IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MBUNGE wa Tarime, Nyambari Nyangwine, amesema kama mwekezaji katika mgodi wa dhahabu wa North Mara hatawalipa wananchi fidia halali ya ardhi waliyoichukua na kuwajengea nyumba za kifahari, ataongoza kuchukua panga na kwenda kuwachinja wawekezaji hao.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Madini na Nishati juzi jioni, Nyangwine alisema pia kama wananchi wa Tarime hawatafaidika na baadhi ya huduma na fursa mbalimbali, ataongoza wananchi wa eneo hilo kwenda kuwafukuza kwa nguvu wawekezaji hao.
"Wengine (wabunge) wamekuwa wakienda mgodini na kupokea ten percent (mgawo wa asilimia 10) na kisha wanarudi, mimi sina mchezo huo...kama wananchi hawatajengewa nyumba za kifahari, tutashika mapanga tutagecha (tutachinja).
"Tunataka pia biashara na zabuni zote wapewe watu wa Tarime hasa wanaozunguka mgodi ule, hatutaki kuona juisi au chakula kutoka Dar es Salaam, hata uzoaji wa chuma chakavu wapewe watu wa Tarime, wale watu wa Kahama (wanaozoa chuma chakavu), nitawafukuza," alisema Mbunge huyo.
Wakati akitoa kauli hizo huku mwenyewe akionekana kutabasamu, wabunge wengine awali walipigwa butwaa na baadaye wakajikuta wakimshangilia na yeye akaendelea kutoa vitisho kuwa hawataki kuona wafagizi waliotoka Afrika Kusini.
Alisema pia watatumia nguvu kuhakikisha umeme uliokwenda katika mgodi huo, unawanufaisha pia wananchi na wasipoushusha kwa wananchi, wao wataushusha kwa nguvu.
"Inaumiza kuona mali ya nchi inaporwa, tutapigana mpaka tone la mwisho nikiwa huku huku ndani ya CCM, haiwezekani madini yote hayo tunayamaliza na Tanzania inabaki masikini," alisema Nyangwine.
Alisema pia anashangaa mgodi huo haujaeleza kwa namna gani wataendeleza wachimbaji wadogo na kuutaka ujenge Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Alimtaka mwekezaji huyo, kurudi vijijini na mkataba mpya kwa wananchi waliochukuliwa ardhi yao na kuachana na mkataba wa zamani kwa madai kwamba mkataba huo, wananchi hao walisainishwa bila kujua walichukuwa wakinyang'anywa.
"Ile mikataba ni feki...tena walisema watajenga barabara ya lami kama hawajengi, nitaongoza kuwafukuza...namtaka Waziri (Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki), kuwaondoa wale polisi wanaolinda mgodi, kazi yao ni kulinda raia si mgodi," alisema kama anatoa amri hivi.
Mbunge huyo alisema hata dola laki mbili wanazopewa Halmashauri ya Tarime ni kidogo na hazilingani na mamilioni ya dola anazochukua mwekezaji huyo na kutangaza kuwa hawataki kulipwa tena dola laki mbili, wanataka kupata na wao mamilioni ya dola.
Kuhusu madai ya sumu kumwagwa katika maji ya Mto Tigithe na mgodi huo, Mbunge huyo alisema uchunguzi umefanyika lakini matokeo hayajatolewa na kuongeza kuwa anahisi Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) limepewa ten percent (asilimia kumi-tafsiri ya rushwa).
Baada ya kumaliza kuchangia hoja na kutangaza kuwa haungi mkono bajeti hiyo kwa kutotendea haki wachimbaji wadogo wa madini, Mnadhimu Mkuu wa Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge William Lukuvi, alitoa kauli ya kusahihisha maneno makali ya Mbunge huyo.
"Simpingi Mbunge ila katika matumizi yake ya lugha ameashiria kutumia mapanga...simuingilii kama anao uwezo wa kumfukuza mwekezaji lakini naomba mheshimiwa Nyangwine, afute neno la kutumia silaha," alisema Lukuvi.
Hata hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai ambaye alikiri kuwa hajawahi kuona Bunge moto kama hilo, alisema amewahi kuishi Mara na kama wabunge wangekuwa Musoma, hivyo alivyozungumza Mbunge, ndiyo angeeleweka na wananchi wake.
"Hawataki mtu anayezungumza legelege lakini Mbunge wakati mwingine lainisha maneno
yako," alisema Ndugai.
Naye Mbunge wa Kahama, James Lembeli, alionya kuwa hata Kahama muda si mrefu itakuwa kama Tarime kwa kuwa haiwezekani wilaya yenye migodi mikubwa miwili ya dhahabu, ikawa masikini.
Alituhumu watendaji wa Serikali kwa kushirikiana na wawekezaji hao kudhulumu wananchi, kuwanyang'anya wachimbaji wadogo eneo nyeti la madini na kuongeza kuwa Kampuni ya Barick imekuwa ikiiibia Serikali kwa kutolipa kodi huku ikitengeneza faida ya mamilioni ya dola.
Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), amesema kama ni kweli mgodi wa madini ya dhahabu wa Buhemba unamilikiwa na Serikali, anaungana na Kambi ya Upinzani
kusema Serikali iliyopo madarakani ni legelege.
Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini juzi usiku, Mkono alisema mgodi huo umeporwa kila kitu kilichokuwa kimewekezwa, kuanzia mitambo mpaka magari huku hata nyumba za mgodi zikiwa katika hali mbaya.
"Ule mgodi kwa sasa hakuna kitu, ni usanii kusema unaukabidhi kwa Stamico (Kampuni ya Serikali ya Madini) na kama Serikali inakiri kuumiliki naungana na wapinzani kusema Serikali ni legelege," alisema Mbunge huyo.
Mkono alisema amefurahishwa mgodi huo kukabidhiwa Stamico lakini akataka Serikali imtaje aliyepora mashine za uchimbaji na kuharibu uwekezaji uliokuwa umeshafanywa mgodini hapo.
Kwa mujibu wa Mkono, alishauliza nani alikuwa akilinda mgodi huo na kujibiwa kuwa ulikuwa chini ya Polisi na kuhoji: "sasa lile ni jeshi la wananchi au jeshi la wahuni?"
"Ninaongea kwa uchungu kwa kuwa ile mitambo ni aghali sana, Waziri (wa Nishati na Madini, William Ngeleja) useme kule unakwenda kukabidhi nini na nani amechukua mitambo hiyo
lasivyo siungi hoja mkono," alisema Mkono.
Kauli hiyo ya Serikali legelege wiki hii, ilitolewa na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) na kusababisha Bunge kuchafuka baada ya Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigangwalla (CCM), kumtaka Mbunge huyo kufuta usemi.
Hata hivyo, Kafulila alikataa kufuta usemi akidai kuwa ni kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuwa Serikali legelege haiwezi kukusanya kodi na kuwa yuko tayari kufia ukweli huo.
Lakini Kafulila pia hakumnukuu vizuri Mwalimu Nyerere, kwa kuwa alisema "Serikali corrupt (inayochukua rushwa) haikusanyi kodi" na neno hilo legelege alisema "Chama legelege huzaa Serikali legelege".
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Mbunge atangaza kuua mwekezaji
0 comments