MUSWADA wa Marejeo ya Katiba uliokuwa umewasi- lishwa katika hati ya dharura kwenye Mkutano wa Tatu wa Bunge unaoendelea mjini hapa kuna kila dalili kuwa huenda ukaondolewa.Habari zilizopatikana jana zimeeleza kwamba mbali ya muswada huo ambao sasa taarifa zinasema utawasilishwa Oktoba mwaka huu, hata ule wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ambao ulipangwa kupitishwa katika mkutano huu pia umeahirishwa mpaka Bunge lijalo.
Lengo la kuondoa miswada hiyo linaelezwa kuwa ni kutoa nafasi zaidi ya kuiboresha, huku habari zikieleza kwamba Muswada wa Marejeo ya Katiba unahitaji kuandikwa upya kwa kujumuisha maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali ambao walionyesha hofu ya namna ulivyoandikwa.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema: " Sijui ‘source’ (chanzo cha habari) yenu ni reliable (ya kuaminika) kiasi gani lakini mimi siwezi kuzungumzia hilo sasa. Utaratibu wangu wa kufanya kazi hauko hivyo, ila kama tutauondoa tutasema na kama hatutauondoa tutasema."
Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani naye alisema hakuwa na taarifa za kuondolewa kwa muswada huo huku akisisitiza kuwa upo mikononi mwa Bunge.
“Lengo letu ni kuunda Katiba itakayoshirikisha watu, Kamati ya Bunge imekusanya maoni kutoka kwa umma ambayo yatahusishwa kwenye muswada huo,” alisema Kombani.
Taarifa za kuondolewa kwa muswada huo bungeni zimekuja wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema kuwa nia ya Serikali kuendelea au kuuondoa bungeni muswada huo itategemea ushauri itakaoupata kutoka kwa Spika wa Bunge, baada ya kupitia mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala.
Akijibu maswali ya wabunge ya papo kwa hapo bungeni jana, Pinda alisema taarifa alizonazo ni kwamba kamati hiyo imeshakamilisha mchakato wa kukusanya maoni ya wadau na imewasilisha mapendekezo yake kwa Spika wa Bunge.
Alisema baada ya kamati hiyo kuwasilisha mapendekezo yake, Spika kwa kutumia wataalamu wake, atashauri iwapo muswada huo uendelee au usitishwe.Pinda alisema Serikali iliwasilisha muswada huo kwa hati ya dharura ikiwa na nia njema kwa sababu iliamini kwamba wananchi wana shauku kubwa ya kupata Katiba mpya haraka.
“Sasa baada ya kuwasilishwa bungeni, kilichopo ni utaratibu wa Bunge. Nimearifiwa kuwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, ilikwishakutana kuzungumzia yaliyojitokeza wakati wa public hearing (maoni ya wadau) walipokuwa wanakutana na Watanzania,” alisema.
Pinda alisema kwa utaratibu, inapaswa mapendekezo hayo kwenda kwa Spika, ambaye akishayapata na kuchambua, akiona inafaa kushauriana na Serikali, atafanya hivyo.
“Niliposimama hapa bado sijapata taarifa yoyote ya wamefikia wapi kwenye hatua hiyo. Kwa hiyo tumejipanga tukiamini kama tulivyoleta jambo hili bungeni, kama hakutakuwa na maoni tofauti tutaendelea nalo,” alisema Pinda na kuongeza:
“Lakini kama tukipata maoni hayo mengine kwa uzito stahiki, kama Serikali tutaridhia kwa kuwa nia ni njema. Nia ni kutaka tusonge mbele kwa namna ambayo Watanzania wote tutaridhia kwamba jambo hilo limekwenda vizuri.”
Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali la Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali juu ya maoni ya wadau waliyoyatoa kwenye Kamati ya Bunge.
“Katiba ni roho ya Taifa na kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya mabadiliko ya Katiba au kuandikwa upya kutoka kwa wananchi, jambo ambalo Serikali imeridhia kupitia kwa Rais, kwa sababu Serikali imeleta muswada katika utaratibu wa haraka, muswada wa constitutional review,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Je, baada ya Serikali kuona 'reaction' ya wadau mbalimbali wakiwamo wanazuoni, vyama vya siasa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambao wanaona mchakato huu ulikuwa unakwenda kwenye kasi ambayo badala ya kujenga inaweza ikatia nyufa katika nyumba yetu. Ni kwa nini Serikali kupitia Waziri Mkuu isitoe tamko rasmi pengine la kukubaliana na utashi wa wadau?”
Mbowe pia alimtaka Waziri Mkuu kutumia fursa hiyo kulieleza taifa kukubaliana na mawazo ya wadau na kuondoa muswada huo kwa kile alichoeleza kuwa suala hilo limezua hofu kubwa kwa taifa kutokana na uzito wake.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema: “Na mimi ni Mtanzania kama wewe na kwa dhamira nzuri tuliyonayo nitaonekana mtu wa ajabu sana iwapo ushauri nitakaopata kutoka kwa Spika niupuuze, niseme naendelea. Siwezi kufanya hivyo.”
Katika kipindi hicho cha maswali, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alitaka kujua iwapo Waziri Mkuu yuko tayari kuzungumzia kashfa ya Meremeta na Tangold, baada ya Rais Jakaya Kikwete kutamka kuwa CCM imeamua kujivua gamba la ufisadi.
“Baada ya kauli hii ya Rais na dhamira hii ya kujivua gamba masuala ya ufisadi, uko tayari kutaja wahusika wa Makampuni ya Meremeta na Serikali kuchukua hatua zinazostahili?” aliuliza.
Hata hivyo, Pinda alikataa kuwataja wahusika hao kwa kile alichoeleza kuwa suala hilo limejengwa kwenye misingi tofauti.
“...Hapo umepandia rafiki yangu, yaliyofanyika ndani ya Chama Cha Mapinduzi, kinashughulika na wanachama wake...chama kizuri lazima muwe na utaratibu wa kujikosoa, kama ulisikia vizuri mwenyekiti wetu alisema tutaendeleza hizo juhudi kwa lengo la kujenga chama kilicho imara kinachokubalika, ili tukifika 2015 tuweze kuwashinda kwa mara nyingine,” alisema Pinda na kuongeza:
“Suala la Meremeta ni jambo tofauti kabisa, pengine sipo katika nafasi ya kuweza kulizungumzia kama unavyotaka nizungumzie kwa sababu ni jambo jingine ambalo lina misingi tofauti sana.”
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema aliyetaka kujua kutotekelezwa kwa tamko la Serikali kuhusu bei ya sukari, Pinda alisema wameelekeza halmashauri kusimamia agizo la Serikali kuwadhibiti wauzaji wadogo wadogo, ambao wameonekana kuwa chanzo cha kupanda kwa bei hiyo... “Tumelazimika kuomba halmashauri zetu zijaribu kuwabana hawa wauzaji wadogo,” alisema
0 comments