Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Ngeleja, Mhando waonja joto ya jiwe kwa wabunge

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter WABUNGE wa Kamati ya Nishati na Madini jana waliwatoa jasho Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando na Waziri wake, William Ngeleja baada ya kuhoji mambo mbalimbali kuhusu matatizo ya nishati ya umeme nchini ikiwemo mkataba kati ya shirika hilo la umma na kampuni ya gesi Songas.


Katika kikao hicho kilichowakutanisha viongozi wa Serikali na Tanesco wakiongozwa na Waziri Ngeleja, jambo zito ukiacha la mgawo wa umeme lilikuwa kuhusu mkataba huo wa Songas ambao unadaiwa kugubikwa na giza.


Miongoni mwa mambo ambayo Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, January Makamba aliibana Tanesco, mbali ya uzalishaji umeme kwa kutumia mafuta wakati wa dharura ni kuhusu faida inayopatikana na umiliki wa mradi huo baada ya serikali kulipa deni Benki ya Dunia (WB).


Hata hivyo, akijibu maswali hayo, Mhando ambaye kila wakati aliposimama alikuwa akiweka suti yake sawa, alisema kuwa hafahamu... "Inabidi nikaupitie tena mkataba huo kwani sijaona kipengele hicho kinachodai kwamba ikiwa gesi imekwisha, basi mafuta yatumike kwa dharura kuendeshea mitambo ya umeme.”


Katika swali lake, Makamba alikuwa na shauku ya kufahamu uwezo wa wanasheria na watendaji waliopo Tanesco akisema ni vigumu kuingia mkataba na watu au kampuni fulani halafu ikawa ngumu kujua ndani ya mkataba kuna kitu gani.


Hata hivyo, Mhando alilitetea shirika hilo akisema lina watendaji wenye uzoefu mkubwa lakini tatizo kubwa ni uwezeshwaji kutoka serikalini, kwani shirika linaalzimika kukopa ili wataalamu wake wafanye kazi kwa ufanisi mzuri.


Alisema ni vizuri shirika likaachwa lijiamulie lenyewe mambo yake pasipo kuingiliwa na serikali akisema hali hiyo ndiyo inayopunguza ufanisi wa kazi.


Mtendaji mkuu huyo wa Tanesco, alisema shirika lake halina uwezo wa kufanya mambo mpaka liihusishe serikali hivyo ingekuwa vizuri waachiwe muda wa kujiendesha wenyewe kama shirika.


Mbunge wa Magu, Dk Festus Limbu alihoji ni kiasi gani Tanesco inahitaji kupatiwa ili kuondokana na tatizo la mgawo wa umeme swali ambalo lilimtoa jasho Mhando baada ya kuorodhesha miradi mingi bila kutoa jibu la kitakwimu za fedha.


Ngeleja aliingilia kati kujibu swali hilo akisema wakati mwingine Tanesco inaonewa kwani wakati ikiomba fedha nyingi za miradi wabunge huwa hawaiungi mkono.Alisema ni vigumu kutoa hesabu kamili ya ni kiasi gani kinachotakiwa kwa sababu wanaotoa fedha ni serikali na hivyo ni vigumu kutoa majibu hayo kwa kamati kwa muda mfupi.


“Ni vigumu sana kutoa tarakimu kamili kwamba ni kiasi gani kinachotakiwa ili kulimaliza hili tatizo la umeme kwa sasa,” alisema.Alisema Tanesco ni taasisi ya serikali inayojitegemea na kujiendesha kwa misingi ya kibiashara, hivyo serikali itaendelea kutoa muongozo wa kisera na kusimamia sheria bila kuingilia majukumu ya kiufundi na kiutendaji ya shirika hilo.


Hata hivyo, alikiri kuwa ni vyema mkataba wa Songas na Tanesco ukapatiwa upya ili kuondoa tatizo hilo la umeme nchini... “Hili linawezekana kabisa kwani ni shirika kubwa la muda mrefu. Linaweza likajiendesha lenyewe bila ya kutegemea serikali,” alisema Ngeleja.


Kuhusu mkakati wa kupata mitambo, alidai taratibu za kukamilisha mazungumzo ya kuuziana umeme na kampuni iliyonunua mitambo ya Dowans ziko katika hatua ya zabuni.


“Mchakato wa zabuni hiyo unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha wiki moja tu,"alisema Ngeleja.


Pia alidokeza kuwa mchakato wa kukodi mitambo ya uwezo wa megawati 260 kufikia Julai, 2011 unaendelea, majadiliano na mshindi wa zabuni ya megawati 70 za Tanga yameshakamilika na mkataba unatarajiwa kutiwa saini hivi karibuni. Alisema zabuni za mitambo mingine ya Tegeta, Tank Farm na Ubungo Old Diesel Plant, hazikupitishwa na bodi ya uzabuni kwa kuwa hazikukidhi viwango vilivyowekwa.


Hata hivyo, alisema zabuni ya kununua mitambo mipya ya megawati 150 itafunguliwa keshokutwa.


Lakini pia, Ngeleja alikiri kuwa kampuni ya Marekani ya Symbion Power, ndiyo iliyothibitisha kuwa imenunua mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Dowans Tanzania Limited.


Ngeleja alisema wizara yake ipo mbioni kukamilisha mkakati wa kurekebisha sekta ya umeme ifikapo Desemba, mwaka huu akisema sekta ya nishati ni mhimili wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii hivyo wizara hiyo itaendelea kushauriana na mamlaka husika ili ipewe kipaumbele kwenye bajeti ya serikali.

0 comments

Post a Comment