumikia kwa mikataba zinatakiwa zijazwe na wataalam wapya ili waendeleze utumishi wa umma hapo baadaye.
"Kwa kutumia utaratibu huu, Baregu alistaafu kazi kwa mujibu wa sheria Februari 24 mwaka 1999 akiwa na umri wa miaka 55 na baada ya kustaafu, aliajiriwa kwa mkataba na UDSM mara tatu na mkataba wa mwisho ulimalizika Januari mwaka 2008," alisema Ghasia.
0 comments