Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Chadema wasusia bajeti , CCM, CUF waipitisha

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MADIWANI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana walisusia Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, kilichokuwa mahususi kwa ajili ya kupitisha bajeti ya maendeleo ya wilaya hiyo kwa mwaka 2011/2012.

Madiwani wa kata sita za Kasamwa, Katoro, Kagu, Kamhanga na Kalangalala walisusia kikao hicho na kulazimika kuondoka wakati kikao kikiendelea na kuwaacha madiwani wa vyama vya CCM na CUF wakiendelea na kupitisha bajeti hiyo.

Wakitoa sababu kubwa ya kususia kupitisha bajeti hiyo, baadhi ya madiwani hao walieleza kuwa kanuni mahsusi zinazohusika na upitishaji wa bajeti hiyo zimekiukwa, ambapo Diwani wa Kata ya Kalangalala, Peter Donald alisema kanuni za halmashauri zinataka madiwani kupatiwa makabrasha ya bajeti siku saba kabla ya kikao lakini wao wamepatiwa makabrasha hayo siku moja kabla ya kikao.

“Kanuni zinataka sisi madiwani kupata makabrasha siku saba kabla ya kikao ili kutuwezesha kuyapitia, lakini makabrasha haya sisi tumepewa jana…hivi kwa mahesabu ya haraka haraka hamuoni kwanza kwamba kanuni zimekiukwa, lakini pili hii ni mojawapo ya njia ya kutaka kutuburuza katika upitishaji wa bajeti hii…,’’ alisema diwani huyo.

Hoja hiyo iliungwa mkono na madiwani wengine wa chama hicho ambapo ilimlazimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Benson Tatala kueleza kwamba pamoja na kanuni kutaka hivyo, lakini tayari madiwani hao walikwishapitisha bajeti hiyo kwenye vikao vyao vya kamati.

“Waheshimiwa wajumbe bajeti hii tunayokuja kuijadili na kuipitisha hapa leo hii ni sisi hawa hawa ambao tumekaa na kuitengeneza na kuipitisha kwenye kamati zetu sasa hili la siku saba kabla ya kikao ni lingine lakini tunaamini kwamba kila kitu kiko sawa naomba tuendelee na kikao…’’.

Baada ya maelezo hayo madiwani wote walianza kuchangia na kuibuka pande mbili ambapo upande mmoja ulikuwa ukitaka kikao kisifanyike na mwingine ukitaka kifanyike na hivyo kuzusha mabishano makali hatua iliyosababisha hoja ya kura kupigwa ili kupata washindi ikaamriwa ambapo baada ya kura kupigwa madiwani waliotaka kikao kufanyika walishinda.

Ushindi huo uliwafanya madiwani wa Chadema kutoka ndani ya ukumbi huo na kuwaacha wenzao wa vyama vingine vya CCM na CUF wakiendelea na kikao ambapo baadaye walipitisha bajeti hiyo kwa kishindo.

Katibu Msaidizi wa Chadema wilayani Geita, Amos Nyanda alisema kwamba kwa kuwa Wabunge wao wamekuwa wakitumia staili ya kutoka ndani ya Bunge katika kufikisha ujumbe wao na hasa pale ambapo madai yao yanaonekana kupuuzwa, nao kama madiwani wameamua kutumia staili hiyo ili kufikisha ujumbe wao kwa serikali pamoja na watendaji wa serikali.
“Ndio tumetoka ndani ya ukumbi kupinga kanuni kukiukwa….hatuwezi kuendelea kupitisha bajeti yenye maslahi ya viongozi na si wananchi, lakini hatuishii hapa tu tunakwenda mbali zaidi na baada ya hapa tutahakikisha kwamba tunakwenda kwa wananchi na kuwaambia ukweli juu ya bajeti hiyo, ni lazima tuwachongee…’’ alisema Katibu huyo.

Hata hivyo alipoulizwa kwamba ni kwanini madiwani wao wamegomea kupitisha bajeti hiyo sababu ikiwa ni kucheleweshewa makabrasha wakati wao ni miongoni mwa wajumbe wa kamati zilizoketi na kuandaa bajeti hiyo na kupitisha kwenye kamati zao, alisema hawezi kujibu swali hilo isipokuwa ni madiwani wenyewe.

Kwa upande wake Katibu wa CUF wilayani Geita, Severine Malugu aliwaponda madiwani wa Chadema kwa kukimbia kikao hicho cha bajeti kwa madai kuwa huo bado ni uchanga wa kisiasa ndio umewafanya kususia kikao, huku akibainisha kwamba mwanasiasa aliyekomaa siku zote anapigana hadi dakika za mwisho na hata akishindwa basi anakubali matokeo na kujipanga upya.

0 comments

Post a Comment