CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimefuta ndoto za Rais Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad ya kuwepo uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya mseto visiwani Zanzibar.
Hivi karibuni kumekuwepo juhudi za chini chini za kutaka Rais Karume wa SMZ aongezewe muda wa urais wakati wanajiandaa kuweka mazingira mazuri ya kuongoza kwa umoja kati ya CUF na CCM visiwani humo.
Hivi karibuni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Jusa Ismail alisema inafaa Rais Karume aongezewe muda ili akamilishe kazi ya kumaliza matatizo ya kisiasa Zanzibar, huku wanasiasa na wananchi visiwani humo wakiunga mkono hoja hiyo tofauti na siku za nyuma ambapo walikuwa wanapinga.
Matumaini ya kuwepo kwa serikali ya mseto visiwani humo, yamezidi kutoweka baada ya Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shamsa Vuai Nahodha kueleza jana kuwa serikali ya mseto haipo.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Katibu wa Itakadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati zinaeleza kuwa kamati Kuu ya CCM inatarajia kukutana mara baada ya sherehe za Mapinduzi Zanzibar kujadili suala hilo.
Chiligati aliiambia Mwananchi Jumapili jana kwamba, Kamati Kuu (CC) ya chama hicho inatarajia kukutana na kutaja ratiba kamili ikiwemo utoaji wa fomu za kugombea urais na ubunge mara baada ya sherehe za miaka 46 ya Mapinduzi ya Zanzibar kesho kutwa.
Chiligati alisema kati ya Januari na Februari, CCM itaanza kutoa fomu hizo kwa wanachama wake wanaotaka kuwania uongozi kupitia chama hicho.
"Tunasubiri sherehe za Mapinduzi zimalizike na Kamati Kuu yetu itakutana na kutoa ratiba kamili ikiwemo utoaji wa fomu kwa wananchama wetu wa Tanzania Bara na visiwani. Fomu hizi zinatarajiwa kuanza kutolewa kati ya Januari na Februari," alisema Chiligati.
Chiligati alisema kuundwa kwa serikali ya mseto visiwani humo kutawezekana tu kutokana na uwiano wa karibu wa jumla ya kura wanazopata wagombea urais ikiwemo viti vya wawakilishi kwa vyama vitakavyoshiriki.
Hata hivyo, Chiligati alisema ni vigumu kwa Tanzania Bara kuwa na serikali ya mseto kufuatia tofauti kubwa ya uwiano wa jumla wa kura wanazopata wagombea kiti cha urais pamoja na viti vya ubunge.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 46 ya Mapinduzi katika ukumbi wa juu wa Baraza la Wawakilishi Maisara jana, Nahodha alisema huu ni wakati wa kuangalia uwezekano wa kutengeneza Zanzibar mpya na siyo wakati wa kujadiliana masuala ya kuundwa kwa serikali ya pamoja.
Nahodha alisema suala hilo linahitaji muda wa majadiliano na iwapo litajadiliwa katika vikao vyote vinavyostahiki na kupitishwa atakuwa miongoni mwa watakaoliunga mkono.
Akizungumzia suala la kubadilishwa kwa katiba ili kumpa nafasi Rais Karume kuendelea kuwa madarakani, Nahodha alisema suala hilo sio jepesi kama inavyofikiriwa na wananchi kwa kuwa linahitaji majadiliano na maamuzi mazito.
Alifahamisha kuwa suala hilo lazima lipelekwe na kujadiliwa katika ngazi tatu kwa kuwa kuna Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya Zanzibar na Katiba ya CCM na kwamba, hata kama katiba za Muungano na Zanzibar, zitabadilishwa haitakuwa rahisi katika katiba ya chama.
Baada ya kufanyika mazungumzo kati ya Rais Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad walisema maafikiano yao ni muelekeo mpya wa siasa za Zanzibar.
CUF ilipata nafasi mbili za uwakilishi katika baraza la wawakilishi kutokana na Maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM(NEC) kumtaka Rais Karume kuteua wawakilishi wawili kati ya kumi aliopewa kisheria kutoka vyama vya upinzani.
Hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara Pius Msekwa alionya kuwa watu wasijenge matumaini kupita kiasi kwa sababu hakuna makubaliano yoyote yaliyosainiwa wala kuafikiwa baina ya vyama hivyo viwili.
Msekwa ambaye pia ni mjumbe katika kamati maalumu ya Mzee Mwinyi, alisema kitendo cha CUF kumtambua Rais Karume si kufikiwa kwa muafaka utakaoleta amani ya kudumu visiwani humo, bali ni ishara yenye matumaini ya kufikiwa kwa muafaka.
Kwa nyakati tofauti Naibu Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Ali Juma Shamhuna na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Muungano), Mohammed Seif Khatib, waliwahi kutoa misimamo yao kuhusu jambo hilo wakionyesha kutofautiana na msimamo wa Karume ambaye alisema uamuzi wa kuwa na serikali ya mseto ni wa Wazanzibari wenyewe.
Tamko hilo la Karume alilitoa siku chache baada ya kukutana kwa faragha na Maalim Seif, ambaye baadaye aliitisha mkutano wa hadhara na kueleza kuwa CUF imeamua kumtambua rais huyo na kwa kufanya hivyo kutarahisisha mazungumzo ya kutafuta muafaka.
Akiwa visiwani Pemba, Waziri Seif, ambaye anatajwa kama mmoja wa watu wanaoweza kujitokeza kuwania urais wa Zanzibar, aliwaambia wananchi kuwa umoja wa Wazanzibari hauhitaji kushirikishwa chama kingine chochote kwa kuwa CCM pekee inaweza kuweka umoja na mshikamano kwa kuwa hiyo ndiyo sera ya chama hicho.
Aliwaambia wananchi wa kisiwa hicho kwamba, MwanaCCM wa Pemba anakuwa ni CCM wa kweli kweli kwa kuwa wanakabiliana na mambo mbalimbali yanayofanywa na wapinzani, lakini wameweza kumudu na kuvumilia bila ya kutoka katika chama hicho.
Pia Mwenyekiti wa CUF taifa, Profesa Ibrahim Lipumba alinukuliwa na vyomba vya habari akisema uamuzi wa kuitambua Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni wa hatari kisiasa kwa kuwa hawana uhakika kama makubaliano waliyoafikiana (kwa mdomo) yatatimizwa kwa asilimia mia.
“Kwa kweli hatua tuliyoichukua ya kuitambua Serikali ya Rais Karume ni political risk(hatari wa kisiasa) na sina uhakika wa asilimia mia moja kama haya makubaliano yatatimizwa,� alisema Profesa Lipumba.
CUF ilitangaza kumtambua Karume na serikali yake, ikieleza kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa maslahi ya Wazanzibari baada ya kuona juhudi zilizofanywa na watu wa nje zikishindwa kuzaa matunda.
0 comments