Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Chadema wamshtaki Makinda

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

KAMBI ya Upinzani Bungeni imemshtaki Spika, Anne Makinda katika Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge, ikimtuhumu kumkingia kifua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda asiwajibishwe na Bunge.Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Spika Makinda kuzuia kujibiwa kwa swali la Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kuhusu sababu za Serikali kutowafikisha mahakamani askari polisi waliohusika katika mauaji ya raia 72 yaliyofanyika katika kipindi cha kati ya mwaka 2008 na mwaka huu.

Mbali ya Lissu, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Esther Matiko naye alitaka kupata maelezo kutoka kwa Waziri Mkuu ya sababu za kutofikishwa mahakamani kwa askari waliohusika na mauaji ya raia katika eneo la Nyamongo, wilayani Tarime.

Wabunge hao walifanya hivyo wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, yanayoulizwa kila Alhamisi wakati Bunge linapokutana.

Spika Makinda alizuia kujibiwa kwa maswali hayo kwa maelezo kuwa masuala hayo yako mahakamani na kwamba kuyajibu kutakuwa ni kuingilia uhuru wa Mahakama ambayo mara kadhaa, imelilalamikia Bunge kuwa limekuwa likiingilia huru wake.

Maelezo hayo yalionekana kutoiridhisha Kambi ya Upinzani ambayo iliamua kumshtaki Spika katika Kamati hiyo ili ichunguze uamuzi wake na baadaye kutoa uamuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Lissu ambaye pia Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chadema, alisema tayari kambi yake imeshakamilisha maandalizi ya hati ya malalamiko ya wabunge hao na kwamba ingewasilishwa kwa Katibu wa Bunge jana jioni.

“Tusingependa kufanya hayo maana vinginevyo tunaonekana kama tunahoji uwezo wa Mheshimiwa Spika, lakini hatuna jinsi imebidi. Tumempeleka katika Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge kwa sababu kuacha uamuzi potofu wa Spika wa Bunge usimame, itakuwa ni ‘precedent’ (kitangulizi cha jambo) ya hatari kwa Bunge letu kwa sababu uamuzi huo kuachwa bila kupingwa, unaweza kutumiwa katika mijadala mingine katika siku zijazo,” alisema Lissu.

Alisema vitendo hivyo vya Makinda ni vya ukiukwaji wa kanuni za kudumu za Bunge na kwamba katu Kambi ya Upinzani haitakuwa tayari kumwacha aendeshe Bunge kama anavyoona binafsi.

“Spika wa Bunge ana mamlaka makubwa sana kiuamuzi, lakini anatakiwa kufuata kanuni na kanuni kuu muda wote ni ya nane inayomtaka kuendesha shughuli za Bunge na kutoa uamuzi kwa haki, uadilifu na bila chuki wala upendeleo wowote kwa kuongozwa na Katiba, sheria na kanuni,” alisema Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria.

Lissu alisema Spika Makinda pia anapaswa kufuata uamuzi wa maspika waliomtangulia na kuzingatia uzoefu, mila na desturi za mabunge mengine yanayofuata utaratibu unaofafana na kufuatwa na Bunge la Tanzania.

Mbunge huyo alidai kwamba hiyo si mara ya kwanza kwa Spika Makinda kutoa uamuzi ulioonekana kumkingia kifua Waziri Mkuu wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo.

“Itakumbukwa kwamba wakati wa Mkutano wa Pili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uliofanyika Februari mwaka huu, Mbunge wa Arusha Mjini, Mheshimiwa Godbless Lema aliomba mwongozo wa Spika kutokana na kauli ya uongo iliyotolewa na Waziri Mkuu kuhusu mauaji ya Arusha. Baada ya kutoa mwongozo alioombwa, Spika wa Bunge alimkemea Mheshimiwa Lema na kumtaka athibitishe kauli yake juu ya uongo wa Waziri Mkuu,” alisema Lissu.

Alisema hata hivyo, Lema alipotoa uthibitisho wake, Spika Makinda alizima mjadala kwa kukalia uthibitisho wa Lema... “Hadi leo Watanzania hawajaambia chochote juu ya jambo hilo, lakini kuna siku tutakumbushia hilo ili wananchi wajue ukweli.”

Mbunge huyo alidai kwamba uamuzi wa Spika kuhusu swali lake, aliufanya bila kuuliza au kupewa taarifa sahihi kuhusu mauaji ya Tarime na kesi dhidi yake na wenzake.

“Hii ni hatari sana kwa uendeshaji bora wa Bunge, kama Spika ambaye pia ni kiongozi wa Bunge atakuwa anatoa uamuzi ambao hana taarifa sahihi juu yake… hadhi na heshima ya Bunge itashuka kwa sababu wananchi wataona Spika anatoa uamuzi kwa lengo la kuwakingia kifua mawaziri na Serikali ili wasiwajibishwe bungeni. Hii ikitokea ni hatari kwa demokrasia yetu kibunge,” alisema.

Alisema yeye na wenzake saba wanakabiliwa na mashtaka ya kuingia kijinai katika eneo la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, kufanya mkusanyiko haramu katika eneo hilo na kuwazuia Mganga wa Hospitali ya Wilaya na askari polisi kufanya uchunguzi wa miili ya marehemu waliouawa katika Mgodi wa Nyamongo na kwamba mashtaka hayo si ya mauaji na kwamba haikuwa sahihi kwa Spika kuzuia maswali yake.

Alipoulizwa juu ya imani yake kwa Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Lissu alisema hana sababu za kuamini kwamba pamoja na kuwa ina idadi kubwa ya wabunge wa CCM, itaacha uadilifu wake na kupindisha haki.

Mbunge huyo alisema kwa mujibu wa kanuni, wakati kamati hiyo yenye wajumbe 15 itakapoketi kuchunguza malalamiko hayo, Spika ambaye pia ndiye wake na naibu wake, watapaswa wasikalie kiti hicho na badala yake, wajumbe watamchagua mmoja wao kuendesha kikao cha uchunguzi.

Alipotakiwa kuzungumzia hatua hiyo, Makinda ambaye jana asubuhi hakuendesha Kikao cha Bunge alijibu kwa simu: “Niko kwenye kikao." Alipotafutwa tena, simu yake ilipokelewa na msaidizi wake ambaye alisisitiza kuwa bado alikuwa katika kikao.

0 comments

Post a Comment