Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Waziri:Waliochana Muswada wahuni

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan amesema, watu waliochana muswada wa sheria itakayosimamia mchakato wa kukusanya maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Tanzania ni wahuni.

Waziri Samia amesema, kitendo kilichofanywa Zanzibar si tabia ya Wazanzibari na kwamba, waliofanya hivyo ni kundi la wahuni.

“Kwa hiyo wamejumuika, wamekuja kufanya uhuni wao pale” amesema Waziri huyo wakati anazungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge mjini Dodoma.

“Ile isichukuliwe kuwa ni tabia ya Wazanzibari kwa kuwa wamesema vile” amesema na akabainisha kuwa, kilichotokea ni tofauti ya mawazo na mitazamo miongoni mwa wananchi.

Waziri Samia ameyasema hayo wakati anazungumzia mafanikio na changamoto za muungano wa Tanganyika na Zanzibar wakati huu unapokaribia kutimiza miaka 47.

Amesema, Muungano huo ni imara lakini kuna vikwazo katika utekelezaji wa Sheria ya Muungano.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, viongozi wa Zanzibar na Tanzania Bara wamekubaliana kuwasilisha miswada Katika Bunge na Baraza la Wawakilishi Oktoba mwaka huu ili kuondoa utata wa kisheria uliopo kati ya pande hizo.

“Kuwa na mfumo tofauti wa sheria kwa pande mbili za muungano hukwamisha utekelezaj i wa baadhi ya maamuzi yanayofikiwa katika kutatua vikwazo vya muungano, mfano katika masuala ya usajili wa magari n.k” amesema.

Amesema, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa zikishirikiana kuondoa vikwazo ili muungano uendelee kuwa imara na uwe na faida kwa wananchi wa pande zote.

Amewaeleza waandishi wa habari kuwa, tangu mwaka 2006 vimefanyika vikao sita vya kamati ya pamoja ya Serikali ya Muungano na SMZ, na kwamba, vikao hivyo vilitanguliwa na vikao vya mawaziri, makatibu wakuu na wataalamu wa kisekta kutoka serikali zote mbili.

Amesema, hoja 13 ziliwasilishwa na kujadiliwa, mbili zimetatuliwa, zikaandaliwa hati za makubaliano, mawaziri wa serikali zote mbili walizisaini Juni 2 mwaka jana mjini Zanzibar.

Samia amesema, hoja nne zimepatiwa ufumbuzi ambazo ni mgawanyo wa mapato yanayotokana na misaada kutoka nje, misamaha ya mikopo ya fedha kutoka IMF, uwezo wa Zanzibar kukopa ndani na nje ya nchi, na malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili.

Amezitaja hoja zilizo katika hatua mbalimbali za kutafutiwa ufumbuzi kuwa ni ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili, uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa Bahari Kuu, ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje, na ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.

Hoja nyingine ni mgawanyo wa mapato yanayotokana na faida Benki Kuu na hisa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizokuwa katika bodi ya sarafu ya Afrika Mashariki.

Amesema, hoja nyingine inayotafutiwa ufumbuzi ni kodi nyinginezo ikiwemo Kodi ya Mapato, Kodi ya mapato inayozuiwa na usajili wa vyombo vya moto yakiwemo magari na pikipiki.

0 comments

Post a Comment