Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KIMATAIFA , HABARI ZA LEO - AU kupeleka majeshi Libya

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
HATIMAYE Umoja wa Afrika (AU), umefikia uamuzi kadhaa ili kunusuru maisha ya wananchi wa Libya ikiwamo kupeleka jeshi la kulinda amani.


Hatua hiyo inafuatia makubaliano ya wakuu wa nchi wanachama wa umoja huo waliokutana nchini Equatorial Guinea kwa lengo la kuzungumzia mgogoro wa vita nchini Libya.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema jana mjini Dar es Salaam kuwa mkutano huo ulihudhuriwa na marais 31.


Alisema katika mkutano huo, viongozi walifikia makubaliano ya kuitaka kamati ya nchi tano iliyochaguliwa kushughulikia mgogoro wa Libya kuendelea na kazi hiyo na kupewa majukumu mapya.


Membe alisema kamati hiyo inazihusisha nchi za Mali, Mauritius, Afrika Kusini, Uganda na Congo DRC.
Membe alisema kamati hiyo imepewa jukumu la kuyapelekea taarifa makundi matatu yanayohusika katika mgogoro wa huo ili kuhakikisha kwamba yanasitisha mapigano.


Makundi hayo ni Serikali ya Libya, waasi na Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (Nato).
“ Viongozi wa nchi za AU, wameitaka kamati hiyo kufikisha taarifa kwa makundi hayo kuhakikisha wanasitisha mapigano ili kulinda maisha ya walibya na mali zao,” alisema Membe.


Alisema kamati hiyo pia imepewa jukumu la kupeleka majeshi ya kulinda amani nchini Libya pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu kwa walioathirika na vita hiyo.


“ Vita ikisitishwa, jumuiya za kimataifa zitakuwa na uwezo wa kuingia nchini humo na kutoa huduma za kibinadamu zinazotakiwa baada ya vita hiyo,” alisema Membe.Kwa mujibu wa Waziri Membe, kamati hiyo inatakiwa kupeleka waangalizi nchini Libya kwenda kushuhudia kama mapigano hayo yamesitishwa.


Waziri Membe alisema kamati hiyo pia imepewa kazi na AU kuhakikisha kwamba inaanzisha mchakato katika nchi hiyo kuelekea katika uchaguzi wa kidemokrasia ambao viongozi watapatikana kwa kuchaguliwa na wananchi.
“ Marais hao wamefikia makubaliano na kuitaka kamati hiyo kuanzisha mchakato wa kisiasa wa walibya wote ili wapate Serikali yenye kufuata sheria na utawala bora,” alisema Membe.


Membe alisema viongozi hao wa AU waliutaka Umoja wa Mataifa (UN) kusitisha vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Libya ili kuharakisha upatikanaji wa amani.

0 comments

Post a Comment