IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MWANASIASA mkongwe nchini, Kingunge Ngombare-Mwiru ameuponda mkakati wa wanawake kutaka kugawana sawa nafasi za uongozi na wanaume akisema wananchi wanahitaji viongozi bora wa jinsia yoyote ile na siyo sura ya mwanamke au mwanaume.
"Njia bora za kuwatumikia watu siyo kugawana nafasi baina ya wanaume na wanawake, bali kuwatendea wema kwa kazi za maendeleo na kudhibiti njia zote za rushwa kwa viongozi," alisema.
Kingunge alisema hayo juzi alipoulizwa maoni yake baada ya kuhudhuria warsha ya mkakati wa kuongeza idadi ya wagombea wanawake kwenye majimbo iliyoandaliwa na Chama cha Wabunge wanawake (TWPG) jijini Dar es Salaam ambapo moja ya maazimo ya warsha ni kuhakikisha wanawake wanagombea ubunge kupitia majimbo ili idadi ya wabunge iwe asilimia 50 kwa 50.
Alisema malengo ya wananchi si kuwaona wabunge wanawake kwenye majimbo, bali ni kuona maendeleo na kuhakikisha viongozi wabovu, wasiojali maendeleo wanaondoka kwenye uongozi na kwamba kwa bahati mbaya viongozi wabovu wengi ndio watoa rushwa.
"Tukifanikiwa kuzuia rushwa tutapata viongozi wazuri wanawake au wanaume," alisisitiza na kuongeza kwamba kwa sasa rshwa ni kero ndani na nje ya vyama vyote vya siasa.
Kauli ya kiongozi huyo inatolewa wakati baadhi ya washiriki wa warsha hiyo wakikilaumu Chama Cha Mapinduzi kwamba kimejenga mfumo wa kuwapendelea wanaume katika uongozi na hata kuteua wagombea wa ubunge kwenye majimbo.
Baadhi ya washiriki walisema CCM inaongoza nchini kwa kuwanyima wanawake nafasi kubwa za kugombea au kuteuliwa hususani kugombea urais au kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na hata kuongoza taasisi nyeti kama polisi au Jeshi la Wananchi.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia nchini (TCD) , Pius Msekwa akifungua warsha hiyo alisema tatizo la wanawake kukosa majimbo linachangiwa na muundo na mifumo ya vyama vyote ambayo inawatenga wanawake kwenye uongozi nyadhifa za juu.
Kauli hiyo ilipingwa na baadhi ya washiriki walipojadili ambapo walisema kambi ya upinzani imejitahidi kutoa nafasi za uongozi kwa wanawake zikiwemo za chama cha PP- Maendeleo kuteua mgombea mwanamke wa Urais wa Jamhuri ya Muungano mwaka 2005 na Chama cha SAU kumteua mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Walisema nacho cha UDP kiliwahi kuwa na Katibu Mkuu mwanamke , Teddy Kasela Bantu ambaye baadaye alihamia CCM.
You Are Here: Home - - Kingunge awaponda wanawake wanaotaka usawa
0 comments