Rais Jakaya Kikwete (katikati) akifafanua jambo kwa mmoja wa maofisa wa Ikulu, Limbilya Fyataga wakati wa hafla ya kukabidhi magari ya kubebea wagonjwa kwa wilaya mbili za Mbozi na Longido, Ikulu jana Dar es Salaam, Hatahivyo hakukabidhi gari kwa mwakilishi wa wilaya ya Ngorongoro, Kayange Jacob (Kushoto) kutokana na mkanganyiko uliojitokeza ambapo gari hilo lilistahili kukabidhiwa kwa wilaya ya Longido.
Rais Jakaya Kikwete akizungumza na mmoja wa Wasaidizi wake Luambilya Fyataga baada ya Rais kushindwa kukabidhi msaada wa magari ya wagojwa Ikulu Dar es Salaam jana kutokana na kuja watu ambao sio walengwa wa kupokea msaada huo. Picha na Fidelis Felix |
Tausi Mbowe
RAIS Jakaya Kikwete jana aligeuka mbogo na kumtimua Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro, Kayange Jacob ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kubaini kuwa wasaidizi wake wamemdanganya.
Mbali na kumtimua mkurugenzi huyo, Rais Kikwete ambaye alitakiwa kukabidhi magari ya wagonjwa kwa halmashauri za wilaya za Mbozi na Longido, aliondoka katika hafla hiyo kwa hasira bila kugawa magari hayo.
Ingawa baadaye jioni ya jana taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilieleza kuwa Rais alimkabidhi Mkurugenzi wa Maendeleo wa Halmashauri ya Mbozi, Levison Jeremiah Chilewa kwa ajili ya wakazi wa eneo la Kamsamba, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Mbeya, gari la wagonjwa ili kupunguza shida ya usafiri wa wagonjwa katika eneo hilo.
Rais Kikwete alifika katika viwanja vya Ikulu saa 7:30 kwa ajili ya kukabidhi magari hayo ya wagonjwa, lakini, kabla ya kuanza kazi hiyo, alimhoji mmoja wa wakurugenzi ambao wilaya zao zilipaswa kupata mgawo huo.
“Wewe bwana unatoka wapi? alihoji Rais Kikwete na mkurugenzi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Kayange Jacob alijibu ametoka wilaya ya Ngorongoro. “Unasema unatoka Ngorongoro?" aliendelea kuhoji Rais Kikwete. "Hapa umefikaje, umekuja kufanya nini na nani kakualika? Aliendelea kuhoji huku akiwageukia wasaidizi wake akiwemo Katibu wa Rais Ikulu.
"Huyu amekuja kufanya nini hapa? Nani kamwalika", alisema Rais Kikwete ambaye sura yake ilionekana wazi kukasirika na kulazimia kuvua miwani.
“Hatuwezi kukupa gari hii. Hii ni kashfa kubwa, nakumbuka vizuri msaada huu niliahidi kwa wananchi wa wilaya ya Longido wakati nilipofanya ziara kijiji cha Engalinaibo kipindi cha ukame ambapo nilifika Kituo cha Afya wakazi wa Engalinaibo wakaniambia hawana gari la wagonjwa na nikawaahidi nitawaletea: “Nakumbuka nilipofanya ziara wananchi wale waliniambia wanayo dispensary (Zahanati ) lakini, hawana gari la wagonjwa na sio nyinyi! Hatukupi bwana, sio lako hatukupi."
"Hatuwezi kukupa gari, watafuteni wanaopaswa kupewa gari hili, hii ni kashfa kubwa, document zote zimeandikwa kwa kijiji cha Engalinaibo iweje tuwape watu wa Ngorongoro?" alihoji.
“Waombeni radhi hawa mabwana (waandishi) mliowaalika kwa ajili ya kufanya coverage hii (kuandika habari hii) kwa kuwasumbua, siwezi kutoa gari hapa waende tu, â€alisisitiza Kikwete na kuondoka eneo la tukio kwa hasira bila kukabidhi magari hayo. Baada ya tukio hilo Mwandishi Msaidizi wa Rais, Premi Kibanga aliwaomba radhi waandishi wa habari kwa kuwasumbua kuhudhuria tukio hilo.
“Hii ni bahati mbaya tu jamani, kilichotokea hapa ni Confusion (mchanganyiko) huyu mkurugenzi amefika hapa baada ya kupewa taarifa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye yeye ndio alipelekewa barua ya mwaliko na Ikulu,â€alisema Kibanga na kulazimika kuisoma barua hiyo mbele ya waandishi wa habari.
Barua hiyo imeeleza kuwa ilienda kwa Katibu Tawala Mkoa wa Arusha na sio mkuu wa mkoa kama alivyosema Kibanga sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa na Katibu wa rais Ikulu ilisomeka:
“Husika na kichwa cha habari hapo juu, Rais wa Jamhuri ya Muungano , mheshimiwa Jakaya Kikwete ameagiza gari moja ambalo limetolewa na Kampuni ya CMC Automobile kwa wananchi wa Tanzania litolewe kwa kijiji cha Engalinaibo Wilaya ya Longido hivyo unatakiwa kuteua madereva wawili watakaohudhuria mafunzo ya jinsi ya kuendesha gari hilo na mkurugenzi wa kuja kukabidhiwa gari hilo.â€
Alipotakiwa kueleza kama barua hiyo imeandikwa kwa kijiji hicho cha Engalinaibo Wilaya ya Longido, iweje waje madereva na Mkurungenzi wa wilaya nyingine na Ikulu isigundue, Kibanga alikiri udhaifu katika hilo.
“Ni kweli walipofika, walipokelewa huwezi kujua walijielezaje lakini, naamini huko walipotokea ndio kulikuwa na mkanganyiko katika mkoa wao badala ya kutumwa wa wilaya ya Longido wamewatuma wa Ngorongoro,â€alisisitiza Kibanga.
Baadaye Mwananchi ilimtafuta Mkurugenzi kupata ufafanuzi ambaye alisema, “Mimi nilipigiwa simu na Mkuu wangu wa wilaya kuwa nije Dar es Salaam kwa ajili ya kukabidhiwa gari la wagonjwa kama msaada kutoka kwa rais siku ya leo (jana) na kupeleka madereva wetu wawili kwa ajili ya kupewa mafunzo ya namna ya kuendesha gari hilo la wagonjwa (Ambulance) na kujiandaa kwa safari."
“Tuliteua madereva na kuwaleta wakafanya mafunzo maalumu na hatimaye mimi mwenyewe nikafika ili kukabidhiwa msaada huo, Kwa kweli hata mimi nimeshangazwa baada ya kusikia kauli ya Rais kuwa Wilaya yangu hatupaswi kupewa msaada huu, mimi nimepigiwa simu tu na mkuu wangu wa wilaya,"alisisitiza mkurugenzi huyo.
0 comments