MMAREKANI aliyekamatwa na Polisi akipiga picha maiti wa mgodini Tarime, amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja baada ya kukiri kosa la kuingia nchini na kufanya kazi bila kibali.
Joyceline Tembi (27) ambaye ana hati ya kusafiria ya Marekani, lakini mzaliwa wa Mbambane Swiziland, alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Tarime mkoani Mara jana kujibu mashitaka yanayomkabili.
Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Yusto Ruboroga, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Casmir Kiria, alidai kuwa mshitakiwa alikutwa mjini Tarime akipiga picha miili ya watu wanne katiya watano waliouawa wakati wa uvamizi wa Mgodi wa North Mara Barrick bila kibali.
Mbali na maiti hao, Kiria alidai kuwa mshitakiwa pia alipiga picha majengo mbalimbali ya Serikali na Mgodi wa North Mara Barrick uliopo Nyamongo.
Kiria alidai kuwa kwa mara ya kwanza Joyceline aliingia nchini kama mtalii akitoka Uganda Mei Mosi mwaka huu na kurudi tena katika nchi hiyo lakini alirejea tena Tanzania Mei 22 mwaka huu, kupitia Kituo cha Uhamiaji Sirari Mpakani ambako alipita kwa mara ya kwanza.
Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa baada ya mshitakiwa kuingia tena wilayani Tarime, alionekana akiongozana na wafuasi wa Chadema huku akipiga picha mbalimbali za matukio na kuzituma nje ya nchi bila kibali na kamera zake zilikutwa na baadhi ya picha hizo.
Mshitakiwa huyo Joyceline alikri kosa lake la kuingia nchini na kufanya kazi ya kupiga picha bila kibali cha Serikali na kujitetea kuwa hakujua kama alikuwa akifanya kosa la jinai.
"Maofisa Uhamiaji wa Kituo cha Sirari ambapo nimekuwa nikipita kwa mara ya pili sasa hawakuwahi kunipa maelekezo kuwa kupiga picha bila kibali ni kosa la jinai, ninakiri kosa hilo na ninaomba msamaha," alijitetea.
Hata hivyo Kiria alimwomba Hakimu Ruboroga kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa, ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaoingia katika nchi zingine na kuanza kuchukua picha bila kibali cha nchi husika.
Katika hukumu yake, Hakimu Ruboroga alisema mbali na kuomba msamaha, mshitakiwa Joyceline atatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh. 50,000.
Baada ya hukumu hiyo, Joyceline alilipa faini hiyo na kukabidhiwa kwa maofisa wa Uhamiaji kwa hatua zaidi za Uhamiaji.
Hata hivyo akiongea na gazeti hili baada ya kuachiwa huru Joycelin, alisema yeye ni mwandishi wa kimataifa na amekuwa akifuatilia migogoro kama ule wa Nyamongo.
Alisema kabla ya kuingia Tanzania, alikuwa nchini Uganda.Katika hatua nyingine, wenyeviti wa vijiji vya Kewanja, Matongo na Nyangoto, wilayani Tarime wamelalamikia uamuzi wa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Constantine Massawe wa kuwanyang'anya bastola walizokuwa wakizimiliki kihalali.
Viongozi hao ambao vijiji vyao vinazunguka mgodi wa African Barrick wa North Mara, walisema uamuzi huo ulifanywa Mei 5 maka huu kufuatia kile kilichodaiwa na polisi kuwa zingetumika katika vurugu za koo.
Wenyeviti waliolalamikia hatua hiyo ni Elisha Nyamhanga wa Kijiji cha Nyangoto, Daud Itembe wa Matongo na O'Mtima Tanzania wa Kewanja.Walidai kuwa maelezo na hatua hizo hazikuwatendea haki hasa ikizingatiwa kuwa watu wanaomiliki silaha kihalali ni wengi.
"Massawe alitutaka twende ofisini kwake na silaha zetu na vibali, tulipofika silaha hizo zilichukuliwa kwa madai kuwa taarifa za kiintelijensia zinaonyesha hali ya amani si nzuri na kuwa vurugu za koo zingeibuka na huenda silaha zao zingetumika," alisema mmoja wa viongozi hao.
0 comments