CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimependekeza uchaguzi mkuu wa mwaka huu uahirishwe visiwani hapa ili Rais Amani Abeid Karume aongoze kwa miaka miwili zaidi.
Tamko hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ikiwa ni siku tatu tangu Rais Karume kutangaza kutokuwa na nia ya kubadilisha katiba na kuongeza kipindi kingine cha uongozi.
Akiwasilisha mada kuhusu mustakabali wa Zanzibar na maridhiano, Maalim Seif alisema Rais Karume anapaswa kubaki madarakani kwa muda huo, ili akamilishe kazi ya kumaliza tofauti za kisiasa aliyoanza kuifanya.
“Baada ya kutafakari, mimi binafsi naungana na wale wanaotoa wito wa kuchukuliwa hatua ya kusogezwa mbele kidogo uchaguzi mkuu wa Zanzibar mwaka huu. Aongezewe kipindi cha kati ya mwaka mmoja au miaka miwili, ili kutoa nafasi kwa Rais Karume ya kukamilisha kazi njema aliyoianza,” alisema Maalim Seif.
Katika kongamano hilo, Maalim Seif alisema Zanzibar haiwezi kukwepa kufanyika uchaguzi, lakini kabla ya uchaguzi lazima kujengwe misingi madhubuti ya maridhiano, ili kuwe na uchaguzi huru na wa haki.
“Hatuwezi kukwepa uchaguzi maana ndiyo njia ya demokrasia ya kuwapata viongozi wetu, lakini tumeshafanya chaguzi saba za vyama vingi Zanzibar na zote zimeshindwa kuleta umoja wa Wazanzibari,” alisema.
Hata hivyo, alisema maridhiano yaliyofikiwa kati yake na Karume kuna baadhi ya watu wameyapokea kwa kinyongo kutokana na malengo yao ya kisiasa ya kurithi nafasi ya urais baada ya Rais Karume kumaliza muda wake.
“Hatuwezi kukwepa, ukweli ni kwamba wapo watu wanaokodolea macho fursa ya kutaka kuchukua madaraka ya juu ya Zanzibar ya nafasi ya urais, ambao wamekuwa hawayapendi maridhiano tuliyofikia,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, aliongeza kuwa watu hao wamekuwa wakieneza taarifa za uongo kwamba maridhiano waliyokubaliana kati yake na Rais Karume yamelenga kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Watu wa aina hii hawawezi kusaidia Zanzibar na kwa hakika ni maadui wa umoja wa Wazanzibari,” alisema Maalim Seif na kuwataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa tayari kufanikisha azma ya mabadiliko ya katiba kumuwezesha Rais Karume kubakia madarakani.
Pamoja na Rais Karume kutoa msimamo wake kuwa anakamilisha kipindi chake cha uongozi na hana nia ya kuongeza kipindi kingine, Maalim Seif alimuomba akubaliane na matakwa ya wanaotaka aongeze muda wa kubakia madarakani.
Hata hivyo, katika kongamano hilo lililohudhuriwa na wanachama wa CUF, Maalim Seif hakueleza idadi ya Wazanzibari wanaotaka katiba kufanyiwa mabadiliko ili Rais Karume aongezewe muda isipokuwa alisema milango ya neema kwa Zanzibar itafunguka na kuwa kituo cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki.
“Natoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa pande zote mbili, serikali na upinzani, kulitafakari hili na kutupa Wazanzibari kile tunachotaka. Naomba Wazanzibari tuungane pamoja kumtaka Rais Amani aweke upande dhamira yake ya kutokuwa na nia ya kuongeza muda,” alisema Maalim Seif.
Hata hivyo, wajumbe katika mkutano huo walisema suala la kubadilisha Katiba ya Zanzibar na kumuwezesha Rais Karume kubakia madarakani bado lina mtihani mgumu kwa vile linahusu Katiba ya Muungano na ya chama tawala - CCM.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona, Mohammed Kassim Abdallah alisema mabadiliko ya katiba yafanyike haraka ili Rais Karume aendelee kubakia madarakani na uchaguzi wa mwaka huu uahirishwe.
Katika kongamano hilo mwanasheria Ali Omar Juma alisema kwamba suala la Zanzibar kubadilisha katiba kumuwezesha Rais Karume kubakia madarakani haliwezekani bila ya kupata baraka ya Serikali ya Muungano na chama chake.
Akichangia mada hiyo alisema Zanzibar haina mamalaka kamili kama nchi na ni tofauti na Rwanda au Burundi, hivyo si rahisi kubadilisha katiba bila ya kuhusisha Katiba ya Muungano na ya CCM, kwa vile Zanzibar imepoteza mamlaka yake baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Hekaheka za kutaka Rais Karume aongezewe muda zilianzishwa kwa mara ya kwanza Zanzibar na baadhi ya wazee wa CCM na hivi karibuni Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) na Jumuiya ya Mihadhara Zanzibar (UAMSHO), zimekuwa zikiendesha kampeni licha ya CCM kupinga suala hilo.
Wakati huohuo, Marekani imesema iwapo Zanzibar inataka kuepuka vurugu za uchaguzi kabla na baada ya uchaguzi hakuna budi kuwepo serikali ya mseto.
Taarifa ya Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa anataka kuona hatua imechukuliwa hasa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ili kuepuka machafuko ya kisiasa kama yaliyotokea katika uchaguzi wa 2000 na ule wa 2005.
Balozi Lenhardt akiitolea mfano nchi yake alisema Katiba ya Marekani imegawanya madaraka kati ya serikali ya shirikisho na serikali kuu, jambo linalofanya kuwepo uwezekano wa kugawanywa kwa madaraka katika mihimili ya Baraza la Mawaziri, Mahakama na Bunge.
“Mwaka huu unaanza na matumaini kwamba kuna ishara kwa Wazanzibar kuelewana, kuweka mazingira mapya ya kisiasa katika misingi ya kuheshimiana... kuanzisha taasisi imara za uchaguzi kati ya waunga mikono wa vyama vikuu vya upinzani na kutafuta ya kuuondoa mfumo wa sasa wa ‘mshindi kuchukua vyote’ na kuunda serikali ya pamoja kati ya vyama vikuu,” alisema balozi huyo.
Alipendekeza hayo huku akiweka maanani kwamba wafuasi wa vyama vya CCM na CUF visiwani Zanzibar idadi yao inakaribiana na kwamba iwapo kukitokea upande unaopinga kushindwa, madhara yake huwa ni kuwepo kwa mvutano na kutoweka kwa amani.
Alieleza ushirikiano wa serikali yake na watu wa Tanzania si kwa kuunga mkono chama chochote cha siasa na kwa hali hiyo Marekani iko tayari kuunga mkono serikali itakayochaguliwa ila iwe katika uchaguzi ulio wa uwazi, huru na halali.
“Tunashauri mabadiliko na tunatazamia hatua madhubuti kuchukuliwa katika uchaguzi, tusingependa kuona tena matukio ya kusikitisha kama ilivyokuwa Zanzibar mwaka 2000 na 2005.
“Nina imani kuwa Wazanzibar watafikia makubaliano na kushirikiana madaraka kwa manufaa ya Wazanzibar. Nina matumanini kwamba mazungumzo yanayoendelea sasa yatafikiwa makubaliano yatakayoleta uchaguzi huru, haki na amani,” alisisitiza.
Alisema Zanzibar kwa sasa haihitaji mtafaruku wowote wa kisiasa na kwa maslahi ya Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla uchaguzi mkuu wa mwaka huu hauna budi kuwepo makubaliano visiwani humo.
0 comments