Wazanzibari waombea dua Marodhiano ya Rais Karume, Seif
Waumini wa dini ya kiislamu waliokusanyika katika uwanja wa Maisara mjini Zanzibar jana, kusali na kuomba dua ya uchaguzi mkuu na kuwaombea viongozi wa kisiasa Rais Abeid Karume na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad waliokubaliana kuleta amani visiwani humo |
Salma Said, Zanzibar
MISIKITI yote jana ilifungwa ili kupisha swala ya pamoja ya Ijumaa iliyoandaliwa maalumu kumuombea rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na katibu mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad ili wakamilishe dhamira yao ya kuwaunganisha Wazanzibari.
Maombi hayo, ambayo yalifanyika kwenye viwanja vya Maisara mjini Unguja baada ya kufungwa kwa misikiti yote, yalikuwa yawashirikishe viongozi hao wawili, lakini Rais Karume hakuweza kuhudhuria.
Mufti mkuu wa Zanzibar, Sheikh Harith Bin Khelef ndiye aliyeiwakilisha serikali katika swala hiyo.
Maombi yalianza kwa dua ya kuiombea Zanzibar kuelekea uchaguzi mkuu na baadaye kuwaombea viongozi hao wawili waliokutana mara kadhaa faragha kujadili mustakabali wa Zanzibar.
Rais Karume na Maalim Seif wamekuwa na mikutano ambayo imeelezewa kuwa ina lengo la kuinusuru Zanzibar dhidi ya machafuko yanayotokana na chaguzi na kuzika tofauti zao za kisiasa.
Swala hiyo ilifanyika kando ya nyumba ya Fatma Karume, ambaye ni mjane wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.
Dua hiyo iliandaliwa na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya juhudi zinazolenga kuweka umoja wa Wazanzibari na kuwaomba viongozi hao wawili wasirudi nyuma katika kuendeleza umoja huo na mshikamano waliouanzisha.
Waandaaji wa swala hiyo walisema kutohudhuria kwa Karume si tatizo katika ibada hiyo kwa kuwa lengo la dua ni kuwaombea viongozi hao wakuu wa vyama vya siasa walete umoja na mshikamano.
Chini ya jua kali, Waislamu hao walionekana kuzingatia maelelezo yaliokuwa yakitolewa na viongozi wa dini yaliyokuwa yakisisitiza msamaha miongoni mwao na kuendeleza mikakati ya kuleta umoja na maridhiano.
Akitoa risala kwenye swala hiyo, Amiri wa Jumuiya ya Uamsho, Sheikh Azzan Khalid Hamdan alisema sala hiyo haikulenga moja kwa moja siasa isipokuwa kutokana na umuhimu wa tukio la maridhiano na kwa kuwa Zanzibar waliamua kutumia fursa hiyo kuwataka wananchi bila kujali itikadi za kisiasa, kusameheana ili kuleta umoja na mshikamano.
Hamdan alisema umma uliokusanyika unawaangalia viongozi hao wakuu ili kuona kama wana dhamira ya kweli ya kurejesha umoja.
"Kama wana dhamira ya kweli umma wote utakuwa pamoja nao na iwapo hawana dhamira ya kweli basi mzigo huo wataubeba wenyewe," alisema.
Alisema mazungumzo ya Rais Karume na Seif yametoa matumaini makubwa kwa wananchi kuweza kujenga uaminifu miongoni mwao hivyo kuna kila sababu ya maridhiano hayo kuungawa mkono ili kuwaunganisha Wazanzibari ambao kwa miaka kadhaa, wamekuwa wakifarikiana kwa sababu zisizo na msingi.
"Viongozi, umma huu wote unakutazameni nyinyi ukitegemea mafanikio ya kuiokoa Zanzibar na machafuko na migogoro isiyokwisha," alisema.
"Mkiwa na nia safi na dhamira ya kweli basi kwa umma huu wa leo tunainua mikono yetu juu kumuomba Mwenyeenzi Mungu afanikishe na kuyafanya mepesi yaliokusudiwa katika maridhiano yaliofikiwa na ikiwa kuna uzito wowote, basi Mungu ayafanye mapesi inshallah," alisema Sheikh Hamdan katika maombi yake.
Awali akiongoza ibada hiyo, Sheikh Farid Hadi Ahmed alisema Waislamu wanapaswa kuanza maisha mapya na kusahau ya nyuma kwani wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakipata shida inayotokana na mifarakano yenye itikadi za vyama.
"Ikitokea viongozi leo wanakaa pamoja ni faraja kubwa ambayo inafaa kuendelezwa," alisema.
Katika mawaidha yake mufti mkuu wa Zanzibar, Sheikh Harith Bin Khelef alisema dua ni kitu muhimu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Aliwaomba Wazanzibari kuendeleza mshikamano huo ili uchuguzi ufanyike kwa uhuru na amani.
Mratibu wa shughuli hiyo, Sheikh Mohammed Suleiman alisema matukio matatu yaliyotokea Zanzibar hivi karibuni; kupatwa kwa mwezi, kuzaliwa watoto walioungana na kupatwa kwa jua ni ishara njema kwa siku za usoni.
Aliwataka wananchi kusoma na kufanya ibada kwa kumuelekea Mwenyenzi Mungu ili kuinusuru nchi na mabalaa huku akiwataka kuachana na maasi kama dhuruma, rushwa, uzinzi na matumizi ya dawa za kulevya.
Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliliambia gazeti hili baadaye kuwa alihudhuria ibada hiyo baada ya kupewa mwaliko.
Alisema Zanzibar inahitaji rehema za Mungu kufanikisha kufanikisha mchakato wa kuleta amani ya kweli na kuwaunganisha Wazanzibari bila ya kujali tofauti zao za kisiasa.
Katika hatua nyingine, CUF imeandaa maandamano makubwa ya kutoa ujumbe kama huo wa kutaka uchaguzi usogezwe mbele ili kutoa nafasi ya kujenga misingi ya maridhiano.
0 comments