Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Wachina wampiga Mkuu wa Kituo cha Polisi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Balozi wa China Nchini Tanzania Bwana Liu Xinsheng akimkabidhi Rais Jakaya Mrisho Kikwete

VURUGU kubwa zilizuka juzi kwenye kituo cha Polisi Babati Mjini mkoani Manyara baada ya wafanyakazi wa kampuni inayojenga barabara ya Chico, raia wa China kumpiga mkuu wa kituo hicho, ASP Shaaban Minginye na mkuu wa polisi jamii mkoani humo, ASP Morris Okinda.


Tukio hilo lililodumu kwa saa mbili kati ya saa 12:30 jioni hadi saa 2:30 usiku liliwalazimisha polisi kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto zilizorushwa hewani ambazo hata hivyo zilijibiwa na Wachina hao wakitumiia bastola nao, hali iliyoweka rehani amani mjini Babati.


Wachina hao wanadaiwa kufanya vurugu hizo na kuwashambulia ASP Mingiye na Okinda kwa madai kuwa polisi walimwachia dereva wa basi la abiria aliyelikwaruza gari lao na kusababisha ajali.


Kitendo hicho cha kuwapiga makonde viongozi hao wa polisi mkoani humo kiliamsha hasira za wananchi ambao walianza kumshambulia mmoja wa raia hao wa China.


Mwananchi ilishuhudia raia huyo wa China, Chang Charles akipigwa na wananchi hao waliochukizwa na kitendo chao cha kuwapiga polisi ambapo alijaribu kutumia mtindo wa kujihami 'kung fu' huku akitoa sauti za, 'huu, haa', lakini alipigwa ngumi iliyomjeruhi usoni


Katika tukio hilo, ASP Minginye alipigwa vibao na ngumi na raia mmoja wa China ambapo raia watatu wa China walijeruhiwa vibaya na wananchi na kulazwa kwenye Hospitali ya Mrara mjini Babati na hali zao zilielezwa kuendelea vizuri.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Liberatus Sabas alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo na kwamba raia 10 wa China wanashikiliwa kwa kuhusika na vurugu hizo.




Alisema chanzo cha vurugu hizo ni raia mmoja wa China, (Chang Charles) kumpiga mkuu wa kituo cha polisi Babati, baada ya kuliachia basi la abiria lililogonga lori linalomilikiwa na kampuni hiyo (Chico), kitendo kilichofanya wananchi kumpiga Mchina huyo.


"Hali hiyo ilijitokeza baada ya basi la abiria aina ya Scania, mali ya Kampuni ya NBS lililokuwa likitokea Kahama kwenda Arusha kukwaruzana na gari la kampuni hiyo ya Kichina lililokuwa linatumika katika ujenzi wa barabara ya Babati-Singida,"alisema.


Alisema baada dereva wa basi hilo kulikwaruza gari la kampuni ya Chico aina ya Ford, tukio hilo liliripotiwa kituo cha polisi Babati na dereva wa basi kutakiwa kuwapeleka abiria Arusha ili kesho yake arudi kituoni hapo.




“Baada ya dereva wa basi kuruhusiwa na kuondoka raia mmoja wa China alianza kurusha mawe kwenye basi hilo na kuvunja taa na kioo cha mbele na kumpiga mkuu wa kituo, ndipo abiria waliposhuka na kuanza kumshambulia Mchina huyo,” alisema Kamanda Sabas.




Alisema baada ya vurugu hizo lilizuka kundi lingine la raia wa China lilijitokeza na kuanza mapambano na wananchi na ndipo katika vurugu hizo askari polisi wakapiga risasi hewani na mabomu ya machozi ili kuwatawanya na kujaribu kusitisha vurugu hizo.




“Hadi hivi sasa Jeshi la Polisi linawashikilia raia 10 wa China wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo na tunatarajia kuwafikisha mahakamani leo (jana), ili wakajibu mashtaka ya uaribifu wa mali na kufanya vurugu,” alisema Kamanda Sabas.


Kamanda Sabas aliwataja Wachina hao wanaoshikiliwa na polisi kuwa ni Chang Charles, Luan Hiten(23), Wang Sheng(23), Sing Yun(24), Sing Jin (23), Lin Jun (37), Whang Puong(23) Lu Gang (23) na Sio Jing (23).


Alisema katika vurugu hizo, askari polisi mmoja ambaye hakumtaja jina alijeruhiwa jichoni na Wachina hao na raia watatu wa China walijeruhiwa na kulazwa Hospitali ya Mrara wakipatiwa matibabu.


Aliwataja raia hao wa China waliojeruhiwa kuwa ni Young Gris, Luan Hiten na Chang Charles ambao alisema hali zao zinaendelea vizuri, baada ya kupatiwa matibabu.

0 comments

Post a Comment