TANESCO YATANGAZA KUREJESHA RATIBA YA KAWAIDA
HATIMAYE mgawo mkali wa umeme uliolitikisa taifa kwa takriban wiki moja umemalizika na sasa taifa limerejeshwa kwenye ratiba ya kawaida ya mgawo wa awali.
Taarifa rasmi iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Shirika la Umeme (TANESCO) kwa vyombo vya habari imethibitisha kupungua kwa mgawo huo.
“TANESCO inapenda kuwaarifu wateja wake na wananchi kwa ujumla kuwa upatikanaji umeme nchini umerejea katika hali ya kawaida kutokana na kukamilika kwa wakati kwa matengenezo ya visima vya kuzalisha gesi asili katika kisiwa cha Songosongo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Ilieleza kuwa visima hivyo vilikuwa katika matengenezo kuanzia tarehe 19 hadi 26 Mei mwaka huu, hivyo kupelekea upungufu mkubwa wa umeme katika Gridi ya Taifa ambao uliwaathiri watumiaji umeme wote walioungwa katika Gridi ya Taifa.
Ilifafanua kuwa upungufu huo wa umeme ulitokana na visima na mitambo ya gesi asili iliyopo katika kisiwa cha Songo Songo, mkoani Lindi, kuzimwa na wamiliki wake ambao ni kampuni ya “Pan African Energy Tanzania Limited” kwa ajili ya ukaguzi na ukarabati.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, lengo la ukarabati huo lilikuwa kuboresha viwango vya gesi inayozalishwa na kusafirishwa kutoka kisiwa hicho hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kufua umeme na kutumiwa viwandani.
Vituo ambavyo hutumia gesi asili ya Songosongo kuzalisha umeme ni Songas, Ubungo Gas Plant na Tegeta Gas Plant. Umeme wa gesi huchangia karibu nusu ya umeme unaofuliwa kwenye vituo vyote nchini.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilieleza kuwa kina cha maji kwenye bwawa kuu la Mtera bado kipo chini sana na hakiridhishi, hasa kutokana na msimu wa mvua kukaribia kumalizika.
“Leo hii Mei 26, 2011 kina cha maji kwenye bwawa la Mtera ni mita 691.08 juu ya usawa wa bahari. Kina cha juu kwenye bwawa hilo ni mita 698.50 na kina cha chini ni mita 690.00, juu ya usawa wa bahari. Tunaomba wateja warudi katika ratiba ya mgawo wa kwanza.
Hivyo basi kutokana na kina cha Mtera kuwa chini shirika litaendelea na mgao wa MW 182.
“Tunashukuru wateja na wananchi kwa ushirikiano na uvumilivu waliouonyesha katika kipindi chote cha mgawo,” ilisema sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya TANESCO.
Ngeleja aipigia debe kampuni ya mitambo
Wakati huohuo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, amelitaka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kufanya mawasiliano na kampuni ya General Electric (GE) inayojishughulisha na utengenezaji wa mitambo ya kufua umeme ili kupata mitambo ya kuzalisha umeme nchini.
Alitoa rai hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya General Electric (GE), John Rice, aliyekwenda ofisini kwake kujitambulisha na kuzungumzia fursa ambazo kampuni hiyo inaweza kuwekeza katika sekta ya nishati nchini.
Kwa mujibu wa Ngeleja TANESCO haina budi kuchangamkia fursa hiyo hivyo kufanya maamuzi ya kununua au kwa kukodi mitambo hiyo kwa kadri itakavyoona inafaa.
Makamu mwenyekiti huyo alimweleza waziri huyo kuwa mitambo inayotengenezwa na kampuni hiyo ni ile ya kutumia mafuta ya taa, dizeli, gesi asili, upepo, jua na joto ardhi (eothermal) kwa ajili ya kufua umeme.
Pia inajishughulisha katika uwekezaji wa miundombinu ya kusafisha na kusafirisha gesi na akabainisha kuwa wako tayari kuanza kufanya kazi hiyo mara moja endapo watafanya mazungumzo na serikali ama kupitia Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) na kukubaliana kama kutakuwa na mahitaji ya mitambo ya aina hiyo.
“Tuko tayari kuja kuwekeza Tanzania kwani tuna uzoefu wa kutosha na tumewekeza katika nchi mbalimbali ulimwenguni na kwa hivi sasa tunatarajia kuwekeza nchini Kenya ambapo tayari mazungumzo yameanza na serikali ya nchi hiyo,” alisema Rice.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO), William Mhando, alimhakikishia Waziri huyo wa Nishati na Madini kufanya mawasiliano zaidi na kampuni hiyo haraka iwezekanavyo ili kuwa na mpangilio madhubuti zaidi.
TGNP yataka TANESCO iimarishwe, Ngeleja ajizulu
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeitaka serikali kutenga pesa katika bajeti yake ya mwaka wa fedha utakaoanza Julai mwaka 2011/2012 hadi 2015/16 katika kuliimarisha shirika la umeme nchini (TANESCO).
Katika taarifa yao iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na kusainiwa na mkurugenzi mtendaji wa mtandao huo, Usu Mallya, ilisema TANESCO itengewe pesa ili kuondokana na tatizo la ukodishaji mitambo ya uzalishaji umeme toka nje ya nchi.
“TANESCO itengewe pesa katika bajeti ijayo ili kuondokana na tatizo la ukodishaji mitambo ya uzalishaji umeme toka nje ya nchi, ambapo mara kwa mara mitambo hiyo imekua ikiligharimu taifa kutokana na kuwepo kwa udanganyifu katika manunuzi na ukodishwaji wake,” alisema Usu katika taarifa hiyo.
Alisema, wameshangazwa na kusikitishwa kuona bado hakuna mkakati wa wazi au chanzo mbadala cha nishati kama vile gesi, upepo au makaa ya mawe kwa ajili ya kutatua changamoto iliyopo ya umeme.
Mkurugenzi huyo alisema kutokana na udhaifu huo, lazima kuwe na uwajibikaji kuanzia kwa Waziri wa Nishati na Madini hadi maafisa wengine wanaohusika na suala la nishati ya umeme hapa nchini.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alimtaka Waziri Ngeleja ajiuzuru, kwa kile alichoeleza kuwa kiongozi huyo ameshindwa kutumia vyanzo vya umeme vilivyopo kukabiliana na tatizo la nishati ya umeme linaloikumba taifa kwa miaka kadhaa sasa.
“Nchi yetu imejaliwa vyanzo vingi vya nishati ya umeme hasa katika maeneo ya maporomoko ya maji, yakitumiwa yote yanaweza kufua umeme wenye megawati 5,000 ukilinganisha na uwezo wa sasa wa umeme wa maji wa megawati 562, umeme wa gridi ya taifa ya megawati 791,” alisema Lipumba.
Alisema makaa ya mawe ambayo yameshagunduliwa yanaweza kufua umeme wa maji wa megawati 1,000 kwa zaidi ya miaka 50 ijayo sambamba na madini ya uranium yaliyogunduliwa katika wilaya za Namtumbo na Manyoni ambazo yanauwezo wa kufua nishati hiyo.
Alisema hata gharama za kufua umeme wa jua na upepo zimepungua na zinaendelea kupungua na kwamba Tanzania ina maeneo mengi ya kuweza kufua umeme wa solar na kwa kutumia upepo.
Alisema miaka 50 baada ya uhuru, nchi haina sababu za msingi za kukosa umeme huku akisisitiza kuwa ombwe la uongozi na ufisadi ndani ya CCM na serikali zake ndiyo chanzo kikuu.
“Serikali ya CCM na Waziri Ngeleja wameshindwa kutatua tatizo hili na kuisababishia nchi kupata hasara kubwa kwa kudhoofisha uchumi wa nchi hali iliyozorotesha uzalishaji viwandani na biashara, huduma za mahospitalini, katika sekta ya elimu na upatikanaji wa maji,” alisema Lipumba.
0 comments