Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO , LEO KATIKA MAGAZETI - Umri wa Lulu waibua mvutano kortini

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
UMRI wa msanii wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu anayekabiliwa na mashtaka ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba jana ulizua utata katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya mawakili wanaomtetea kutaka kesi hiyo iondolewe mahakamani hapo ili akashtakiwe kwenye Mahakama ya Watoto.


Kesi hiyo ilitajwa jana huku mawakili wanaomtetea wakiongozwa na Keneth Fungamtama, wakiwasilisha maombi kuhusu suala hilo la umri wa mteja wao wakitaka asishtakiwe mahakamani hapo kama ilivyo sasa. Fungamtama ambaye alikuwa akisaidiana na Mawakili Peter Kibatala na Fulgence Masawe, alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa miaka 17 hivyo, kesi yake ilipaswa kusikilizwa katika Mahakama ya Watoto. “Mshtakiwa ana umri wa miaka 17 na tuna uthibitisho wa cheti cha kuzaliwa ambacho kinaonyesha mahali na tarehe aliyozaliwa mshtakiwa,” alidai Fungamtama.


Fungamtama alisema Kifungu cha 4 cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 Kipengele namba 21, kinatamka wazi kuwa mtoto ni yule aliye na umri chini ya miaka 18. Wakili huyo aliendelea kunukuu vifungu mbalimbali vya Sheria ya Mtoto kama 98 (i) na 114 (ii), ambavyo alidai kuwa vyote vinawapa nguvu ya kuwasilisha maombi yao hayo ya kuihamisha kesi hiyo. “Hata katika suala la Mahakama, vifungu vyote vya sheria hii vimefafanua, hivyo tunawasilisha maombi yetu kwamba mteja wetu ana umri wa miaka 17 na shauri hili lingepaswa kusikilizwa Mahakama ya Watoto,” alidai.


Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda aliomba wapewe muda zaidi kwa sababu bado wanaendelea na upelelezi wa kesi hiyo. “Kesi hii imekuja mahakamani hapa kama ya mauaji na upelelezi bado haujakamilika. Tunaposema haujakamilika, tunapeleleza kila kitu, likiwamo suala la umri,” alieleza Kaganda. Alisema hata jina linaloonekana katika cheti cha kuzaliwa kilichowasilishwa mahakamani hapo, linasomeka Diana Elizabeth wakati mshtakiwa ametajwa mahakamani hapo, kwa jina la Elizabeth Michael. “Tunaomba muda tuweze kuchunguza kuhusu umri wa mshtakiwa kwa sababu aliwaeleza polisi kwamba ana umri wa miaka 18 halafu mawakili wake wanakuja kueleza hapa mahakamani kwamba ana umri wa miaka 17,” alidai Kaganda. Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa kutokana na mvuto wa kesi hiyo katika jamii, wanaomba wapewe muda zaidi kufanya upelelezi ili kumtendea haki mshtakiwa huyo.


Kuhusu cheti hicho kusomeka Diana Elizabeth, Wakili Fungamtama alikiri na kudai kuwa ni jambo la kawaida hasa kwa Wakristo kuwa na majina mawili. Fungamtama alidai kuwa hawana pingamizi na maombi ya upande wa mashtaka kwamba wapewe muda zaidi wa kufuatilia cheti cha kuzaliwa cha mshtakiwa, ingawa alidai kuwa suala hilo halina ugumu. Akitoa uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mkazi Augustina Mbando alisema: “Mahakama imesikiliza maombi yaliyoletwa na Fungamtama na Kaganda na imeona kesi iliyopo hapa ni ya mauaji na jinsi kesi hii ilivyo, hatuwezi kufanya hoja yoyote hadi upelelezi utakapokamilika.”


“Kama defence (upande wa utetezi) wana maombi yoyote wanaweza kufanya hivyo kupitia Mahakama Kuu,”
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 21, mwaka huu itakapotajwa tena. Inadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka huu katika eneo la Sinza Vatican, Dar es Salaam msanii huyo wa kike, alimuua Kanumba. Jana Lulu alifikishwa mahakamani hapo saa 2:50 asubuhi akiwa peke yake kwenye gari linalobeba mahabusu, huku akisindikizwa na magari mengine mawili.


Alipoingia mahakamani alikuwa amezingirwa na askari Magereza na Polisi zaidi ya 10 na kuufanya umati mkubwa wa watu uliofurika mahakamani hapo kushindwa kumwona. Miongoni mwa watu waliofika mahakamani hapo jana ni baba mzazi wa msanii huyo, Michael Kimemeta na ndugu zake wengine kadhaa.

0 comments

Post a Comment