Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Zanzibar wataka Tume huru ya uchaguzi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WADAU wa uchaguzi, hususani vyama vya siasa hapa Zanzibar, wametaka kuwepo kwa Tume ya Uchaguzi yenye mamlaka na itakayofanya kazi kwa ufanisi zaidi katika siku zijazo, na pia wameiomba serikali na nchi wahisani kusaidia kifedha wakati wa uchaguzi.

Wakitoa maoni yao na tathmini ya utendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) katika uchaguzi wa mwaka jana, vyama vya siasa vimesema kuwa pamoja na kuwa uchaguzi mkuu ulifanyika vizuri, lakini walibainisha udhaifu wa ZEC katika kusimamia uchaguzi.

"Tunataka Tume ya Uchaguzi ambayo inaweza kuwa na mamlaka kwa viongozi wa mikoa, polisi, na mamlaka yoyote kama watavuruga uchaguzi kama vile kuvikatalia vyama vya siasa maeneo ya kufanyika kampeni.

Tunataka serikali kutenga fedha hata kama ni asilimia moja ya bajeti ya ZEC kwa ajili ya kusaidia vyama vidogo vya siasa’,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AFP), Soud Saidi Saidi na kuongeza:

"ZEC haina meno, tunawataka watunga sera na serikali kuiwezesha Tume ya Uchaguzi ili iweze kufanya kazi zaidi kwa kujitegemea katika kusimamia masuala yote yanayohusu uchaguzi, angalau wakati wa kipindi cha uchaguzi”.

Katibu Mkuu wa Chama cha TADEA, Juma Ali Khatib, alisema katika mkutano wa tathmini ya uchaguzi ulioandaliwa na ZEC kwa kushirikiana na UNDP, uliofanyika kwenye Hoteli ya Zanzibar Ocean View kuwa ZEC inahitaji msaada wa kisheria katika kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu.

Vyama vya siasa vikiwamo AFP, TADEA, UMD, UPDP vimeungana pamoja katika kushawishi kwa ajili ya kuweka usawa katika uwanja wa siasa wakati wa uchaguzi kama vile kusaidia vyama vyote vya siasa katika gharama za uchaguzi, “bila kuvisaidia vyama vidogo, hatuwezi kuwa na ndoto ya kushinda hata kiti kimoja cha ubunge”.

“Tunatoa wito kwa kuwapo mageuzi makubwa katika sheria kabla ya uchaguzi ujao (2015). Muda mfupi kabla ya uchaguzi, wabunge wote wanalipwa mamilioni ya fedha kama ‘kiinua mgongo’, hivyo ni ngumu kwa mgombea mpya kumshinda mtu ambaye ana fedha za kutosha katika akaunti yake,” alisema Khatib.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mwenyekiti wa ZEC, Khatib Mwinyichande aliwataka wadau vikiwemo vyombo vya habari, wanasiasa na mashirika ya kijamii kutoa tathmini ya kujenga kwa lengo la kuboresha Tume ya Uchaguzi.

"Maoni yangu yatasaidia kuiboresha Tume. Tunataka kuhakikisha kwamba uchaguzi usiwe chanzo cha kuanzisha vurugu visiwani humu. Ndiyo tunaweza, kufanya uchaguzi wa amani, huru na wa haki katika chaguzi zote zijazo. Sote tunahitaji kuwa makini, ukweli, uwazi na haki, "alisema Mwinyichande.

Ofisa Mwandamizi kutoka UNDP, Hamida Ali Kibwana, alisema, ingawa Mradi wa Kusaidi Uchaguzi (ESP) wa UNDP unafikia mwisho Mei mwaka huu, taasisi inatakiwa kuwashirikisha wadau katika kutoa mapendekezo muhimu kwa ajili ya uchaguzi ujao.

"Ninawapongeza wote kwa kufanya uchaguzi wa amani na kwa aliyeshindwa katika nafasi ya urais kukubali matokeo. Hii ni nzuri kwa nchi yenu na kile kinachoendelea Ivory Coast, Zimbabwe na Kenya juu ya matokeo ya uchaguzi si kizuri kwa maendeleo ya Afrika," alisema.
Tags:

0 comments

Post a Comment