Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Maombi ya kujiunga vyuo vikuu sasa kwa 'message'

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Boniface Meena


TUME ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), imeanzisha mfumo mpya wa wanafunzi kuomba kujiunga na vyuo vikuu ambapo hivi sasa wanafunzi wanatakiwa kuomba kwa kutuma ujumbe kwenda namba 15789 au kutumia mtandao na maombi yote yatapokelewa na TCU.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Mayunga Nkunya, alisema kwa kupitia mfumo huo, waombaji hawatatakiwa kutoa vyeti vya majibu yao wakati wa maombi kwa kuwa TCU itakuwa inayapata moja kwa moja kutoka Baraza la Mitihani nchini( Necta).

Lakini alisema kwa wale wanafunzi watakaoomba kutoka shule za kimataifa watatakiwa kupeleka majibu yao Necta ili yakahakikiwe kabla hawajatuma maombi yao.

``Wanaotakiwa kuomba ni wale waliomaliza kidato cha sita, ndiyo watakaoweza kutumia mfumo huo, na ni kwa kuanzia wale waliomaliza mwaka 1988 hadi leo,``alisema Prof Nkunya na kuongeza;

``Wale ambao hawakumaliza kidato cha tano au wamepitia elimu ya watu wazima hawataweza kutumia mfumo huo kwa kuwa haiwaruhusu,``.

Kuhusu majibu alisema nayo yatatolewa kwa ujumbe mfupi au mtandao na kwamba ni muhimu waombaji wakaambatanisha namba mbili za simu ambazo zinapatikana au email kwaajili ya kurahisisha mambo.

"Ili wanaotaka kutuma maombi waweze kuelewa mfumo huu, TCU imeandaa kitabu chenye maelezo kamili kuhusu namna wanafunzi wanavyoweza kufanya na vitasambazwa katika mikoa yote, kwenye vyuo vyote vya elimu ya juu, wizarani, Nacte, ofisi za bodi ya mikopo zilizipo mikoani na Dar es Salaam na ofisi za TCU,"alisema.

Profesa Nkunya alisema pia katika tovuti ya TCU, wizara ya elimu, Nacte, vyuo vya elimu ya juu na bodi ya mikopo maelekezo hayo vinapatikana.

Alisema wanafunzi watakaotuma maombi watatakiwa kuomba programu 12 tu kwa taasisi tofauti kama mfumo huo ulivyoandaliwa, lakini katika kufanya hivyo muombaji anatakiwa kuchagua programu nane kwenye taasisi tofauti na programu tatu kwa taasisi moja.

Prof Nkunya alisema mfumo huo unaanza kutumika kuanzia mwaka wa masomo wa 2010/2011 na wanaotuma maombi wanatakiwa kuanza kufanya hivyo kuanzia Februari 15 hadi Mei 31 mwaka huu.

``Hakuna maombi yatakayokubaliwa baada ya mwezi Mei 31 mwaka huu,``alisema Profesa Nkunya.

Alisema waliotuma maombi watapewa majibu yao June 4, na watatakiwa kuhakikisha majibu hayo hadi ifikapo Juni 11 mwaka huu.

Alisema mfumo huo umeigharimu TCU kiasi cha Sh 1 bilioni ambazo zimetolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Tags:

0 comments

Post a Comment