Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mrema azidi kuibua 'madudu' Kilimanjaro. wafanyakazi Same wafyekwa mishahara

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Augustine Mrema imedai kugundua kuwapo kwa mtandao wa mafisadi ndani ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao unatetea ufisadi.

Mrema alisema kila wakati Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anapotoa taarifa ya wizi na ubadhirifu wa fedha katika baadhi ya halmashauri, mtandao huo hujenga mazingira ya kuwasafisha watuhumiwa.

Juzi, Kamati hiyo ikiwa Halmashauri ya Same iliagiza wakuu wa idara wa halmashauri hiyo wafyekwe asilimia 15 ya mishahara yao kutokana na utata kwenye fedha za umma.

“Tumegundua Mkoa Kilimanjaro una mtandao wa ufisadi yaani CAG anatoa taarifa ya wizi wa fedha za umma, ofisi ya mkoa nayo inaunda tena kamati ya kuchunguza na hatimaye kuwasafisha watuhumiwa,” alisema Mrema.

Msimamo huo wa kamati ulitokana na maelezo kuwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga waliotuhumiwa kwa wizi na ubadhirifu miaka ya 2004/05 na 2005/06 walirudisha kazini baada ya ‘kusafishwa’ na kamati hiyo.

Awali mkaguzi mkuu wa ndani Mkoa Kilimanjaro, Joseph Shirima aliiambia kamati kuwa ofisi ya CAG ndicho chombo kilichopewa mamlaka ya kikatiba ya kukagua hesabu za serikali na ndio yenye wataalamu wenye sifa hizo.

“Lakini tume hii iliyoundwa na mkoa kuja tena kufuatilia taarifa ya CAG ilikuwa na wajumbe ambao hawakuwa na sifa za mahesabu na badala yake watuhumiwa wakawaletea vielelezo batili na kuwasafisha,” alifafanua Shirima.

Katika tamko lake baada ya kukaa kama kamati, LAAC imemtaka Waziri Mkuu kukomesha tabia iliyoanza kuota mizizi ya watumishi wa halmashauri wanaojihusisha na ufisadi kusuka mipango ya kuhamishiwa halmashauri nyingine.

Pia kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Mrema imemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Willy Njau kuwakata watumishi wake jumla ya Sh25 milioni walizojilipa baada ya kujipandisha vyeo kinyemela.

Uamuzi huo wa kamati hiyo ya LAAC ulitolewa jana mjini hapa baada ya kupitia ripoti ya ukaguzi maalumu uliofanywa na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka ya 2004/05 na 2005/06.

Akisoma uamuzi huo wa kamati, Mrema alisema kamati yake imesikitishwa na hatua ya watumishi wanaotuhumiwa kwa wizi na ubadhirifu wa fedha za umma katika kipindi hicho kuhamishiwa halmashauri nyingine kuficha madhambi.

“Utaratibu wa mtumishi anaiba halmashauri moja, tena anatajwa kwa jina na cheo chake na CAG, matokeo yake anahamishiwa halmashauri nyingine, tunataka kumwambia Waziri Mkuu ,utaratibu huo ukomeshwe mara moja,” alisema Mrema.

Katika ripoti hiyo, CAG alibainisha malipo ya Sh25 milioni yaliyofanywa kwa watumishi sita wa halmashauri hiyo ambao ofisa utumishi aliwapandisha vyeo na kujilipa mishahara wasiyoistahili inayofikia Sh25 milioni.

“Kibaya zaidi watendaji waliohusika katika wizi na ubadhirifu huu ulioitia hasara serikali ya Sh25 milioni ambao ni mkurugenzi na ofisa utumishi walikula njama na kuhamishiwa halmashauri nyingine,” alilalamika Mrema.

Katika kikao hicho, ilibainika kuwa watendaji hao mbali na kuhusika katika ubadhirifu wa zaidi ya Sh50 milioni, lakini walilipotosha Baraza la Madiwani na kupitisha azimio la kuwarejesha kazini watumishi waliohusika na wizi.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo, Zabein Mhita, Subira Mgallu na Susan Kiwanga walionyesha wasiwasi wao jinsi CAG anavyoingiliwa katika utendaji wake wa kazi kiasi kwamba wapo wanaopinga ripoti yake nje ya utaratibu.
Tags:

0 comments

Post a Comment