IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imehoji hatua ya kurejeshwa kazini kwa Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Tanga, baada ya
kufukuzwa kazi kwa tuhuma za kuuza viwanja mara mbili, ambapo imeelezwa kuwa amerejeshwa kwa barua ya ikulu.
Kamati hiyo chini ya mwenyekiti wake, Bw. Agustino Mrema, imesema kuwa imeshangazwa na taarifa ya ardhi katika halmashauri hiyo lakini pia kuhusu kurejeshwa kazini kwa afisa huyo Bw. Makwasa Biswalo aliyehusika na matatizo ya ardhi wilayani hapo.
Wakichangia hoja kuhusiana na taarifa hiyo wajumbe wa LAAC, Mbunge wa Kigoma Kusini Bw. David Kafulila, Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Morogoro Bi. Susan Kiwanga waliikataa taarifa hiyo na kutaka hatua kuchukuliwa.
Walisema haiwezekani kuwapo na taarifa ya migogoro ya ardhi ambayo imesababishwa na mtumishi huyo lakini iamriwe arudishwe kazini, hivyo ni vyema hatua za awali za kumsimamisha kazi zikachukuliwa tena.
Katika taarifa yake kwa kamati hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Gikene Mahene alisema mtumishi huyo awali alifukuzwa baada ya kubainika kuhusika na utata wa umiliki viwanja.
Alisema mtumishi huyo alibainika kuwauzia wananchi viwanja zaidi ya mara moja hivyo kusababisha migogoro mikubwa ya ardhi katika halmashauri hiyo lakini pia wananchi kukosa imani na uongozi. Bw. Gikene aliongeza kusema kuwa ushahidi wa zaidi ya viwanja 70 ulipatikana hivyo kuifanya halmashauri kuchukua hatua za nidhamu dhidi ya mtumishi huyo ikiwa ni pamoja na kumfukuza kazi.
"Baada ya kumfukuza kazi alikata rufaa tume ya utumishi wa umma ambayo hata hivyo iliridhia kufukuzwa kazi kwa mtumishi huyo lakini baadaye ilikuja tume ya rais ya kushughulikia migogoro ya ardhi na kumrejesha kazini,” alisema.
Alisema mtumishi huyo aliwasilisha barua ya kurejeshwa kazini kutoa ikulu jambo lililowafanya wamrejeshe kazini ambapo mpaka sasa ni afisa ardhi katika halmashauri ya jiji la Tanga.
Baada ya kuwasilishwa kwa taarifa hiyo Mwenyekiti wa LAAC, Bw. Mrema alitaka barua iliyotoka ikulu kuwasilishwa katika kamati hiyo huku pia akielezea kamati kutoridhishwa na hatua hiyo iliyochukuliwa.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Kamati ya Mrema yakwaa kigingi ikulu
0 comments