Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Watanzania washushwa ndege ya Precision Air

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

ZAIDI ya abiria 15 raia wa Tanzania waliokuwa wakisafiri kwa ndege ya Shirika la Precision Air kutoka Arusha kuelekea Dar es Salaam wameshushwa na kupakizwa raia wa kigeni.

Tukio hilo lilitokea jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kusababisha mtafaruku uliodumu kwa zaidi ya dakika 30 kabla ya walinzi wa uwanja huo kuingilia kati, ili kutuliza hali hiyo kutokana na abiria hao kugoma kushuka.

Wakizungumza na Tanzania Daima uwanjani hapo, abiria hao wamedai kuwa, kitendo cha kuteremshwa katika ndege waliyopanda na kupakizwa abiria wengine ambao ni raia wa kigeni (Wazungu) bila kuelezwa sababu za msingi ni cha ubaguzi wa hali ya juu.

Akizungumza na Tanzania Daima, mmoja wa abiria aliyekumbwa na kadhia hiyo, Pamela Msuya, mkazi wa Dar es Salaam, alisema dakika chache kabla ya ndege kupaa hewani, rubani alizima injini ya ndege na wahudumu kuwaeleza kuwa kumetokea dharura, hivyo hawataweza kupaa.

Alisema kutokana na hali hiyo, waliombwa kusubiri hadi saa 5:40 asubuhi. Awali walikuwa waondoke na ndege hiyo saa 1:00 asubuhi.

Abiria huyo alieleza kuwa, ilipofika saa 5:40 waliingia katika ndege na rubani kuiwasha, lakini ilizimwa tena na kuamriwa kuteremka kwa maelezo ndege hiyo ilipaswa kupakia abiria wa Zanzibar ambao ni raia wa kigeni.

Pamela aliendelea kudai kuwa, wakiwa wanashushwa katika ndege hiyo, baadhi ya abiria waligoma na kusababisha kutokea kwa mtafaruku mkubwa wa zaidi ya dakika 30 kabla ya walinzi wa uwanja huo kuitwa na wahudumu wa ndege hiyo na kwenda kuwashusha huku wakiwaita wazamiaji.

“Si siri, tumedhalilishwa sana, yaani tunaitwa wazamiaji mbele ya wageni, watatuelewaje? Tuna booking ya muda mrefu tofauti na hao (raia wa kigeni),” alisema Pamela.

Baada ya kushushwa abiria hao, wengine ambao wengi ni raia wa kigeni, walionekana wakipanda ndege hiyo kuelekea Zanzibar.

Abiria mwingine ambaye hakupenda kutaja jina lake gazetini, alisema alishangazwa na kitendo hicho kutokana na abiria hao (wazungu) kutokuwa na taarifa za usafiri (booking) na kwamba walifika muda huohuo na kupatiwa usafiri.

Aliongeza kuwa, baadaye waliambiwa kuwa wasubiri ndege ya saa 11:00 jioni ambayo itawapeleka jijini Dar es Salaam.

“Tulishushwa tukaambiwa tusubiri ndege ya saa tano, tukavumilia na muda huo ulipofika tena wakatuambia tusubiri ya saa 11. Huu si uungwana hata kidogo,” alisema abiria huyo.

Baada ya jitihada za kupata uongozi wa shirika hilo kugonga mwamba, mmoja wa wafanyakazi wa Precision Air mkoani Arusha ambaye alikataa kutaja jina wala cheo chake, alisema kwa kifupi tatizo hilo linashughulikiwa, na alipoulizwa zaidi aliwataka waandishi wa habari waende katika Uwanja wa KIA.

“Nimeshawaambia tatizo linashughulikiwa, kama mnataka zaidi nendeni KIA,” alisema mfanyakazi huyo.

Tags:

0 comments

Post a Comment