Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Maofisa wa JWTZ watua Samunge

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MAOFISA 12 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wakiongozwa na Mkuu wa Kikosi cha Ardhini, Meja Jenerali Winjos Kisamba jana, walifika wilayani Ngorongoro kukagua hali ya mipaka na usalama kutokana na wimbi la watu kutoka ndani na nje ya nchi kuingia wilayani hapa kwa wingi.

Maofisa hao wa jeshi waliwasili juzi jioni na jana kabla ya kuanza kazi ya ukaguzi, walikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngorongoro. Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali, alithibitisha ujio wa maofisa hao na kusema watafanya kazi ya kukagua mipaka.

 "Ni kweli kuna maofisa wa JWTZ wamekuja ila wapo katika majukumu yao ya kawaida kutazama hali ya mipaka ya nchi kwa wilaya hii," alisema Lali. Maofisa hao, jana jioni walitarajiwa kufika Samunge kujionea hali ya eneo hilo inakotolewa tiba ya magonjwa sugu na Mchungaji Ambikile Mwasapila.

Ujio wao umetokana na taarifa kwamba baadhi ya watu wanaoingia nchini wapo wanaotumia njia za panya.
Wageni wengi wa Kenya wamekuwa wakiingia Samunge kwa malori licha ya magari hayo kupigwa marufuku kupeleka wagonjwa. Malori aina ya Mitsubishi Fuso zaidi ya matano yakiwa na abiria wapatao 300 yalifika Samunge jana.

Kijiji cha Samunge chaanza kukusanya mapato
Serikali ya Kijiji cha Samunge jana ilianza rasmi kukusanya mapato baada ya kupita siku mbili bila ya magari na helikopta kulipiwa.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Samunge, Michael Lengume alisema kuwa fedha zote zitakazokusanywa, zitapekekwa benki."Tumeanza kazi leo (jana) na fedha zetu Sh2,000 tutazitumia kwa shughuli mbalimbali na Sh3,000 tutawapa halmashauri kwa ajili ya kupeleka kwenye vituo vya uratibu," alisema Lengume.

Mgogoro wa maku-baina ya Kijiji cha Samunge na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ulidumu kwa muda mrefu na hatimaye wiki iliyopita ulimalizika baada ya jukumu hilo kuachiwa kijiji hicho. Kila gari linatozwa Sh5,000 na helikopta Sh150,000.

Mchungaji Mwasapila apewa tuzo
Kampuni ya ENSOL (T) LTD, jana ilimkabidhi tuzo ya kutambua kazi ya kutoa tiba, inayofanywa na Mchungaji Mwasapila kwa gharama ndogo.Meneja Masoko na Mauzo wa kampuni hiyo, Godwin Msigwa alimkabidhi Mchungaji Mwasapila tuzo hiyo muda mfupi baada ya kukamilisha kazi ya kumwekea umeme wa jua juzi.

Msigwa alisema kampuni ya Ensol yenye makao makuu yake Dar es Salaam, imetoa tuzo hiyo kutokana na kuthamini mchango wa Mchungaji Mwasapila katika sekta ya afya.Alisema wamefunga umeme huo kutokana na ushirikiano mkubwa waliopewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

0 comments

Post a Comment