Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Wavulana wafanya kweli 'form six'

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
UFAULU wa mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka huu umepungua kwa asilimia moja ikilinganishwa na mwaka jana.

Wavulana wameibuka kidedea kwa kushika nafasi zote 10 bora. KWA MATOKEO KAMILI BOFYA HAPA

Pamoja na hayo, masomo ya Sayansi, Biashara na Hisabati ni miongoni mwa yaliyoongoza kwa kufaulisha wanafunzi wengi ikilinganishwa na Sayansi ya Jamii na Sanaa, huku wanafunzi wengi wakifeli zaidi katika masomo ya lugha za Kiswahili na Kiingereza.

Akisoma matokeo ya kidato cha sita ya mwaka huu Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Joyce Ndalichako, alisema , asilimia 87.24 ya wanafunzi waliofanya mtihani walifaulu mtihani huo, ikilinganishwa na asilimia 88.85 ya mwaka jana.

Hata hivyo waliofaulu kati ya daraja la kwanza na la tatu ni asilimia 78.53 tu ya waliofanya mtihani. Mchanganuo wa Necta unaonesha kuwa daraja la kwanza waliofaulu ni asilimia 7.25, daraja la pili (20.23%), daraja la tatu (51%), daraja la nne (13.51%) na waliopata sifuri ni asilimia 7.97 ya wanafunzi wote.

Kwa mtazamo huo, kwa vigezo vya awali vya wanafunzi watakaopata udhamini wa Serikali kuingia vyuo vikuu ni asilimia 27.48 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo kwa maana ya waliopata daraja la kwanza na la pili.

Tofauti na ilivyokuwa katika matokeo ya kidato cha nne, katika matokeo ya kidato cha sita sekondari za Serikali zimejitokeza zaidi kutoa wanafunzi bora.

Dk. Ndalichako aliwataja walioshika nafasi ya 10 bora katika mtihani huo kuwa ni Muhagachi Chacha wa Kibaha, Samweli Katwale (Mzumbe), Amiri Abdallah (Feza Boys), Aron Gerson na Shaban Omary wa Tabora Boys na Kudra Baruti (Feza Boys).

Wengine ni George Assenga wa Majengo Sekondari, Comman Nduru (Feza Boys), Francis Josephat (Tabora Boys) na George Felix (Mzumbe).

Kutokana na nafasi zote 10 bora kuchukuliwa na wanaume, Dk. Ndalichako alisema Necta ilitengeneza orodha maalumu ya 10 bora ya wasichana peke yao.

Katika orodha hiyo, wasichana walioongoza ni Doreen Kabuche wa Benjamin Mkapa, Rahabu Mwang’amba (Kilakala), Mary Moshi (Kifungilo Girls), Nuru Kipato (Marian Girls), Zainab Hassan (Al-Muntazir Islamic).

Nafasi ya sita kwa kundi hilo maalumu ilichukuliwa na Catherine Temu wa Ashira, Anthonia Lugomo (Usongwe), Cecilia Mville (Kifungilo Girls), Mariam Matovolwa (Kilakala) na Suzana Makoi (Tarakea).

Shule bora iliyoongoza kwa kufaulisha katika kundi la shule zenye wanafunzi zaidi ya 30 ni Marian Girls iliyofuatiwa na Feza Boys, Kifungilo, Kibaha, St Mary’s Mazinde, Ilboru, Tabora Boys, St Mary Goreti, Mzumbe na Mafinga Seminari.

Kundi la shule bora zenye wanafunzi chini ya 30, lilikuwa na shule nyingi za seminari zikiongozwa na Seminari za Uru, St James, Same, Maua na Dungunyi. Nyingine ni DCT Jubilee, Parane, St Joseph-Kilocha, Mlama na ya Wasichana Masama.

Somo lililoongoza kwa kufaulisha wanafunzi wengi ni Uchumi lililofaulisha asilimia 93 ya watahiniwa na kufuatiwa na Biashara (88.7%), Advanced Mathematics (81.5%), Kemia (80.3%), Fizikia (67.03%), Basic Applied Mathematics (50.69%) na Jiografia (9.65%).

Baraza limefuta mitihani ya watahiniwa 12 kutokana na udanganyifu kati yao watano ni wa shule na saba wa kujitegemea ambapo pia watahiniwa 218 matokeo yao yamesitishwa hadi watakapolipa ada ya mitihani.

0 comments

Post a Comment