*Mwera awatimulia vumbi Kangoye, Makanya na Haruni *Makamba akubali yaishe asema 'walibanwa nusu uwanja' *Alonga kama mgombea wao hajaridhika aende mahakamani Na George John, Tarime WAKATI CHADEMA ikiibuka kidedea katika uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani Tarime, CCM imepinga matokeo hayo kupitia mgombea wake, Bw. Christopher Kangoye katika kinyang'anyiro cha ubunge. Katika uchaguzi huo uliofanyika juzi, mgombea wa CHADEMA, Bw. Charles Mwera, alipata kura 34,545 dhidi ya kura 28,996 alizopata Bw. Kangoye. Akitangaza matokeo jana, Msimamizi wa Uchaguzi, Bw. Trasias Kagenzi, alisema jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 67,733, halali zikiwa 64,795 na 2,938 zikiharibika. Katika pingamizi lake, Bw. Kangoye alisema hakubaliani na matokeo yaliyompa ushindi mgombea Bw. Mwera. Bw. Kangoye alitangaza msimamo huo muda mfupi baada ya kufika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kukuta tayari matokeo hayo yameshatangazwa na Msimamizi. Alidai kuna baadhi ya mambo, ambayo hata hivyo hakuyataja, hakubaliani nayo hivyo alitarajia kuwasilisha rasmi malalamiko yake kwa Msimamizi bila kusema kama anaweza kwenda mahakamani kupinga kwa mujibu wa sheria za uchaguzi. “Mimi nimekuja kusikiliza matokeo, nikidhani nimeshinda nafika, naambiwa eti tayari matokeo yameshatangazwa...mimi siamini, lazima nikalalamike kwa Msimamizi wa Uchaguzi, kuhusu mambo fulani fulani yaliyojitokeza katika uchaguzi huu,” alisema Bw. Kangoye akiwa amefuatana na mtu aliyetajwa kuwa ni Katibu wa CCM wa Wilaya ya Tarime. Wakati Bw. Kangoye alilalamikia matokeo hayo, vyama vingine vimekubaliana na matokeo hayo huku kauli ya Bw. Kangoye ikipingana na ya Katibu wa Uenezi wa CCM, Kapteni mstaafu John Chiligati aliyoitoa juzi mbele ya waandishi wa habari mjini hapa, kuwa watakubaliana ma matokeo yoyote yatakayotangazwa. Baada ya matokeo hayo kutangazwa, shangwe, nyimbo na vigelele vilitawala hasa kuitokana na wagombea wote wawilib wa CHADEMA akiwamo diwani mteule wa Tarime Mjini Bw. John Heche naye kushinda dhidi ya mfanyabiashara Peter Zacharia wa CCM. Bw. Trasias ambaye alitangaza matokeohayo chini ya ulinzi mkali wa Polisi ukiongozwa na Mkuu wa Operesheni Maalumu Polisi, Bw. Venance Tossi, alisema wapiga kura 146,919 ndio waliotarajiwa kupiga kura juzi. Mbali na CHADEMA na CCM, vyama vingine vilishoshirikini DP ambacho mgombea wake, Mchungaji Benson Makanya alipata kura 305 na NCCR-Mageuzi ambayo mgombea wake, Bw. Marwa Haruni alipata kura 949. Akizunguza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Bw. Zitto Kabwe, alisema ushindi huo ulitarajiwa, kutokana na chama hicho kuwa makini katika kushughulikia mambo ya kitaifa hasa yanayogusa uchumi wa nchi. Hata hivyo, alisema alisikitishwa na vitisho vya Jeshi la Polisi, kuwapiga wananchi kwa mabomu ya kutoa machozi, maji ya kuwasha, huku wakiwanyanyasa wagombea wa chama chake, hali ambayo pia ilichangia idadi kubwa ya watu kushindwa kujitokeza kupiga kura. “Polisi walitumia nguvu kubwa kuisaidia CCM, lakini nguvu ya umma ilikataa na wao wakajua hilo, ndiyo maana wamekubaliana na umma wa wana Tarime, sasa kazi kubwa ni kapambana na ufisadi kwa kasi na nguvu kubwa tena kwa vitendo,” alisema Bw. Kabwe. Naye Bw. Mwera alisema ushindi aliopata ni matokeo ya kazi nzuri aliyoifanya akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi za CHADEMA hata kufikia kutoa elimu bure ya sekondari kwa watoto wote wanaojiunga na sekondari. Alisema kazi kubwa sasa katika kurejesha imani aliyopewa na wananchi wa Tarime, ni kuvaa viatu vya marehemu Chacha Wangwe kwa kutetea maslahi ya wananchi wa Tarime, yakiwamo madini na ardhi, ili raslimali hizo zitumike kikamilifu kuwakomboa wana Tarime. “Nilijua lazima niwe mbunge, kwani tayari nilianza kazi ya kutumikia wananchi kwa kuboresha miundombinu ya barabara, elimu na huduma zingine za kijamii, nikiwa Mwenyekiti wa Halmashauri hii,” alisema Bw. Mwera. Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi Kata ya Tarime Mjini, Bw. Renatus Mahimbali, alimtangaza Bw. John Heche kuwa diwani wa kata hiyo kwa kupata kura 4,820, akiwashinda Bw. Zacharia wa CCM aliyepata 3,239 huku NCCR ikipata kura 161, CUF 79 na DP kura 24. Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, barabara zote za Tarime zilifungwa baada ya wananchi wa rika mbalimbali kujitokeza na kufanya maandamano makubwa kwa kuimba nyimbo za furaha na kejeli kwa CCM na za kupongeza ushindi. “Makamba habari ndiyo hiyo, hapa ni Tarime si Kiteto... uliotuita wahusi sasa soo mzee, umeambulia ulichopanda,” walisikika wananchi hao wakiimba na mabango yakionesha maandishi hayo. Naye Reuben Kagaruki anaripoti, kwamba Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, amesema anakusudia kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Bw. Mwera, kwa kile anachodai haukuwa huru na wa haki. Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Mchungaji Mtikila, alidai uchaguzi huo ulitawaliwa na vurugu kutoka kwa baadhi ya watu. "Huwezi kusema uchaguzi ulikuwa halali wakati watu tumepigwa mawe na kuumizwa ni lazima tufungue kesi ya kupinga matokeo," alisisitiza Mchungaji Mtikila. Alipoulizwa anajisikiaje kwa chama cha upinzani kushinda jimbo hilo, Mchungaji Mtikila alisema kwa Tarime CHADEMA ndicho chama tawala na vyama vingine ndivyo vilikuwa vya upinzani. "Kwa Tarime CHADEMA ndicho chama tawala kwa sababu ndicho kinaongoza halmashauri na sisi tuliobaki (Ikiwa ni pamoja na CCM) tulikuwa wapinzani, hivyo si kweli kusema kuwa chama cha upinzani kimeshinda," alisisitiza Mchungaji huyo. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TLP, Bw. Augustino Mrema, alisema wananchi wa Tarime wameonesha ushujaa na wamedhihirisha kuwa hawahongeki kwa kofia na fulana. Alisema kuna umuhimu kabla ya kuingia kwenye uchaguzi wowote, kwenda Tarime kujifunza kwani wameonesha ukomavu wa kisiasa. Alisema kushindwa kwa CCM hizo ni dalili za mvua ya rasharasha, kwani kazi ndiyo kwanza inaanza. nao Jovin Mihambi na George Boniphace, wanaripoti kutoka Mwanza kwamba CCM imekiri kuwa uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani Tarime ulikuwa mgumu kuliko viongozi wake walivyokuwa wakitarajia. Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusufu Makamba wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa. Alisema yeye na CCM wameupokea ushindi huo na kuongeza kuwa CHADEMA ilikuwa inajibu mapigo ya uchaguzi wa mwaka 2005 ambapo CCM ilipata ushindi mkubwa dhidi ya CHADEMA ambayo ilipata kura 30,000 za Freeman Mbowe huku Rais Jakaya Kikwete akipata kura 50,000. Alisema mchakato mzima wa uchaguzi katika jimbo la Tarime kwa upande wa chama chake ulikuwa haumpi usingizi kwani CCM ilikuwa imebanwa 'nusu uwanja'. Alisema kushindwa kwa CCM katika udiwani na ubunge si kwamba chama hicho hakina uwezo wa kunyakua kiti hicho katika uchaguzi wa mwaka 2010 na kuongeza kuwa CCM kwa sasa inaangalia wapi imeteleza na kujikwaa na kuangalia upya kwa kusahihisha makosa ambayo yalijitokeza katika uchaguzi ambao umepita na kuipa CHADEMA ushindi. Alisema kutokana na ushindi wa CHADEMA, CCM inakubali matokeo ingawa hadi sasa mgombea wake katika ngazi ya ubunge amekataa kusaini karatasi ya kukubali matokeo. Alisema kuwa mgombea huyo, ana haki ya kutafuta haki mbele ya sheria, lakini atafanya hivyo kwa gharama yake na wala si ya CCM. Uchaguzi huo mdogo wa ubunge na udiwani umefanyika, kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa Tarime na Diwani wa Tarime Mjini, Bw. Chacha Wangwe kilichotokea kwa ajali ya gari eneo la Pandambili mkoani Dodoma Julai 28 mwaka huu. Kutoka Iringa Francis Godwin, anaripoti kwamba CCM mkoani humo imejikuta chali baada ya mgombea wa udiwani wa TLP kata ya Lupingu, Ludewa, Bw. John Kiowi kuibuka kidedea. Bw. Kiowi alipata kura 633 dhidi ya kura 578 alizopata mpinzani wake, Bw. Alfred Kona wa CCM. Akitangaza matokeo kwa mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jana, Kaimu Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Bw. Fridolin Mwapinga, alisema CCM imekubali matokeo. |
You Are Here: Home - - CHADEMA yaibuka na ushindi Tarime. matokeo kupingwa mahakamani
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments