You Are Here: Home - - WABUNGE wengi wamepinga mapendekezo ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ya kutaka kuwepo ukomo wa ubunge.
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Hata hivyo baadhi yao wanaunga mkono pendekezo hilo wakisema litaondoa baadhi yao kuhodhi nafasi kama mali binafsi na wengine wakisema demokrasia iachwe mikononi mwa wananchi...
Wasomi na wanasiasa wengine hususan kutoka vyama vya upinzani wamesema tatizo la kuwepo maneno na kutafutana uchawi wakati wa mchakato wa kuwania ubunge, utatuzi wake si ukomo, bali namna wanavyochaguliwa kutokana na baadhi kutoa rushwa.
Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango -Malecela, amepinga pendekezo la Waziri Mkuu kwamba muda wa kuwa Mbunge usizidi miaka 15.
Mbunge huyo amesema, wabunge wasiwekewe kikomo, wananchi ndiyo wanaostahili kuamua na kwamba, umri usiwe kikwazo.
Mbunge wa Kwela, Chrisant Mzindakaya (CCM) na Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti (CCM) ni miongoni mwa wabunge waliokaa muda mrefu bungeni ambao hivi karibuni walitamka uamuzi wa kung’atuka.
Mbunge wa Mtera, John Malecela na Mbunge wa Njombe Kaskazini, Jackson Makweta (wote wa CCM) pia ni wakongwe ambao hawajaeleza nia ya kuachia nafasi hizo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Wakichangia zaidi maoni, Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes ingawa aliunga mkono kwamba maneno maneno yanaweza kudhibitiwa kwa kuweka ukomo, alisema wananchi pekee ndiyo wanaofahamu muda anaostahili mbunge wao kuwatumikia.
Blandes alisema, “hayo maneno maneno kama kuna ukomo, ni kweli unaweza kuyakomesha. Hata mbunge atafanya kazi kwa amani siyo sasa hivi ambapo wengine wanafanya kazi kwa kuwazia majimbo. Lakini wananchi ndiyo wenye ‘speed governor’ (kidhibiti mwendo) cha ubunge.”
Mbunge huyo alitofautiana na wa Muhambwe, Kijiko, kuhusu wabunge wa muda mrefu kwa kusema kutokana na uzoefu walio nao, wanasaidia kutoa michango mizuri na ambayo ni chachu kwa wabunge wengine.
Alitoa mfano wa Mbunge wa Njombe Kusini, Anne Makinda, Mzindakaya, Malecela na Kimiti kuwa ni miongoni mwa watu wenye michango endelevu inayotokana na uzoefu wao bungeni.
Mbunge wa Tabora, Siraju Kaboyonga pia alipingana na mapendekezo ya kuweka ukomo kwa malengo ya kumfanya Mbunge asikae muda mrefu na kusema ni chanzo cha kuyapotezea majimbo maendeleo.
Akitolea mfano wa majimbo ya mkoani Tabora aliyodai yamekuwa yakibadilisha wabunge kila kipindi cha uchaguzi isipokuwa Tabora Mjini, Kaboyonga alisema majimbo yasiyobadilisha mara kwa mara wabunge yana maendeleo tofauti na yanayobadilisha.
Mbunge wa Muhambwe, Felix Kijiko (CCM) alikubaliana na Waziri Pinda kwa kusema wabunge wanaokaa muda mrefu wamebaki kufanya kazi kwa mazoea.
Alisema Mbunge aliyepata wadhifa huo tangu miaka ya 1970 hapaswi kuwepo hadi sasa na kwamba hafanani kimtazamo na wabunge wa sasa.
“Wabunge wa miaka ya 1970 walichaguliwa kutokana na uwezo wa kusema sema. Waangalie wabunge wanaosema sema sana majimboni kwao wamefanya nini,” alisema Kijiko ambaye ana kipindi kimoja bungeni bila kuwataja wabunge waliokaa muda mrefu bungeni huku akisisitiza, “wewe wachunguze wabunge wanaosema sana, majimboni mwao hakuna wanachofanya.”
Mwanataaluma, Profesa Mwesiga Baregu pia aliunga mkono kwamba wananchi waachiwe wachague kiongozi wanayemtaka bila kushawishiwa kwa hongo na kujengewa hofu yoyote.
Alisema iwapo Watanzania watakuwa na uwezo wa kuchagua kiongozi kwa kuzingatia utendaji wa mgombea ni lazima watakuwa wanachagua kiongozi bora kuliko ulivyo mfumo wa sasa hivi.
“Sasa hivi wananchi hawachagui kiongozi bora, wanaweka mbunge ambaye anatumia fedha nyingi kuwahonga na kila baada ya uchaguzi anatumia fedha, katika hali ya namna hiyo hakuna kiongozi bora wa jimbo,” alisema Profesa Baregu.
Alisema Waziri Mkuu ahangaike na elimu ya uraia kwa wananchi ili waepuke kurubuniwa na kujengewa hofu, kwamba wakichagua fulani au chama fulani hawawezi kupelekewa maendeleo.
Alisema sasa hivi wananchi wanahongwa na kujengewa hofu hivyo kujikuta wanachagua mbunge chini ya shinikizo.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Victor Kimesera alisema tatizo kwenye ubunge si ukomo, bali tatizo ni namna hata wabunge wabovu wanavyochaguliwa tena kuongoza kwa vile tu wanatoa rushwa.
“Tatizo ni rushwa, hili tukiliondoa Watanzania watapata wabunge bora.” Mwenyekiti wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi alidai mapendekezo ya Waziri ni kujisumbua kwa kuwa ndani ya CCM wapo watu walioigeuza siasa kama ajira yao, jambo ambalo ni vigumu kwao kumuunga mkono.
0 comments