Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kamati yaagiza Gavana Ndulu BOT achunguzwe

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuteua mthamini huru ambaye atachunguza na kupitia taratibu na hesabu zilizotumika katika ujenzi wa nyumba mbili za viongozi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kamati hiyo ilitoa agizo hilo jana baada ya kupokea maelezo ya Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, kuhusu ujenzi wa nyumba hizo – ya Gavana na ya Naibu wake - ambazo zinadaiwa kukarabatiwa kwa zaidi ya Sh bilioni moja.

“Unajua sisi sote hapa ni wanasiasa, maelezo yako tumeyapokea na kuridhika, lakini tutaridhika zaidi kama hayo uliyosema na nyaraka ulizonazo zitafanyiwa tathmini na mthamini huru, ili kupata ukweli, namwomba CAG ateue mthamini huyu,” alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe.

Awali akitoa ufafanuzi juu ya ujenzi wa nyumba hizo, Gavana alikanusha kukarabatiwa na kueleza kuwa zimejengwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, na mchakato wake ulianza mwaka 2007 ambapo iliamuliwa zijengwe baada ya kubainika kuwa gharama za ukodishaji nyumba kwa ajili ya viongozi wa benki hiyo ni kubwa kuliko kujenga.

Alisema kwa kuzingatia sheria ya manunuzi ya mwaka 2004, walianza mchakato wa ujenzi wa nyumba hizo tofauti, ya Gavana huyo ambayo tayari amehamia miezi sita iliyopita iliyopo Oysterbay eneo la Morogoro Stores, ujenzi wake ukihusisha wazabuni 10 na kuteuliwa mmoja wa bei ya chini na kujengwa kwa Sh bilioni 1.274.

Alisema awali, mzabuni huyo alitaka ujenzi wa nyumba hiyo uwe wa gharama ya Sh bilioni 1.7 wakati wa bei ya juu kabisa alitaka Sh bilioni 1.847, hata hivyo Bodi ya Wazabuni ilikutana na mzabuni wa bei ya chini na kushauriana naye na gharama ikapungua hadi Sh bilioni 1.274 na waliingia mkataba wa kutobadilisha bei.

Ndulu alisema nyumba hiyo ina vyumba vitano, nyumba ya watumishi, chumba cha huduma kwa ajili ya mapishi kukiwa na wageni wengi, kibanda cha walinzi, jenereta kubwa moja, mashine ya viyoyozi ya kisasa, mitambo ya ulinzi kwa usalama wa Gavana na bwawa la kuogelea ambalo limegharimu Sh milioni 40.

“Nasikia kuna watu wanasema eti siwezi kukaa kwenye nyumba ambayo haina bwawa la kuogelea, nawaambia mimi nimeanza kuogelea kwenye mito nikiwa na miaka 12, nimeishi kwenye nyumba hazina mabwawa kwa miaka mingi, hivyo si lazima kuwa nalo, liwepo lisiwepo hainisumbui,” alisema.

Alisema nyumba ya pili nayo ilifuata mchakato na taratibu zilizowekwa ambapo ilikuwa na wazabuni watano akapatikana mmoja na kujengwa kwa Sh bilioni 1.272 tofauti ya Sh milioni mbili katika ujenzi wa nyumba ya Gavana na tayari Naibu Gavana amehamia.

Alisema kabla ya kuhamia nyumba hiyo mpya, akiwa Naibu Gavana, aliishi katika nyumba yake Mbezi, kutokana na utaratibu uliopo wa viongozi wa benki hiyo kukaa kwenye nyumba za benki, alipangishiwa nyumba Masaki ambako ililipiwa dola 7,000 za Marekani kwa mwezi.

Hata hivyo, alisema pamoja na kuhamia katika nyumba hizo mbili kwa mujibu wa mkataba, wana takribani mwaka mmoja kuzifanyia uhakiki, ili kubaini kama zimejengwa kwa kiwango cha fedha hizo na ikiwezekana kufanya marekebisho ndani ya kipindi hicho kupitia mkataba huo.

Benki hiyo imekuwa ikiandamwa na tuhuma za kutumia mabilioni ya fedha kukarabati nyumba za viongozi wake wanne, ambapo inadaiwa Gavana Ndulu aligoma kuhamia nyumba ya Gavana wa zamani marehemu Daudi Balali iliyopo Chole, Masaki, kutokana na kukosa bwawa la kuogelea.
Tags:

0 comments

Post a Comment