MABADILIKO makubwa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) yamefanyika baada ya wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho kujiuzulu.
Kutokana na hali hiyo, huenda Kamati Kuu nayo ikajiuzulu na kubakiwa na Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete, Spika wa Bunge, Anna Makinda ambao wanaingia kwa nafasi zao na John Malecela ambaye ni Mjumbe wa Kudumu.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM iliyokutana mjini Dodoma jana, zinaeleza kuwa hatua hiyo inatokana na mgawanyiko uliokikumba chama hicho.
Hatua hiyo ya kujiuzulu kwa wajumbe wa nafasi nyeti ya chama hicho, inakuja miezi mwili baada ya Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Jakaya Kikwete kueleza wazi kuwa chama kinahitaji kujivua gamba ili kiweze kurejesha heshima yake.
Akihutubia kilele cha maadhimisho ya siku ya kuzaliwa CCM, mjini Dodoma Februari 5 mwaka huu, Rais Kikwete alisema chama hicho kinahitaji mabadiliko makubwa kiweze kurejesha hadhi yake.
Wajumbe waliojiuzulu ni Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba ambaye ni mwenyekiti, manaibu makatibu wakuu wa CCM Bara na Visiwani, George Mkuchika na Saleh Ramadhan Feruzi na Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati.
Wengine ni Katibu wa Uchumi na Fedha, Amos Makala, Katibu wa Mipango, Kidawa Saleh na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mambo ya Nje, Bernard Membe.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili imezipata jana usiku zilieleza kwamba Makamba aliwasilisha barua yake kwa kuiweka kwenye meza ya mwenyekiti kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma.
Taarifa hizo zinasema kuwa baada ya kuwasilisha barua hiyo, Makamba aliomba ruhusa ya kuondoka kwa maelezo kuwa amepata msiba nyumbani kwao Tanga.
Hata hivyo, wajumbe wa kamati hiyo walikataa kutokana na umuhimu wake kwenye kikao hicho, hivyo wakamweleza kuwa atume mwakilishi kwenye msiba.
Habari zaidi zinasema, Makamba amemtuma mwanaye, Januari Makamba ambaye ni mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga kwenda kumwakilisha kwenye msiba huo.
Awali wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC-CCM), waliendelea kuvutana na kusababisha kuahirishwa kwa Mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho kilichokuwa kianze jana.
Kikao cha CC ambacho kilianza juzi jioni kilitarajiwa kumalizika usiku wa siku hiyo na jana kilikuwa kifanyike kikao cha NEC, ajenda kuu ikiwa ni kujadili tathmini ya uchaguzi mkuu uliopita.
Hata hivyo, Kamati Kuu iliyoanza kikao saa 10 jioni juzi, iliahirisha kikao chake saa 1:00 usiku na kurejea tena saa 3:00 hadi saa 5:00 usiku, bila kumaliza kupanga ajenda za NEC.
Wajumbe wa NEC walianza kukusanyika asubuhi jana katika Makao Makuu ya CCM, baadaye walitakiwa kurudi tena saa 7:00 mchana, lakini waliporejea walitakiwa kurudi tena saa 10:00 jioni, pia walitakiwa kurejea leo saa 3:00 asubuhi.
Kuahirishwa kwa kikao cha NEC, kulidaiwa kuwa kumetokana na CC kutomaliza kuandaa ajenda za kikao hicho.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zilidai kuwa hatua ya kuahirishwa kwa kikao hicho ilitokana na kuwepo kwa mvutano mkali kati ya wajumbe wa CC, wakitaka baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wajiuzulu ili kukinusuru chama kutokana na tuhuma mbalimbali kinazobebeshwa na kuharibu taswira yake.
Kundi hilo linadai pia kuwa kama wajumbe hao watatoswa watakuwa wamewanyima Chadema ajenda mbele ya wananchi, lakini kundi jingine linalowaunga mkono likipinga mapendekezo hayo.
Baadhi ya wenyeviti wa mikoa wa CCM, wanaunga mkono kundi hilo la watuhumiwa lilikuwa likikutana kwenye hoteli moja, wakihaha kuhakikisha ajenda hiyo inazimwa.
Katika mkutano huo, inadaiwa ajenda nyingine iliyokuwa na mvutano zaidi ni ya Muswada wa Sheria ya Kubadilisha Katiba wa 2011 ambapo katika kikao hicho Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema pia alihudhuria.
Wanaotajwa kurithi nafasi ya Makamba ni, Balozi wa Tanzania nchini Russia, Jaka Mwambi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Kanali Abdulrahman Kinana, ambaye anadaiwa anaweza kukinusuru chama hicho na mgawanyiko uliopo, anadaiwa kukataa nafasi hiyo baada ya kuombwa na mwenyekiti. Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa amekubali kuwa Naibu Katibu Mkuu.
Mwingine anayetajwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, lakini anahukumiwa na historia yake ya kuhama chama hicho kwenda NCCR-Mageuzi mwaka 1995.
Kikao hicho kinadaiwa pia kujadili matamshi ya kejeli na matusi yaliyotolewa na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) dhidi ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kuwa yanakigharimu chama.
“Kama kuna kitu kimetugharimu kichama ni kauli za UVCCM, huwezi ukabeza mchango wa Frederick Sumaye. Huyu amelitumikia taifa na chama kwa muda wa mrefu,” kilisema chanzo chetu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati, alisema ngoma bado ni nzito na kuwataka wajumbe wa Nec kuwapo kwa ajili ya kikao leo saa 5:00 asubuhi.
Hata hivyo, Chiligati alikataa kutaja ajenda zilizokuwa zikijadiliwa kupelekwa NEC na kuahidi kuzitaja kwa waandishi wa habari leo saa 3:00 asubuhi.
0 comments