Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Pengo avunja ukimya kuhusu uhusiano wa Katoliki na Serikali ya JK

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amezungumzia uhusiano wa kanisa hilo na Serikali, akikanusha tuhuma kwamba maaskofu wake wanatumiwa na mafisadi kumchafua Rais Jakaya Kikwete na familia yake.Kardinali Pengo alisema kuwa hakuna askofu yeyote wa kanisa hilo anayetumiwa na watuhumiwa wa ufisadi kumchafua Rais Kikwete na Serikali yake kama baadhi ya watu wanavyodai.

Kardinali Pengo alisema hayo jana katika Ibada ya Jumatatu ya Pasaka iliyofanyika katika Parokia Kristu Mfalme Tabata ikikutanisha pia kwaya zote za kanisa hilo jimboni humo.“Kanisa limeshtakiwa kuwa lipo kinyume na utawala uliopo madarakani hivi sasa na kuna uzushi kuwa eti maaskofu wake, wanawaandaa wapinzani kuchukua madaraka ya kuongoza taifa,” alisema Kardinali Pengo.

Kardinali Pengo alisema maneno hayo ni uzushi usiokuwa na msingi kwani kanisa hilo halina na halipaswi kuwa na upande wowote katika masuala ya utawala wa dunia.Alisema kauli hizo alizodai za uzushi, ni hatari kwa kuwa zinalifanya kanisa hilo lionekane kuwa chombo cha kuziendeleza mamlaka za kisiasa au linapingana na watawala.

Akitumia maandiko ya matakatifu ya Biblia, Kardinali Pengo alisema kinachotokea sasa ni kama kilichotokea wakati wa Kristu katika utawala wa Herode, Yesu Kristu alishutumiwa kwa kula na kunywa na watoza ushuru.“Hata Yesu alipokuwa karibu na watoza ushuru, alionekana kama kibaraka wa utawala wa Rumi wakati huo na kuna ambao walimwona anakufuru kwa kushirikiana na watu hao ambao ni chukizo,” alisema Pengo.

Alisema kama ilivyokuwa kwa Kristu ambaye aliwajibu waliomchukia kuwa hakuja kwa ajili ya wenye haki bali wenye dhambi, Kanisa Katoliki halitawatenga wala kuwazuia makanisani wanasiasa watakaofukuzwa kwenye vyama vyao kwa tuhuma za ufisadi.

“Hatutamtenga mtu au kumzuia asije kanisani kisa tu amefukuzwa katika chama chake cha siasa,” alisema Kardinali Pengo na kuongeza:
"Kufanya hivyo ni  kuwanyima ya huduma za kiroho. Hata mimi siwezi kuacha kumwungamisha mtu ambaye amefukuzwa katika chama chake kwa sababu za ufisadi, kwani kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafundisho ya Yesu Kristu ambaye alikuja duniani kwa ajili ya wenye dhambi.

"Pengo alisema binafsi anasikia machache lakini waumini hao watakuwa wanasikia mengi kwa kuwa ndiyo waliopo mitaani na huko ndipo wanapogombea madaraka ya kisiasa.Alisema huyasikia yanapopelekwa kwake na walioshindwa kuyamaliza huko mtaani  na kwamba anaamini wanasikia mengi, lakini akasisitiza kwamba msimamo wa kanisa ni kuwa halitakuwa na upande katika utawala wa kidunia kama alivyokuwa Kristu.

“Litakuwa jambo baya sana na kwenda kinyume na mafundisho ya Kristu kama muumini wa namna hiyo atanifuata, halafu nikamweleza kuwa akanunue silaha,” alisema Pengo na kuongeza kuwa atamshauri kulingana na maandiko na si vinginevyo.Pengo aliwataka waumini wa kanisa hilo kutafakari na kuliombea taifa amani hasa katika kipindi hiki ambacho alikifananisha na nyakati za kuzaliwa kwa Yesu ambapo alituhumiwa, kusulubiwa, kifo chake hadi alipofufuka na kuendelea kulitangaza jina la Bwana.

Ingawa Askofu Pengo hakumtaja mtu wala taasisi inayotoa madai hayo dhidi ya Kanisa, Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye amewahidi kukaririwa na vyombo vya habari akidai kuwa baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa dini, wanatumiwa na mafisadi kwa ajili ya kumchafua Kikwete na Serikali yake kwa minajili ya kutaka kuingia madarakani.

Nape alitoa madai hayo Aprili 16, mwaka huu katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Bakhresa Manzese, Dar es Salaam.Alisema mafisadi wametangaza vita ya kumchafua mwenyekiti wa chama hicho na familia yake kupitia vyombo vya habari hata baadhi ya viongozi wa dini na makanisa.Nnauye alisema wamegundua mpango huo na kwamba wanatangaza kuamua kupambana nao hadi wang'oke ndani ya CCM.

0 comments

Post a Comment