IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
KAMATI Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni, imemtia hatiani Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, kwa kitendo chake cha kuchangisha fedha kutoka taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kinyume cha utaratibu.
Juni 21 mwaka huu, Jairo aliwaandikia barua watendaji wakuu wa taasisi nne zilizo chini ya wizara hiyo akizitaka kuchanga fedha kwa ajili ya kugharamia kile kilichoelezwa kuwa ni maandalizi na uwasilishaji wa hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/12 bungeni Dodoma.
Ripoti hiyo pia imewatia hatiani Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, Philemon Luhanjo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Utoh na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kwa kushindwa kutimiza wajibu wao, hivyo kubariki udanganyifu wa Jairo.
Akiwasilisha ripoti hiyo bungeni jana, Mwenyekiti wa kamati, Ramo Makani, alisema taasisi zilizoandikiwa kuombwa michango ni Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) sh milioni 40, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Maji na Mafuta (Ewura) sh milioni 40, Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) sh milioni 50 na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ambazo kwa pamoja zingechangia jumla ya sh milioni 180.
Makani ambaye pia ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini (CCM), alisema kuwa taasisi zilizoitikia maombi ya kuchangia ni tatu, TANESCO, Rea na TPDC ambazo kwa pamoja zilichanga sh milioni 140,000 zilizotakiwa kuwekwa katika akaunti ya Geological Survey of Tanzania (GST) Na. 5051000068 NMB Tawi la Dodoma.
“Ewura walikataa kutoa kiasi walichoombwa badala yake iligharamia chakula cha mchana kwa siku tatu kwa sh 3,656,000 na tafrija ya Julai 18 mwaka huu, kwa sh 6,141,600, siku ambayo bajeti ya wizara ilitarajiwa kupitishwa. Kwa maana hiyo Ewura ilichangia jumla ya sh 9,797,600,” alisema Makani.
Kamati hiyo ilisema kuwa sababu zilizoifanya wizara kuchangisha fedha haziwezi kutiliwa maanani kwa sababu hadi kufikia Juni 25 mwaka huu, wizara hiyo ilikwishapata mahitaji yote ya fedha za uwasilishaji wa bajeti baada ya kupokea sh milioni 171,542,000 za matumizi mengineyo (OC) kutoka Hazina.
“Baada ya kukamilisha uchunguzi wake kuhusu jambo hili, kamati teule ilibaini kwamba Katibu Mkuu wa wizara hiyo, hakuomba kibali cha waziri wa fedha ili kupata ridhaa ya kuchangisha, hivyo alikiuka masharti ya waraka huu,” alisema Makani.
Aliongeza kuwa hata nyaraka za mipango kazi na bajeti za taasisi hizo zilizochangia, kwa mwaka wa fedha 2010/2011 ilibainika kuwa haikuwa na kasma mahususi kwa ajili ya kuchangia wizara kuwasilisha hotuba ya bajeti yake bungeni.
Katika mahojiano na watendaji wa TPDC, kamati ilibaini kuwa shirika hilo lililazimika kuchanga fedha hizo bila idhini ya bodi kama inavyotakiwa na kanuni zake za fedha ili kutii maagizo ya Jairo.
Kwamba shirika hilo, walilazimika kuchanga kinyume na utaratibu kwa kuhofia kuitwa wakaidi kutokana na uzoefu waliokwisha kuupata siku za nyuma.
“Kamati teule ilibaini kuwa mahitaji halisi ya maandalizi ya uwasilishaji wa hotuba ya bajeti yalikuwa sh 207,042,000, ambayo Jairo aliyaridhia.
Kati ya fedha hizo zilizohitajika, sh 35,500,000 zilitoka kwenye kifungu cha Project Co-ordination and Monitoring cha wizara. Kwa mantiki hiyo, wizara ilibaki na upungufu wa sh 171,542,000,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema fedha iliyoingizwa kwenye akaunti ya GST kwa ajili ya shughuli za uwasilishaji bajeti ni sh 418,081,500 ambazo matumizi yake yalikuwa ni posho za siku tano kwa ajili ya kujikimu kwa watumishi 69, sh 32,425,000, vikao kwa watumishi 243, sh 127,820,000, licha ya Jairo kuelekeza kuwa maofisa 61 ndio walipaswa kwenda Dodoma.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa malipo ya chakula na vinywaji kwa watumishi 169 kwa siku tano yalikuwa sh 17,480,000 na mafuta ya magari 15 yaligharimu sh 5,754,000, vifaa vya kuandikia sh. 625,020 na takrima na viburudisho sh 8,000,000.
Kati ya sh 225,482,880 zilizobakia, benki ziliwekwa sh 99,438,400 wakati sh 126,044,480 ziko mikononi.
Pia kamati hiyo ilibaini kulikuwepo na uwasilishwaji wa taarifa za kughushi za malipo ya posho za watu mbambali walioshiriki kwa namna moja shughuli za wizara hiyo kama watumishi wa ofisi ya Bunge, wizara husika, waandishi wa habari, afya na polisi.
Makani alisema taarifa zilizokuwepo kwenye ofisi ya Bunge zilionesha kuwa viwango vya posho vilikuwa sh 250,000 kwa viongozi wa Bunge, wabunge (vikao) sh 80,000, wabunge (usafiri) sh 30,000, wakuu wa idara/kazi maalumu sh 80,000, maofisa sh 50,000 na watoa huduma wengine sh 20,000.
“Wakati wa kupitia matumizi ya wizara, viwango vya posho vilikuwa tofauti na maelekezo ya ofisi ya Bunge, kwa mfano wakati wabunge walilipwa sh 110,000, mtumishi wa ngazi ya mhudumu alilipwa sh 120,000 badala ya sh 20,000, wakurugenzi sh 180,000 badala ya sh 80,000 na maofisa wengine sh 150,000 badala ya sh 50,000,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa upande wa wizara hiyo, kamati teule iliona nyaraka na kwa maelezo ya watendaji kati ya Julai 18 hadi Agosti 26 mwaka huu, wakati wa mkutano wa nne wa Bunge, waziri na naibu wake walilipwa sh 4,000,000 kila mmoja kama posho ya takrima.
Katika maoni na mapendekezo yake, kamati teule inataka serikali ichukue hatua za kinidhamu kwa Jairo kwa matumizi mabaya ya madaraka, kukusanya na kutumia fedha za umma kinyume cha sheria, vile vile na watumishi wengine wa wizara hiyo waliotajwa na taarifa hiyo pia wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria.
Aidha, Waziri Ngeleja kama msimamizi mkuu wa wizara husika, suala la uchangishaji halikupaswa kufanyika bila yeye kufahamu, hivyo kamati teule inapendekeza achukuliwe hatua zinazofaa.
Lakini pia CAG amelalamikiwa kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake kikamilifu hususan katika kutoa ushauri na hitimisho katika ripoti yake kuhusu Jairo na hivyo kuonekana sehemu ya kuficha uovu, hivyo naye kamati teule imependekeza achukuliwa hatua kwa upotoshaji huo.
Kwa upande wa Luhanjo ambaye ametajwa sana na kamati kuwa aliamua kwa makusudi kumsafisha Jairo kwa kuficha ukweli wa taarifa ya CAG, badala yake aliamua kumrejesha kazini akidai hakuwa na kosa la kinidhamu, ilipendekezwa serikali imchukulie hatua zinazofaa kwa kitendo hicho cha upotoshaji.
Wabunge wang’aka
Wakichangia taarifa hiyo ambayo utekelezaji wake utatolewa katika Bunge la Sita mwezi Januari mwakani baada ya serikali kupitia mapendekezo hayo na maoni ya wabunge, wachangiaji wote zaidi ya 10 waliitaka serikali kujipanga upya kwa kuzichunguza wizara zake zote na kuwawajibisha wahusika.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema watendaji wa serikali wanatumia kificho cha posho kujichotea mabilioni ya fedha za serikali lakini akashangaa kuona wahusika bado wanaendelea kuwa kazini.
Alimwomba waziri mkuu kuangalia utaratibu wa kufuta semina kwa wabunge wakati wa Bunge, akisema hicho ndicho kichaka cha ufisadi, ambapo alitoa mfano wa waandaaji semina hizo kulipa viwango vidogo vya posho, ilhali kwenye nyaraka zao wanaghushi na kuonesha wamelipa viwango vikubwa.
“Chanzo cha ubadhirifu mawizarani ni makatibu wakuu…sasa lazima tuelezwe serikali inaongozwa na makatibu wakuu au mawaziri huko wizarani. Mawaziri hawa usiwaone hivi huko wizarani hawana sauti mbele ya makatibu wakuu,” alisema Mbowe.
Katika michango yao, wabunge James Lembeli na Godfrey Zambi (CCM), Tundu Lissu na Ezekia Wenje (CHADEMA), Moses Machali na Agripina Buyogela (NCCR-Mageuzi), mbali na mengi waliyochangia lakini walimsihi Ngeleja na naibu wake Adam Malima, kuachia ngazi ili kulinda hadhi zao na chama chao.
“Tunachokizungumza hapa ni rushwa ambayo imepiga hodi hadi Ikulu kwa Katibu Mkuu Kiongonzi Luhanjo, anamtakasa mtu anayetuhumiwa kwa rushwa…halafu CAG naye ameingia huko kwenye rushwa, nchi hii imebakia mifupa, minofu wanakula wakubwa na maskini wanabaki kutaabika,” alisema Lembeli.
Lembeli pia aliungana na Wenje pamoja na Machali kutaka Luhanjo na Jairo wachukuliwe hatua mara moja kama ilivyo kwa watuhumiwa wengine.
Lakini kuhusu CAG wabunge wengi licha ya kutaka awajibishwe vile vile walishauri iundwe kamati teule ya kumchunguza ili kubaini ukweli, wakieleza kuwa kuna kila dalili kuwa alishinikizwa kumtakasa Jairo.
Mchungaji Yohane Natse (CHADEMA) na Martha Umbulla, ambao walikuwa miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo teule, walisema kuna ubadhirifu mkubwa serikalini na hivyo serikali inapaswa kujitafakari kupitia hayo yaliyojitokeza kwenye wizara hiyo.
Natse alisisitiza kuwa madaraka ya makatibu na wakurugenzi ni makubwa mno na hivyo kumnyima waziri nguvu ya kusimamia baadhi ya mambo.
Kwamba mhimili wa serikali unatumia Bunge kuhalalisha ufisadi kwa wizara kuwaandalia wabunge semina zipate sehemu ya kufanya ufisadi kupitia malipo ya posho.
“Mmoja wa mawaziri wakuu wastaafu alituambia kuwa Bunge letu ni dhaifu limeshindwa kuisimamia serikali. Sasa tutumize wajibu wetu bila woga kwa kuisimamia serikali. Na katika hili Rais anapaswa kumwajibisha Ngeleja,” alisema Natse.
Hata hivyo, Mbunge wa Bumbuli, Beatrice Shellukindo (CCM), ambaye ndiye aliyeibua sakata hilo bungeni kwa kuonesha barua hiyo iliyoandikwa na Jairo, jana aliwashangaza wabunge pale alipoungana na Christopher ole Sendeka (Simanjiro) na Anne Killango (Same Mashariki), kuwatetea Ngeleja na Malima wasijiuzulu.
Alisema anasema hivyo bila kushinikizwa wala kumwogopa mtu bali alitaka uozo huo ufahamike na wahusika wachukuliwe hatua, huku akisisitiza kuwa kujiuzulu kwa mawaziri hao peke yao hakutoshi bali watendaji wote wa wizara zote wachunguzwe na kuchukuliwa hatua.
“Nilipoibua hoja hii bungeni baadaye ilikwenda pale wizarani, lakini kila mtu alikuwa akiniona kama tatizo hata wale walionipa nyaraka ile walikuwa wakinikimbia, masharti kibao niliwekewa hadi niweze kuingia ndani…lakini niliwaambia watendaji, acha unafiki, fanya kazi,” alisema.
Shellukindo alisema kuwa alitumiwa ujumbe mfupi na kupokea simu kutoka kwa watu 1,215 wakimpongeza kwa ujasiri wake, kisha akawataka watumishi wa sehemu nyingine wenye nyaraka za wakuu wanaofuja fedha za umma wampatie azifanyie kazi.
“Lakini mimi kama Beatrice Matumbo Shellukindo… hili si la Ngeleja na Malima peke yao bali ni kila wizara, hawa wamezungukwa na watendaji wao…sasa kuwataka pekee wajiuzulu ni kuwatoa kafara”, alisema.
Killango katika mchango wake alianza kwa kutoa tahadhari kwa wale wanaozigeuza majina kamati teule za Bunge na kuziita majina ya wenyeviti wanaowasilisha ripoti, akisema hatua hiyo imeleta usumbufu na chuki kubwa kwa baadhi yao, huku akimtolea mfano aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati teule ya Richmond, Dk. Harrison Mwakyembe.
Alisema kuwa yaliyojitokeza kwenye ripoti hiyo ni uthibitisho kuwa wizarani hali si shwari.
Kwamba wizara nyingi zina makatibu wakuu ambao hawana mahusiano mazuri na mawaziri wao.
Mbunge wa Mbozi Mashariki, Zambi katika mchango wake aliunga mkono msimamo wa wabunge wa CHADEMA wanaopinga posho akisema kutokana na taarifa hiyo, ameanza kuelewa ni kwa namna gani zinatumika kuendeleza ufisadi, ambapo kwa siku moja mtu analipwa mara tatu tofauti.
“Naongeza pendekezo kuwa wale watumishi wote waliotajwa katika taarifa hii kuhusika katika upotevu wa fedha zilizokosa vielelezo vya matumizi yake, wakamatwe na kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kukatwa mishahara ili warejeshe hasara waliyoisabaisha,” alisema Zambi na kutoa angalizo kwa CCM kuwa ikiwa serikali haitawachukulia hatua wahusika, wapinzani watazidi kujichukulia umaarufu.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Bunge lammaliza Jairo. NGELEJA, MALIMA, LUHANJO NA CAG NAO KUADHIBIWA
0 comments