Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Wanafunzi wataka kuua walimu, shule yafungwa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SERIKALI imeifunga Shule ya Sekondari Lusaka wilayani Sumbawanga Mkoa wa Rukwa, kwa muda usiojulikana baada ya wanafunzi kutaka kuwaua walimu wao kwa kuwachoma na moto wakiwa wamelala.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Christian Laizer amesema, shule hiyo ya kutwa imefungwa tangu Machi 19, mwaka huu.

Laizer amesema, walimu wanane wamelazimika kutafutiwa vituo vingine vya kazi baada ya kutokea vurugu kutokana na wanafunzi wa shule hiyo kugoma kutoa michango iliyopangwa na Serikali.

Amesema , vurugu zilikithiri Machi 18, baada ya saa 5 usiku wanafunzi kutaka kuwaua walimu wanane waliopo shuleni hapo kwa kuwachoma na moto baada ya kujigawa katika vikundi.

Inasadikiwa baadhi ya wanafunzi wema walivujisha taarifa hizo na kuwaeleza walimu ndipo walipoanza kuzilinda nyumba zao wakiwa nje, lakini walipobaini kuwa wanafunzi hao ni wengi, ilibidi watoe taarifa Polisi huku wakiwa wamejificha porini.

Polisi waliopo Kituo cha Laela walipofika eneo hilo waliwatawanya wanafunzi hao waliokuwa na silaha mbalimbali zikiwamo mapanga, marungu nondo.

“Hali ilikuwa mbaya sana sasa ilipofika Machi 19 asubuhi tulifika pale ikabidi tuwachukue walimu wote na walibeba vile vilivyowezekana tu, lakini mifugo na samani za ndani vyote vilibaki.

“Tuliona tuokoe maisha yao kwanza…tuliingia gharama ya kuwapangisha kwenye nyumba za kulala wageni mjini Sumbawanga wakisubiri kupangiwa vituo vingine vya kazi,” alisema Mkurugenzi huyo.

Kwa mujibu wa Laizer, waliwasiliana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na zikatoa ridhaa shule hiyo ifungwe hadi hapo uongozi wa kijiji utakapohakikisha shule inakuwa na ulinzi na pia waliofanya vurugu wanabainika.

Kwa mujibu wa Laizer katika siku hizo za vurugu, wanafunzi hao walifanya uharibifu mkubwa kwa kuvunja vioo kwenye nyumba ya mkuu wa shule hiyo na kwenye madarasa.

Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Emiliana Fungo alisema michango iliyokuwa ikilalamikiwa na wanafunzi hao ni ada kwa wanafunzi wa kutwa, tahadhari, dawati ulinzi na nembo ya shule ambapo jumla yake ni Sh 65,000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi.

0 comments

Post a Comment