IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
HALI ya hewa ndani ya Chadema mkoani Arusha, imezidi kuchafuka baada ya taarifa za uhakika kueleza ya kuwa, baadhi ya madiwani wake wapo kwenye hatihati ya kutimliwa na kufikia mwafaka na CCM bila ridhaa ya chama.
Taarifa hizo zinakuja ikiwa ni siku moja baada ya Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, kutoa tamko la kutomtabua Naibu Meya, Estomih Mallah wa Chadema na mwafaka uliofikiwa kumaliza mgogoro wa meya.
Taarifa za uhakika zinadai ya kuwa, tayari kamati ya utekelezaji ya chama hicho mkoani hapa, juzi kiliwasilisha mapendekezo mbele ya kamati kuu miongoni mwake ni madiwani hao kuchukuliwa hatua.
Inadaiwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, amewasilisha mapendekezo mbalimbali mbele ya kamati kuu ambayo yanataka madiwani hao kuomba radhi, kujivua madaraka au kukubali kufukuzwa ndani ya chama.
Wanaotakiwa kuomba radhi ni madiwani wa chama hicho, ambao walifikia mwafaka na CCM hivi karibuni, huku taarifa zikisema mapendekezo hayo yamemtaka Mallah sanjari na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Mipango Miji na Mazingira, John Bayo, wajivue nyadhifa kuomba radhi au wakubali kutimliwa.
Hatahivyo, taarifa hizo zilienda mbali zaidi na kubainisha ya kuwa mapendekezo hayo yaliyowasilishwa mbele ya kamati kuu ya Chadema yalitokana na mahojiano yaliyofanywa baina ya kamati ya utekelezaji ya mkoa dhidi ya madiwani hao iliowahoji hivi karibuni kutaka kujua hatua ya wao kukubali kufikia muafaka huo bila idhini ya chama.
Mwigamba alikiri madiwani hao kuhojiwa hivi karibuni, lakini hakuweza kukubali au kukataa kuhusu mapendekezo ya kuwatimua, huku akisihi kusubiri uamuzi wa kamati kuu.
“Ni kweli tuliwahoji kujua walipata wapi mamlaka ya wao kufikia mwafaka wakati chama hakina taarifa, lakini tayari nimewasilisha mapendekezo mbele ya kamati kuu, hivyo subiri haitachukua siku mbili mtasikia tamko,” alisema Mwigamba
Naye Mallah Bayo walisema wao wanasubiri uamuzi wa kamati kuu na wako tayari kwa hatua yoyote itakayochukuliwa dhidi yao.
You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA - Madiwani wa Chadema Arusha hatihati kutimliwa
0 comments