Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Wahadhiri wanne watimuliwa Chuo Kikuu

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kimewafukuza kazi wahadhiri wanne, mfanyakazi mmoja, na kimefuta matokeo ya wanafunzi 20 baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu katika matokeo ya mitihani. Wanafunzi wengine 71 wapo hatarini kufutiwa matokeo endapo mpaka kesho hawatajitokeza kwenye kamati maalum iliyoundwa kuchunguza kadhia hiyo ya udanganyifu wa matokeo iliyoibuka miezi takribani minne iliyopita na gazeti hili kuwa la kwanza kuitangaza kwa umma. Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Tolly Mbwette aliwaeleza waandishi wa habari jana Dar es Salaam, kuwa uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Baraza la Seneti kilichokaa Ijumaa iliyopita na kikao cha jana cha Baraza la Chuo, kilichohitimisha suala hilo lililochunguzwa chini ya mfumo wa Student Academic Recording System (SARS). Aliwataja wahadhiri waliofukuzwa na nafasi zao katika mabano ni Saimon Kitila (Mhadhiri Msaidizi, Kitivo cha Uongozi na Biashara); Jovin Mwehozi (Mhadhiri Msaidizi, Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii); Juma Kanuwa (Mhadhiri Msaidizi, Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii) na Jamal Mwasha (Mkufunzi Msaidizi, Kitivo cha Sheria). Mtumishi mwingine aliyefukuzwa kazi ni Richard Ngwalida, ambaye ni mtaalamu wa kompyuta ambaye amedaiwa alipokea hongo na kumsaidia mwanafunzi kujaribu kughushi matokeo. Hata hivyo, Profesa Mbwette hakuwa tayari kueleza ni hongo ya kiasi gani na hatua zilizochukuliwa kwa mtoa hongo. Kuhusu wahadhiri hao, Mbwette alisema, “Uchunguzi uliofanywa na kamati maalumu iliyoundwa na chuo kuchunguza suala hilo, ulibaini kuwa walihusika kughushi matokeo ya wanafunzi kwa kuyaingiza katika vitivo mbalimbali bila idhini na huku ni kughushi na ni kosa, Baraza la Chuo halikupendezwa na suala hili na hatupo tayari kuvumilia haya.” Akifafanua kuhusu wanafunzi, Profesa Mbwette alisema uchunguzi wa chuo ulioanza Oktoba mwaka jana, uliwezesha kuandikiwa barua wanafunzi 278 kutoka ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma ikiwataka wafike katika kamati maalumu ya Baraza la Seneti kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo, ambapo 207 waliitikia mwito. “Kati ya hao 207 waliofika, mpaka Januari 8, mwaka huu, wanafunzi 120 walishajieleza na kuonekana hawana makosa yoyote, 31 vitivo vyao vimeagizwa vihakikishe takwimu za matokeo yao kwa upya, 36 takwimu tuna mashaka nazo na vitivo vyao vinachunguza ambapo Baraza la Seneti la Februari mwaka huu, litatoa uamuzi dhidi yao, lakini 20 tumewafutia matokeo na 71 tumewapa muda, wasipotokea mpaka keshokutwa (kesho) tunajua wamejifuta wenyewe,” alisema Makamu Mkuu wa OUT. Katika hatua nyingine, wanafunzi 50 ambao majina yao hayakuwemo katika orodha ya wahitimu mwaka jana kutokana na uzembe wa chuo, watashiriki mahafali ya mwaka huu na kwa mujibu wa Profesa Mbwette, matokeo yao watapewa wakati wowote kuanzia sasa ili wayatumie katika kazi na ajira zao. Oktoba mwaka jana, uongozi wa OUT ulibainisha kuhusu kuwepo kwa wanafunzi wanaotuhumiwa kufanya udanganyifu katika matokeo ya mitihani, ambapo gazeti hili pia lilibaini kuhusu wahadhiri hao wanne kuhusika pia katika sakata hilo. Pamoja na mambo mengine, Profesa Mbwette amevishauri vyuo vingine kufanya uchunguzi kama huo ili kulinda hadhi ya elimu nchini.
Tags:

0 comments

Post a Comment