Dr. Magufuli alipokula Shahada ya Udaktari wa Falsafa |
Hatua hiyo ya Pinda ilitangazwa jana wakati akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara mjini Chato ambapo pamoja na kumsifu, alimwagiza Waziri wa Ujenzi, John Magufuli aliyejitwalia sifa katika kutekeleza majukumu yake kusimamia agizo hilo.
Januari 13, mwaka huu Magufuli alitoa Ilani kwa wananchi waliojenga nyumba ndani hifadhi ya barabara kuanza kubomoa nyumba hizo mapema na kwamba wasitegemee kulipwa fidia.
Pia alimtaka Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na madiwani kujipanga na kuondoa nyumba zilizo katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya njia ya mabasi yaendayo kasi ili kuwawezesha makandarasi kuanza kazi hiyo.
Kutokana na amri ya Pinda huenda utekelezaji wa mradi huo wa mabasi yaendayo kasi ukachelewa kuanza kwani baadhi ya nyumba zinatakiwa kubomolewa ili kupisha utekelezaji wake.
Waziri Magufuli amekuwa akisisitiza kwamba waliojenga ndani ya barabara wamevunja sheria namba 13 ya mwaka 2007 na kwamba hawastahili kulipwa fidia.
Hofu ya Pinda
Jana Pinda alisema kasi aliyoanza nayo Magufuli katika wizara yake mpya imeitisha serikali na kuwa ameagiza kusimamisha zoezi hilo mpaka litakapojadiliwa na Baraza la Mawaziri.
“Rais aliona kwenye barabara panalegalega na kumrudisha Magufuli kwenye wizara hiyo, huyu serikalini tunamwita ‘buldoza’ hata hivyo ameanza kwa speed kubwa na tumwemwagiza asimamishe zoezi hilo mpaka litakapojadiliwa na Baraza la Mawaziri,”alisema Pinda.
Alisema baraza hilo litakaa na kuangalia upya maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya bomoa bomoa na kusema kuwa kabla ya kuruhusu zoezi hilo kuendelea lazima wakubaliane kwanza kwenye Baraza la Mawaziri.
Akiwahutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara katika shule ya msingi Chato jana jioni Waziri Mkuu Pinda alisema inabidi pia itolewe elimu kwanza akidai maeneo mengine bomoa bomoa sio lazima.
Alisema zoezi hilo ambalo limezua malalamiko limesimamishwa na serikali kwa nia ya kujipanga upya, huku akisisitiza kuwa serikali inamwamini Waziri Magufuli kama kiongozi mwenye uwezo na ilimpa ofisi hiyo ili pia aweze kuwabana makandarasi wazembe.
Pia katika mkutano huo ambao awali Waziri Magufuli aliutumia kujifagilia kwa
kukiponda chama cha Chadema kilichofanya maandamano ya amani hivi karibuni wilaya kwake, Pinda alisema waziri huyo amekuwa akitumiwa kunyoosha mambo kwenye wizara zinazolega lega.
Kasi ya Magufuli ambayo pia inaonekana katika jimbo lake kwa nyumba nyingi zilizo katika hifadhi ya bara bara kuwekewa mkasi wa kuziondoa ilianzia katika ubomoaji wa ofisi za Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoa wa Dar es Salaam, zoezi ambalo alisema litaendelea kuyakumba majengo mengi ya serikali.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wanaoishi kando kando ya barabara ya Ubungo Maziwa hadi Kigogo tayari wamefungua kesi mahakamani kupinga kubomolewa bila fidia, ambapo mahakama imeweka zuio la kubomoa na keshokutwa Jumatano Mahakama Kuu itatoa uamuzi iwapo kesi hiyo iendelee au la wakati serikali itakapotoa maelezo yake.
Waziri mkuu amemaliza ziara yake jana wilayani Chato kwa kukagua miradi
mbalimbali ya maendeleo na leo Jumatatu anaengelea na ziara yake wilaya ya Biharamulo.
0 comments