Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kauli ya Rais Kikwete ya kuwaonya mabalozi yazua Balaa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

SIKU mbili baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaonya mabalozi wasijihusishe na chama chochote cha siasa katika Uchaguzi Mkuu ujao Oktoba, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamesema, kauli hiyo ni nzito na kwamba kama hataki wajihusihe na siasa nchini aache kupokea misaada yao.

Akizungumza katika hafla ya kusherehekea Mwaka Mpya na mabalozi kutoka nchi mbalimbali jijini Dar es Salaam juzi, Rais Kikwete alisema kitendo chochote cha mabalozi hao kushabikia chama kitashughulikiwa vema na serikali yake.

Lakini kwa nyakati tofauti jana viongozi wa vyama vya upinzani, walisema serikali haina haki ya kukataza mabalozi kujihusisha na siasa endapo watabaini misaada wanayoitoa inatumika 'kubaka' demokrasia nchini.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Hamad Rashid Mohammed alisema hakuna balozi yeyote anayeingilia mambo ya ndani ya nchi bila ya kushirikishwa na serikali.

Alisema serikali inawashirikisha mabalozi mbalimbali na nchi zao katika masuala mbalimbali ya siasa nchini, kupitia misaada yao na kifedha na kiufundi katika miradi mbalimbali ya kuboresha demokrasia na utawala bora.

“Kauli ya rais Kikwete ni nzito na hii ni kwa sababu anajua kitakachotokea ndio maana anajihami mapema kwa kutoa onyo na vitisho kama silaha dhidi ya mabalozi.

"Vyama vya upinzani vinapaswa kuitafakari kauli ya Kikwete kwa makini. Kwetu sisi tafsiri ya kauli yake ni kwamba mwaka huu hakuna uchaguzi huru na haki, kwa sababu kama upo uchaguzi huru na wa haki tungeona rais akiwaalika mabalozi kuangalia demokrasia, badala ya kuwatisha," aliongeza Rashid.

Rashid ambaye ni mbunge wa Wawi Pemba (CUF), alisisitiza kuwa, "kama rais Kikwete hataki mabalozi wajihusishe na siasa nchini, basi asipokee wala kuomba misaada yao, kwa kuwa mabalozi hawataweza kukaa kimya iwapo wataona fedha za walipakodi wao zinatumiwa vibaya."

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Chadema John Mnyika, alisema anasikitishwa na hotuba ya rais Kikwete kwa mabalozi, ambayo ilikuwa ya vitisho badala ya kutoa taarifa ya utekelezaji wa mambo aliyowaahidi mwaka 2006 alipokutana nao.

"Rais aliwaahidi mabalozi mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuboresha uwanja wa siasa nchini, lakini inasikitisha kwani badala ya kuwapa taarifa ya utekelezaji wa ahadi hizo, anawatisha," alisema Mnyika.

Mnyika alisema katika mkataba wa Viena kuna vifungu vinavyokataza mabalozi kuingilia mambo ya ndani ya nchi na kuhatarisha usalama wa nchi, lakini vifungu hivyo vimepotoshwa na Rais Kikwete pamoja na waziri wa Mambo ya Nje Benard Membe.

Alisema serikali ilikaa meza moja na mabalozi na kuanzisha mradi wa 'kapu la pamoja’ kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za kuendeleza demokrasia nchini, sambamba na Mradi wa Kuimarisha Demokrasia (DDP) wa Umoja wa Matifa (UN).

"Kwa sheria za nchi za mabalozi, wanapotoa fedha za walipakodi wao, hutakiwa kufuatilia matumizi yake kama zinatumika vizuri au zinatumika kubaka demokrasia ya Africa,"alisema Mnyika.

“Sasa kama rais Kikwete anawaonya mabalozi kujihusisha na siasa nchini, basi aache safari za nje kila siku kwenda kuomba misaada yao, ambayo inatokana na fedha za walipakodi wao,” alisema Mnyika.

Alisema katika dunia ya sasa suala la kuheshimu mikataba ya kimataifa na kuacha serikali ya nchi ikikiuka na kupora haki za binadamu, limepitwa na wakati.

Alisema hali hiyo ndio imesababisha mabalozi na mashirika ya kimataifa kutoa matamko mbalimbali ya kutaka kukamatwa kwa rais wa Sudan Omar al Bashir kwa sababu amevunja haki za binadam.

Aliziomba jumuiya hizo na mabalozi kupitia mswada wa sheria ya uchaguzi na ule wa sheria ya matumizi ya fedha katika uchaguzi na kuitolea matamko, kwa kuwa serikali itafanikiwa kuipitisha, itakuwa kaburi la demokrasia nchini.

Mwenyekiti mstaafu wa Chadema Bob Makani alisema onyo la rais Kikwete litakuwa ni sahihi endapo litakua na maana ya mabalozi kutowachagulia watanzania viongozi.

"Kwa mimi onyo lake, ni sahihi endapo linalenga katika mtazamo wa mabalozi hao kutowatuchagulia wananchi viongozi, wasituchagulie wabunge wala rais wawaachie watanzania kufanya maamuzi yao wenyewe kuhusu viongozi wao,"alisema Makani
Tags:

0 comments

Post a Comment